ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 14, 2016

Watatu wahofiwa kufa mgodini Mirerani

By Joseph Lyimo, Mwananchi -- jlyimo@mwananchi.co.tz

Mirerani. Watu watatu wanahofiwa kufariki dunia, baada ya kufukiwa na kifusi kwenye mgodi wa JW unaomilikiwa na Kampuni ya TanzaniteOne, iliyopo Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Inadaiwa kuwa, watu hao ambao ni wachimbaji haramu waliingia kwenye mgodi huo tangu Marchi 7 wakiwa wanne huku wakifanya kazi kwenye mgodi huo bila ruhusa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Francis Masawe alisema ajali hiyo lilitokea Machi 12 saa 8.30 mchana na kwamba siku hiyo mmoja kati ya wachimbaji, Kidishi Benedict (32) mkazi wa kitongoji cha Songambele alifika Kituo cha Polisi Mirerani na kutoa taarifa kuwa wenzake, Saidi Mgosi na Khalidi wakazi wa mji mdogo wa Bomang’ombe, Hai na mwingine alijulikana kwa jina moja la Dominick mkazi wa Zaire, Mirerani wameangukiwa na udongo.

Alisema polisi na uongozi wa TanzaniteOne wanaendelea kuwatafuta watu hao ili kubaini kama ni wazima au la.

Kaimu Mkurugenzi wa TanzaniteOne, Modest Apolinary alisema watu hao siyo wafanyakazi wake na kwamba mgodi wa JW haufanyi kazi tangu Agosti mwaka jana.

Alisema wanaendelea na kazi ya kufukua mgodi huo ili kubaini kama watu hao wapo hai au wamefariki dunia.

No comments: