Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mbele) na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Profesa Justin Ntalikwa (kushoto kwa Waziri) wakiwa katika kikao cha pamoja na Ubalozi wa Canada na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Taasisi zake.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mbele) akishuhudia Balozi wa Canada nchini Tanzania, Alexandre Leveque akitia saini kitabu cha Wageni mara alipofika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Kansela Siasa, Uchumi, Masuala ya umma kutoka Ubalozi wa Canada nchini, Theressa de Haan.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), Balozi wa Canada nchini Tanzania, Alexandre Leveque (kulia kwa Waziri) na Kansela Siasa, Uchumi, Masuala ya umma, Theressa de Haan wakiwa wakiwa katika picha ya pamoja jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiwa na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Alexandre Leveque katika picha ya pamoja ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Na Rhoda James.
Serikali imesema inakaribisha kampuni mbalimbali kutoka nchini Canada ili kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini lengo likiwa ni kuongeza kiwango cha umeme.
Wito huo umetolewa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokutana na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Alexandre Leveque. “Tunataka kiwango cha umeme nchini kiongezeke mara mbili ya kiwango kilichopo sasa,” alisema Profesa Muhongo.
Aliongeza kwamba bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam lina matoleo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo wilayani Mkuranga ambapo linaweza kuzalisha si chini ya megawati 2000. “Tunahitaji mwekezaji makini ambaye ataweza kuwekeza kwenye eneo hilo,” alisema Profesa Muhongo.
Profesa Muhongo alisema kuwa tayari ameshafanya mazungumzo na makampuni mbalimbali duniani kwa ajili ya kuwekeza kwenye nishati ya umeme na kwamba bado anaendelea kutafuta makampuni makini ya ndani na nje ya nchi ili Tanzania iweze kuwa na nishati ya uhakika.
Kwa upande wa Sekta ya Madini Profesa Muhongo alisema kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo katika masuala mbalimbali ikiwemo utoaji wa ruzuku na mafunzo ya uchimbaji bora wenye tija.
Alisisitiza kwamba lengo la Serikali ni kuwakomboa wachimbaji wadogo kuondokana na umasikini na alieleza kuwa wachimbaji hao wakiwezeshwa itachangia ongezeko la ajira.
Pia Profesa Muhongo alimuomba Balozi huyo wa Canada kufuatilia suala la kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake ili kuleta ufanisi wenye tija katika sekta za Nishati na Madini.
Kwa upande wake Balozi Leveque, alisema Canada inavutiwa kuwekeza hasa katika nishati jadidifu ikiwemo umeme wa jua na kwamba atayakaribisha makampuni ya nchini Canada kuwekeza katika uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia.
Balozi Leveque pia aliishauri Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi na kutoa wito wa usimamizi madhubuti wa Sekta ya Madini ili kuepusha muingiliano wa maeneo ya wachimbaji madini wakubwa wa nje na ndani ya nchi.
Aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo mbili na kuahidi kuwa Serikali ya Canada itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa masuala mbalimbali yakiwemo kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara na Taasisi zake.
No comments:
Post a Comment