Uamuzi wa Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) kuinyima Tanzania msaada wa Sh1 trilioni kwa ajili ya kufadhili miradi ya umeme, umewagawa wananchi kutokana na baadhi kuilaumu Serikali na wengine kuunga mkono msimamo wa kujenga uchumi bila ya kutegemea misaada.
Katika kikao chake kilichofanyika Machi 28, Bodi ya Wakurugenzi wa MCC, shirika lililoundwa na Bunge la Marekani kusaidia nchi zinazoendelea, iliamriwa kuwa Tanzania iondolewe miongoni mwa nchi washirika watakaonufaika na misaada ya mfuko huo kutokana na kupoteza sifa.
Bodi hiyo ilisema kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, na kuendesha uchaguzi wa marudio Machi 20 bila ushirikishwaji wa wadau na utekelezaji wa Sheria ya Mtandao ni sababu zilizofanya Tanzania ipoteze sifa za kuwa mnufaika wa miradi hiyo.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani Oktoba 28, 2015 siku ambayo alitakiwa amtangaze mshindi wa kiti cha rais. Uamuzi huo ulipingwa na chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar, CUF lakini Jecha akatangaza tarehe mpya ya uchaguzi ambao ulirudiwa Machi 20.
Pia, kwa kutumia Sheria ya Mtandao, watu kadhaa walikamatwa kwa tuhuma za kusambaza habari za upotoshaji, huku Chadema ikilalamika kuwa vijana wake waliokuwa wakijumlisha matokeo ya uchaguzi walikamatwa na kunyang’anywa kompyuta zao.
Akizungumzia hatua hiyo, Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, Peter Msigwa alisema wakati tukijenga uwezo wa kujitegemea, bado tunahitaji kuutumia ushirikiano uliopo na nchi marafiki ya mashirika ya kimataifa ili Tanzania isiishi kama kisiwa.
“Nimesikitishwa na Tanzania kukosa fedha za MCC ambazo zilikuwa ni muhimu sana katika kuharakisha upatikanaji wa umeme kwa Watanzania wa vijijini. Hata hivyo, ningependa kuweka wazi kuwa Tanzania haijaonewa hata kidogo kunyimwa msaada wa Sh1 trilioni na Shirika la Misaada la Marekani la MCC kama ilivyopotoshwa na Serikali,” alisema Msigwa katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
“Ni vema ikazingatiwa kuwa MCC inazingatia vigezo 17 katika kuchagua nchi inayostahili kupata msaada na miongoni mwa vigezo vya msingi kabisa ni nchi husika kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha demokrasia na kuendesha chaguzi zilizo huru na haki.
“Na katika taarifa yake MCC ilieleza maeneo ambayo Tanzania imekiuka vigezo kuwa ni marudio ya uchaguzi wa urais Zanzibar na kupitisha Sheria ya Makosa ya Mawasiliano ya Mitandaoni –“Cyber Crime.”
Mchungaji Msigwa ameelezwa kushangazwa na kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga kuwa amestushwa na uamuzi wa MCC, badala ya kukiri makosa yaliyofanywa na Serikali na chama tawala katika suala la Zanzibar na mtumizi ya Sheria ya Mtandao, ambayo amesema yananyima uhuru wa habari na kujumuika.
Makamu Mkuu wa Chuo Kiku Kishiriki cha Ruaha (Ruco), Profesa Gaudence Mpangala aliungana na Mchungaji Msigwa kuhusu uamuzi wa MCC.
“Uroho wa madaraka wa kundi dogo la Watanzania umesababisha dhahama hiyo itakayoligharimu Taifa kwa muda mrefu wakati mikakati ya kusaka mbadala ikiandaliwa,” alisema.
“Pamoja na jitihada za serikali kubana matumizi na kuongeza ukusanyaji wa mapato hatuwezi kuziba pengo lililopo. Itachukua muda.”
Naye mkurugenzi mtendaji wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali inalojihusisha na Masuala ya Kijamii (Fordia), Buberwa Kaiza ameandika katika ukurasa wake wa facebook kuwa Tanzania inapaswa kuwa makini zaidi.
“Tunachotakiwa kufahamu ni kuwa Tanzania isipokuwa makini itaelekea njia ile ile na kuishia iliko Zimbabwe ya sasa. Si muda mrefu tutasikia Eurozone (nchi za barani Ulaya) nao wameamua hivi au vile dhidi ya Tanzania. Haitachukua muda tutasikia G7 wameamua kuunga mkono Serikali ya Marekani dhidi ya Tanzania. Baadaye watafuata Paris Club, WTO na kadhalika,” ameandika mwanaharakati huyo.
Lakini wachambuzi wengine waliilaumu Marekani kwa kutaka kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.
Mhadhiri mwanadamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Francis Michael alisema MCC wana haki ya kufanya kile walichoamua, lakini wanapaswa kutambua kuwa Tanzania pia ina haki kama hiyo katika kuendesha mambo yake.
“Hatuwezi kuamuliwa au kupangiwa masuala yetu ya ndani kwa mgongo wa misaada. Huu ni ukoloni mamboleo. Wakae na misaada yao. Jambo muhimu ni kwa Rais (John) Magufuli kusimamia uzalishaji nchini,” alisema Dk Michael.
“Viwanda vilivyokufa vifufuliwe na kilimo kipewe mkazo unaohitajika ili kutosheleza mahitaji ya ndani na ziada isafirishwe nje. Marekani ni wazuri kwenye kuhubiri demokrasia. Ni wao ndio wanaoifadhili Israel wakati wanafahamu kuwa inaikalia Palestina kwa mabavu. Demokrasia hainunulwi.”
Mtaalamu wa masuala ya fedha na utawala jijini hapa, Asanterabi Barakaeli alisema: “Kwa kipindi kirefu tumekuwa tukitegemea misaada hiyo, lakini haijatufikisha popote. Tuanze kufikiri uchumi bila misaada.”
No comments:
Post a Comment