ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 23, 2016

UKAWA WATWAA DAR ES SALAAM

Hatimaye, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umeshika hatamu za uongozi wa Jiji la Dar es Salaam baada ya Isaya Mwita kuchaguliwa kuwa meya wake.
Diwani huyo wa Vijibweni kwa tiketi ya Chadema aliibuka mshindi katika uchaguzi huo ulioahirishwa mara tatu kabla ya jana kushinda kwa kura 84 dhidi ya 67 za Diwani wa Mburahati (CCM) Yusuph Yenga, kati ya kura 151 zilizopigwa.
Mara ya kwanza uchaguzi huo, ulipangwa kufanyika Januari 23, lakini uliahirishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene ili kutoa nafasi mameya wa Manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni kuteua wajumbe.

Uchaguzi huo ulipangwa tena Februari 8, lakini uliahirishwa baada ya kubainika nyongeza ya wajumbe 14, katika orodha iliyowasilishwa na wakurugenzi wa manispaa za Kinondoni na Ilala.
Simbachawene aliagiza tena uchaguzi huo ufanyike Februari 29 lakini uliahirishwa baada ya makada wawili wa CCM, kuweka zuio katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali zuio hilo na Simbachawene kuagiza ufanyike kabla Machi 25. Pamoja na agizo hilo, CCM, walikwenda tena mahakamani kuomba wajumbe wake walioondolewa warudishwe kwa madai kuwa ni wapigakura halali.


Juzi, mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi hilo ikisema haikuona sababu za msingi zilizowasilishwa na walalamikaji kuzuia kufanyika kwa uchaguzi huo.
Mbali na mahakama kusema hayo, juzi, Rais John Magufuli alizitaka pande zote zinazogombea kiti cha umeya, kukamilisha mchakato huo badala ya kuendeleza malumbano na kuacha demokrasia ichukue mkondo wake.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa chama cha upinzani kushinda kiti hicho tangu uchaguzi wa vyama vingi uliporejea nchini mwaka 1995. Upinzani pia kwa mara ya kwanza umeshinda umeya katika manispaa mbili za Mkoa wa Dar es Salaam za Ilala na Kinondoni.

Ilivyokuwa jana
Jana, kikao cha Baraza la Madiwani la Jiji la Dar es Salaam kilifunguliwa saa 4.50 asubuhi baada ya wajumbe wote kukamilisha taratibu za kujisajili na kuhakikiwa majina yao. Lakini safari hii hali ilikuwa tofauti kwani wajumbe hao walihakikiwa majina yao nje ya geti kuu la Karimjee.

Baadaye wakiwa ukumbini, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sarah Yohana alifungua kikao hicho na kutaja idadi ya wajumbe watakaostahili kupiga kura kuwa ni 163 endapo watafika wote katika ukumbi huo.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando huku akiwa amezungukwa na askari wanne wenye sare, aliwataka wajumbe hao kufanya uchaguzi wa haki na amani huku akieleza utaratibu utakaotumika kumpata meya ukiwamo wa kura kupigwa kwa siri na wagombea kupewa dakika tano kujieleza.

Ulinzi huo uliimarishwa kwa Mmbando kutokana na vurugu zilizotokea uchaguzi huo ulipoahirishwa kwa mara ya mwisho ambao alitiwa msukosuko na wajumbe wa Ukawa.
Upigaji kura ulianza saa 5.20 asubuhi na kuhitimishwa saa 12.23 mchana. Mchakato huo ulichukua muda mrefu kwani licha ya wajumbe kupewa namba wakati wa kuandikishwa, walikataa kuzitumia na kuamua waitwe jina mmojammoja, apige kura hadi kumaliza ndipo mwingine afuate.
Baada ya upigaji kura kumalizika, Yohana aliyekuwa msimamizi alitangaza kwamba kura hizo zitahesabiwa kwa uwazi hatua ambayo ilishangaliwa na wajumbe wa Ukawa kwa kupiga makofi.

Wakati wa kuhesabu kura hizo, Mwita alimchagua Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob kumsimamia wakati Yenga aliamua kusimama mwenyewe.
Kura hizo zilimwagwa katika meza na kuanza kuhesabiwa na ofisa wa Jiji ambaye alikuwa akikabidhi kura za Ukawa kwa Jacob na CCM kwa Yenga.
Wakati kazi hiyo ikiendelea, baadhi ya wajumbe wa CCM, akiwamo mfanyabiashara Yusuph Manji waliondoka.
Hata kabla ya kutangazwa rasmi wajumbe wa Ukawa walianza kulipuka kwa shangwe wakisema Peoplees… na wengine wakiitikia power…
“Jamani mnavunja sheria wenyewe, ninayestahili kutangaza matokeo ni mimi. Kwa hiyo kuweni wavumilivu hadi nitangaze,” alisema Yohana.

Akitangaza matokeo, Yohana alisema kura halali zilizopigwa ni 151 na zilizoharibika ni saba na wajumbe waliopiga kura ni 158 kati ya 163. Kisha alitangaza matokeo hayo na kufuatiwa na shangwe za wajumbe wa Ukawa ambao safari hii walikuwa wakiimba ‘Maalim Seif... Maalim Seif...’ wakimtaja Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar kabla ya chama hicho kujitoa kushiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumapili iliyopita baada ya ule wa Oktoba 25, mwaka jana kufutwa.

Ahadi za wagombea
Awali, akijinadi, Mwita aliahidi kufanya kazi na kila mtu akisema jiji hilo lina changamoto nyingi ikiwamo wanafunzi kukaa chini na foleni za magari.
“Nawaomba leo mfanye maamuzi ya dhati ya kunichagua. Nina uwezo na ninatosha, maendeleo hayana chama,” alisema Mwita.
Kwa upande wa Yenga, alisema endapo angepata nafasi hiyo, angemtumikia kila mtu bila kujali itikadi ya vyama huku akiwasihi wajumbe wasihofu kumchagua kwani ana uwezo.
“Nitatimiza malengo ya maendeleo na msiwe na wasiwasi. Hapa hatumchagui mtu, bali tunachagua kiongozi,” alisema Yenga.

Lowassa ukumbini
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alikuwa ni miongoni mwa wageni waliohudhuria uchaguzi huo. Alishangiliwa kwa nguvu na wafuasi wa Ukawa waliokuwa wamejazana nje ya lango la kuingilia Karimjee huku wakiimba rais… rais…
Hata alipoingia ndani ya ukumbi, wajumbe wa Ukawa walimshangilia huku wakiimba; “Mabadilikooo Lowassa... Lowassaaaa Mabadiliko,” walipokuwa wakisema maneno hayo, walikuwa wakizungusha mikono yao.
Viongozi wengine wa Ukawa walioshuhudia uchaguzi huo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wake, Dk Vincent Mashinji na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya, wabunge, Ester Bulaya, Ester Matiko, Gobless Lema na Joseph Haule, wote wa Chadema.

MWANANCHI

3 comments:

Anonymous said...

Ndio maana wana kosa Kura Vijijini wanafikiri watanzania wako Dar tu mi kijijini kwetu hawajui ukawa wana jua ccm wanganie Dat maana ndio kuna watanzania wengi uchaguzi ukija wameibiwa kura

Anonymous said...

fanyeni kazi sasa acheni vurugu na domo

Unknown said...

Hawa UKAWA wakiwa Dodoma wanalilia eti mambo ya maslahi yanayovuka kuta za kivyama. Wakishinda tu (hata ushindi wa udiwani, wanarudia hayo hayo ya kivyama. Ndio, Dar ni ya UKAWA lakini, kama alivyoandika huyo anon wa hapo juu, Dar is never a starter...yaaani ni non-starter of political voting deciocions in Tanzania. Kimantiki,Dar ni ya UKAWA; Tanzania ni ya CCM, ama sivyo?