ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 30, 2016

Rorya wapewa siku saba kuhakiki silaha

Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Felix Lyniva ametoa siku 14 kwa wamiliki wa silaha kuzihakiki na kuonya kuwa watakaokiuka watasakwa na kuchukuliwa hatua.
Amri hiyo inakuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutoa agizo kama hilo, huku Rais John Magufuli akiwa wa kwanza kuhakiki silaha anazozimiliki.
Lyniva amesema silaha zinazomilikiwa bila kibali zimekuwa zikitumika katika matukio ya uhalifu, kuibuka kwa wimbi la ujambazi nchini hususan unyang’anyi.
“Hakikisha unachukua silaha yako unaipeleka kwa OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) husika ili iweze kuhakikiwa, kuanzia Aprili 7 hadi 13 tutaanza usajili wa silaha hizo upya na Aprili 14 tunaanza msako mkali,” amesema Lyaniva.
Katika hatua nyingine, Lyniva amepiga marufuku kilimo cha bangi na kuwataka wananchi wanaojisughulisha nacho kuacha mara moja na kuanza kulima mazao halali ya biashara na chakula.
“Tunaanza msako mkali dhidi ya wakulima wa bangi kata za Ikoma na Goribe, ambazo zinaongoza kwa kilimo hicho, hatuwezi kuvumilia kuona vijana wetu wanaharibikiwa maisha kwa watu wachache wanaolima dawa za kulevya,” amesema.
Katika kuunga juhudi za mkuu wa wilaya huyo kuhamasisha shughuli za kilimo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Rorya, Samwel Keboye amewataka wanaCCM wanaomiliki silaha kihalali kuwa mstari wa mbele kuzipeleka kuhakikiwa kwa muda uliopangwa.
“Chama tawala tunapaswa kuonyesha mfano wa kuigwa ili na wenzetu waige kutii agizo hili unaona Rais katika eneo lake yeye alikuwa wa kwanza kutii agizo la mkuu wake wa mkoa, nasi tufanye hivyohivyo kwa kufuata nyayo zake,” amesema Keboye.
Amesema iwapo wananchi watafuata utaratibu kwa kile wanachotakiwa kufanya kwa muda uliopangwa, nchi itapata maendeleo haraka na nidhamu ya utendaji kuzidi kurejea.
Keboye amesema suala la amani halina mjadala kwa sababu maendeleo hayawezi kupatikana bila usalama.

No comments: