Sefue ambaye alitumikia nafasi ya ukatibu mkuu kiongozi kwa miezi miwili katika utawala wa sasa wa Rais John Magufuli, alizoeleka kwa ukarimu wake na pia namna alivyokuwa mwepesi kupokea simu na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kikazi pindi alipoombwa na waaandishi wa habari kufanya hivyo.
Balozi Sefue (62), akiwa kwenye nafasi hiyo, aliwavutia waandishi wa habari wengi kutokana na hulka yake ya kutoa ushirikiano kwa kila mmoja, pasi na kukacha jukumu lake la kuhabarisha umma kwa kisingizio chochote kile.
Hata hivyo, uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa hivi sasa, Sefue yule aliyekuwa pia akipokea simu bila kujali kama anamjua anayepiga au hamjui, ameamua kubadilisha kabisa aina hiyo ya ‘ukarimu’ baada ya kuondolewa kwenye nafasi yake.
Licha ya Nipashe kutafutwa mfululizo na Nipashe kwa wiki mbili zilizopita, simu iliyokuwa ikitumiwa na Balozi Sefue imekuwa haipokewi tena na kwa namna iliyozoeleka na hata alipopotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu hiyo hakujibu.
Nipashe ilizungumza na Sefue mara ya mwisho Machi 6, ikiwa ni siku moja tu kabla ya kuondolewa Ikulu. Alizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu uchaguzi wa Meya wa Dar es Salaam, ambapo kwa uwazi alisema Ikulu haitapoteza chochote iwapo uchaguzi utafanyika na Ukawa wakachukua uongozi wa Jiji.
Akizungumza kwa kujiamini, Balozi Sefue alisema hakutakuwa na jambo la ajabu kwa Ikulu kuwa eneo linaloongozwa na Ukawa kwa sababu kuna mataifa mbalimbali duniani ambayo Ikulu ziko maeneo yanayoongozwa na wapinzani.
Lakini kwa wiki ya pili sasa, Nipashe ilijaribu mara kadhaa kumtafuta Balozi Sefue kwa kutumia simu yake ambayo ilikuwa ikitumiwa kuwasiliana naye mara kwa mara alipokuwa Ikulu, lakini iliita muda mrefu bila kupokewa.
Hata alipotumiwa ujumbe mfupi mara kadhaa kwenye simu yake hakujibu.
Sefue aliondolewa Ikulu Machi 7 baada ya kuitumikia serikali ya Rais Magufuli kwa siku 67 na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini India, Balozi John Kijazi.
Balozi Sefue alijizolea umaarufu mkubwa katika siku zote alizotumikia nafasi yake chini ya utawala wa Rais Magufuli. Kila alipoonekana kwenye luninga alivuta hisia za watu wengi waliokuwa wakitaka kumsikiliza, hasa wakitarajia kusikia kigogo gani ‘ametumbuliwa jipu’.
Umaarufu wake ulitokana na ukweli kwamba ni yeye ndiye aliyekuwa akitangaza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Rais Magufuli katika kuunda safu ya serikali yake, ikiwa ni pamoja na kutangaza mabadiliko mbalimbali aliyokuwa akiyafanya tangu aingie Ikulu Novemba 5, mwaka jana.
Hatua ya kutangaza mabadiliko yanayofanywa na Rais Magufuli yaliyopewa jina la ‘kutumbua majipu’ ilimfanya Sefue kuwa maarufu zaidi nchini tofauti na alivyokuwa kwenye serikali ya Kikwete.
Balozi Sefue alizaliwa Agosti 26, 1954 katika Wilaya ya Same, mkoa wa Kilimanjaro na baadaye alisomea Sera za Umma na Utawala katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Ana Shahada ya Uzamili kwenye fani hiyo aliyoipata kwenye Chuo Kikuu cha The Hague, Uholanzi mwaka 1981 na Astashahada ya Uzamili ya Uhusiano wa Kimataifa, ya Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam.
Alikuwa Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2007 na kabla ya hapo aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada kati ya mwaka 2006 hadi 2007 .
Balozi Sefue amewahi kufanya kazi kama msaidizi binafsi wa aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassani Mwinyi na mwaka 1995, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alipoingia madarakani aliendelea kuwa na Sefue hadi mwaka 2005.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment