Mwendesha bodaboda Ramadhan Rajab akijaribu kupita katika barabara mbovu inayotokea Kimanzichana kuelekea vijiji vya Mnyonzole na Kibesa, Kata ya Panzuo, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.
Na Mwandishi Wetu, Mkuranga
JUMLA ya Sh Milioni 37 zimetangwa kwa ajili ya kukarabati barabara ya Mbogo na Mbezi Muungwana, inayopita katika vijiji kadhaa vya Kata ya Panzuo, wilaya Mkuranga, mkoani Pwani kwa ajili ya kupunguza adha za ubovu wa barabara wanazokutana nazo wananchi wa maeneo hayo hali inayopelekea wakati mwingine akina mama kujifungulia njiani.
Mapema mwezi uliopita baadhi ya wananchi wakiwamo akina mama
walizungumza kwa uchungu juu ya ukosefu wa barabara katika maeneo hayo, jambo
linalowanyima raha na ukosefu wa mbinu za kujikwamua kiuchumi kwa kukosekana
barabara inayopitika kwa wakati.
Akizungumza juu ya ukosefu wa barabara na mipango yao,
diwani wa Kata ya Panzuo, wilaya Mkuranga, mkoani Pwani, Juma Magaila, alisema
kwamba kiasi hicho cha pesa kitaanzia kwanza kuweka kifusi katika maeneo
mbalimbali ili wananchi wae ndelee na majukumu yao kwa kuhakikisha kwamba suala
hilo la barabara mbovu linashughulikiwa.
Alisema ni kweli wananchi katika maeneo hayo wamekuwa
wakiishi kwa mashaka hususan mvua zinapoanza kunyesha, ila tayari fedha
zimetangwa kwa ajili ya kuanza ukarabati wa barabara hiyo inayotumiwa na
wananchi wengi wilayani Mkuranga.
“Tunaendeelea na mikakati ya kuikwamua Kata yetu hususan
katika changamoto kubwa za ubovu wa barabara wanazokutana nazo wananchi wangu
wa Panzuo ambao wanashindwa kukuza uchumi wao kwasababu barabara haipitiki
kirahisi wakati wote.
“Naamini kwa kutengwa kiasi cha Sh Milioni 37 kutachangia
kwa kiasi kikubwa kuiweka barabara yetu katika kiwango cha kupitika huku
tukielekea katika safari ya kuona tunafikia hatua ya kuiwekea changarawe na
mengineyo,” Alisema.
Awali wananchi wa vijiji vya Kibesa wakiongozwa na
mwenyekiti wao Khamis Ningwe walitumia muda mwingi kuilalamikia barabara hiyo
sanjari na kuiomba serikali ya Halmashauri ya wilaya Mkuranga iliangalie suala
hilo kwa jicho pevu.
Endapo barabara hiyo itakarabatiwa japo kwa kiwango cha
kifusi, si tu akina mama wajawazito hawatajifungulia njiani kunaponyesha mvua,
bali wananchi wanaweza kuingiza kipato kwa kuuza bidhaa zao mbalimbali kama
vile nanasi na nyinginezo zinazopatikana katika maeneo hayo sanjari na kuleta
urahisi watu kuingia na kutoka kwenye maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment