ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 27, 2016

SHEIN TUMBUA MAJIPU KAMA MAGUFULI - ASKOFU

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein akimwapisha Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Said Hassan Said katika hafla iliyofanyika jana Ikulu Zanzibar. Picha na Ikulu. 

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ametakiwa afuate nyayo na dhana ya utumbuaji majipu ya Rais John Magufuli kwa kuwa imegusa maisha ya wananchi wanyonge.
Wito huo ulitolewa juzi na Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Jimbo la Tabora Francis Ntiruka katika mahubiri ya Ijumaa Kuu katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu mjini Dodoma.
Askofu huyo alisema Yesu Kikristo aliteseka hadi kuuawa kwa ajili ya kutetea haki za wanyonge na vivyo hivyo lazima viongozi wawatetee wanyonge.
Alisema kifo chake kiliambatana na vipigo vya mateso ya dhihaka nyingi kutoka kwa watawala waliotaka kujinufaisha wao binafsi pasipo kujali wengine.
“Ni bora ufe kwa ujali wengine kuliko kujinufaisha, alisema askofu huyo ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John.
Alimtaka Dk Shein aliyeapishwa juzi kuwa Rais wa Zanzibar ajipange kuhakikisha analeta umoja na amani ya Wazanzibari na kutumbua majipu kama anavyofanya Rais Magufuli.
Alisema Watanzania wana mateso mengi kama ya umaskini, magonjwa, kuporwa haki na rasilimali zao jambo alilosema bila kutafutiwa ufumbuzi, malalamiko yao hayataisha.
Akizungumzia uchaguzi wa marudio ya Zanzibar, Askofu huyo alisema uligubikwa na malalamiko yenye giza la sintofahamu na kunyima demokrasia hadi wengine kukataa kupiga kura, jambo ambalo alisema lilihitaji mazungumzo ili kila mtu aridhike.
“Shein kashinda, nampongeza na maandiko yananitaka niitii hivyo, lakini waliompigia kura ni chama chake pekee,” alisema huku akihoji; “kulikuwa na nini hadi marudio ya uchaguzi yafanyike?”
Shein amwapisha mwanasheria mkuu
Katika hatua nyingine, Rais Shein jana alimwapisha Said Hassan Said kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar baada ya kumteua juzi.
Mteule huyo wa kwanza wa Dk Shein awamu hii, ndiye anayetarajiwa kumsaidia kiongozi huyo kubeba mzigo mzito kuteua makamu wa kwanza na makamu wa pili wa Rais na Baraza la Mawaziri kukidhi matakwa ya Katiba ya kuwapo Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), bila kuwapo chama cha upinzani kilichokidhi vigezo vya kushirikishwa katika kuunda Serikali.
Aliapishwa saa 4.30 asubuhi katika Ikulu ya Zanzibar kwa mujibu wa Ibara cha 55 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Said alikuwa akishikilia nafasi hiyo tangu Rais Shein alipotengua uteuzi wa aliyemtangulia, Othman Masoud mwaka juzi.
Said aliyewahi kufanya kazi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar miaka ya 2000, anatokea katika familia ya wanasheria akiwamo baba yake, Hassan Said Mzee.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu.

No comments: