
Panga linalonolewa na Rais John Magufuli kwa ajili ya kufyeka mishahara minono, litatikisa vigogo wa taasisi za umma zinazomiliki mali zenye thamani ya Sh22 trilioni, Mwananchi limebaini.
Thamani ya mali za taasisi hizo ni pungufu ya Sh900 bilioni ya Pato la Taifa, kwa mujibu wa taarifa ya matokeo ya awali ya Pato la Taifa la Oktoba-Desemba 2015 iliyotolewa na Shirika la Taifa la Takwimu (NBS).
Kwa maana hiyo, taasisi hizo ambazo ni pamoja na mashirika makubwa ya umma, zinashikilia takriban robo ya uchunmi wa Taifa.
Rais Magufuli akiwa nyumbani kwake Chato juzi, alisema atapunguza mishahara ya wakurugenzi na watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma wanaolipwa takriban Sh40 milioni hadi kufikia kiwango kisichozidi Sh15 milioni.
“Katika Serikali ninayoongoza, sitegemei kumlipa mtumishi zaidi ya Sh15 milioni. Tayari nimeunda tume kushughulikia hilo,” alisema Rais Magufuli, ambaye tangu aingie madarakani amejikita katika kukusanya mapato ya Serikali, kupunguza matumizi na kupambana na wizi wa mali za umma.
Ingawa si mashirika yote ya umma yenye wakurugenzi wanaolipwa kiwango hicho, uamuzi huo unaweza kuyaathiri mashirika karibu yote 216 ya umma kwa kuwa upo uwezekano wa wakurugenzi na maofisa wengine wa chini ambao pia wataingia katika mkumbo huo ili wasiwazidi mabosi wao.
Akizungumzia suala hilo, Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru alisema kutokana na hesabu za ukaguzi uliofanyika hadi Juni 2015, jumla ya mali za mashirika 216 ya umma na taasisi za Serikali zilizofanyiwa ukaguzi ni Sh22 trilioni kutokana na taarifa ya ukaguzi wa kipindi cha kuishia Juni 2015.
Kwa mujibu wa Mafuru, idadi hiyo ya mashirika na taasisi za umma inajumuisha mashirika ya habari, vyuo vikuu, taasisi, mamlaka mbalimbali na wakala.
Lakini Mafuru hakuwa tayari kujadili tamko hilo la Rais akisema ni mapema kwa kuwa ni vizuri kuangalia madhara na faida za hatua hiyo kwa pande zote mbili.
Alisema Rais Magufuli ana nia nzuri ya kuweka usawa na kuwasaidia wananchi walio katika lindi la umaskini kama kauli yake ilivyojieleza juzi akiwa Chato.
“Rais amesema jana (juzi), hivyo ni mapema mno kujua madhara na faida. Baada ya muda tutajua Serikali imeokoa kiasi gani na huenda hata tukajua wakurugenzi hao wataathirika vipi,” alisema.
Alisema suala hilo ni pana kwani pamoja na Rais kutaka kuweka usawa, kuna wakurugenzi ambao wana thamani na wanategemewa katika taasisi na mashirika yao, hivyo iwapo wataondoka au watahama ni vyema tukaangalia athari zake.
Alisema wakati muafaka ukifika itajulikana fedha zitakazookolewa kwa kupunguzwa mishahara hiyo na matumizi yake. Hata hivyo, Rais Magufuli alisema fedha zitakazopunguzwa zitaongezewa kwenye mishahara ya watu wa chini.
Wakati tamko la Rais likiwa limeibua mjadala mzito, hasa kuhusu athari za kupunguza mishahara na uwezekano wa jambo hilo kufanyika, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura amesema mwajiri ndiye mwenye uamuzi wa mwisho wa mshahara wa muajiriwa.
Alisema anaamini uamuzi huo hautavunja sheria na taratibu za utumishi wa umma, ndiyo maana umepangwa katika bajeti ijayo ambayo hujadiliwa na kupitishwa kisheria.
Alipoulizwa kama kuna tatizo lolote la kisheria iwapo mishahara itashushwa kwa vigogo hao, Rwechungura alisema hiyo hupangwa na mwajiri ambaye kwa mashirika ya umma ni Serikali kupitia kwa bodi za wakurugenzi.
“Sheria zinazoanzisha mashirika hayo zinaeleza kuwa kuna wakati Bodi itapokea maelekezo na ushauri kutoka kwa waziri mwenye dhamana, hivyo bodi zinaweza kupokea maagizo hayo ya kupunguza mishahara ya wakurugenzi wakuu,” alisema Rwechungura.
Wakurugenzi wafunguka
Mwenyekiti wa Jukwaa la Maofisa Watendaji Wakuu (CEORoundtable), Ali Mufuruki alisema pendekezo la kupunguza mishahara kwa mabosi hao linatakiwa lichambuliwe kwa kina kwa sababu linaweza kupunguza ufanisi katika mashirika ya umma na kusababisha baadhi ya wafanyakazi wazuri kukimbilia sekta binafsi.
Alisema mishahara ya wakurugenzi hao inatakiwa kutolewa kwa mujibu wa ukubwa, uzalishaji na umuhimu wake katika ukuzaji wa uchumi na si mienendo ya kisiasa kwa sababu hata kipindi cha ujamaa watu walilipwa kutokana na wanachozalisha.
“Rais anaweza kuwa na nia nzuri ya kubana matumizi, lakini asisahau kuna mashirika 10 yanayoshikilia asilimia 40 ya Pato la Taifa. Tusipoangalia, yanaweza kuendeshwa na watu duni, ikitokea hivyo hayatafanya vizuri na tutakula hasara,” alisema.
Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, watumishi wengi wa Serikali na taasisi za umma, hasa madaktari na wahandisi waliamua kwenda nje ya nchi kutafuta ajira bora, wengi wakienda nchi za kusini mwa Afrika ambazo zilikuwa zinaondokana na utawala wa kikoloni.
Hata hivyo, katika Serikali ya Awamu ya Nne, Rais Jakaya Kikwete alishawishi kurejea nchini kuungana na wenzao kujenga Taifa, baadhi akiwapa nafasi nyeti za kisiasa.
Pamoja na tamko hilo la Rais kufyeka mishahara, Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu alisema anaamini mkuu wa nchi ana nia nzuri.
“Mimi naona si jambo baya, isitoshe sipo huko kwenye hiyo mishahara inayotajwa na nitafurahi ikipunguzwa ili kuwe na usawa,” alisema.
Alisema hatua ya Rais Magufuli ina nia ya kuwaondoa watu kutoka katika lindi la umaskini.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale hakutaka kujadili tamko hilo.
“Mimi ni nani hata nijadili maamuzi ya Rais? Rais akishasema mimi sina la kusema. Mnataka kutuchonganisha?” alihoji.
Alisema kiongozi wa nchi ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kwa hiyo hakuna wa kumpinga.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema uamuzi wa Rais Magufuli unafanywa kila nchi na nia yake ni kupunguza tofauti katika mishahara.
“Ni hatua nzuri na sina matatizo nayo. Kila nchi inajaribu kuondoa tofauti. Hata wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere alifanya hivyo. Haiwezekani mtu akapata mshahara mkubwa kwa mwezi wakati mwingine atatumia miaka sita kupata mshahara kama huo,” alisema.
Hata hivyo, alisema yeye si miongoni mwa wakurugenzi wanaolipwa mishahara mikubwa na hivyo hatua ya Rais hana matatizo nayo.
Wakati Profesa Museru akisema hayo, Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake (BW), Margareth Chacha alisema anaisubiri hatua ya Rais kwa kuwa bado haijachanganuliwa na kujulikana itawagusa wakurugenzi wa aina gani.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdulkarim Mruma aliunga mkono uamuzi huo akisema hali ya nchi ilifikia pabaya kwa wakurugenzi watendaji kujipangia mishahara mikubwa kwa kuzishawishi bodi zao za wakurugenzi.
“Sisi Watendaji wakuu wa Serikali ndiyo wenye marupurupu ya vikao na burudani huku watendaji wa chini wakiwa hawana kitu,” alisema.
Hata hivyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Usimamizi wa Biashara wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Tumsifu Elly alisema uamuzi huo wa Rais utasaidia kuongeza morali kwa wafanyakazi wa chini ambao mishahara yao ilikuwa midogo.
Dk Elly alisema hoja kuwa watumishi hao watakimbilia sekta binafsi na kuathiri utendaji wa mashirika ya umma haina mashiko kwa kuwa sekta binafsi haina uwezo wa kubeba vigogo wote kutoka serikalini.
“Kama watakuwa wakipunguza mshahara kwa shirika moja moja, italeta shida lakini kama itashushwa kwa pamoja italeta mshtuko mdogo na baada ya hapo hali itarudi kama kawaida kwa sababu soko la ajira la sekta binafsi haliwezi kuwamudu,” alisema.
Mfanyabiashara wa matunda, Moses Andrew alisema Rais amefanya jambo zuri litakalopunguza mwanya wa kimapato kati ya maskini na tajiri kwani sasa kuna tofauti kubwa kimapato ukilinganisha na ukuaji wa uchumi wetu.
No comments:
Post a Comment