Pichani Dr. Albina Chuwa , Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (mstari wa mwisho) katika siku ya mwisho ya Mkutano wa 47 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa, mkutano uliopitisha mfumo wa viashiria vya kupitia utekelezaji wa Malengo ya Endelevu ya Maendeleo ( agenda 2030) aliyeketi nyuma na Mkurugenzi Mkuu, ni Afisa Mwandamizi wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Bw. Songelael Shilla.
Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano wa 47 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa wakifuatilia majumuisho ya mkutano wao wa wiki mmoja uliomalizika mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi Maalum, New York
Wajumbe wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa, ( UNSC) wamekubaliana juu ya mfumo ambao utatumika kupima utekelezaji wa Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030)
Makubaliano hayo yamefikiwa mwishoni mwa wiki wakati wajumbe 24 wanaounda Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa, pamoja na wadau wengine walipokutana kwa mkutano wao wa 47 uliodumu kwa wiki moja.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dr. Albina Chuwa aliongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano huu, ambapo Tanzania ilishiriki kama Mjumbe wa Kundi la Waatalamu kuhusu Viashiria vya Mendeleo Endelevu (Inter-Agency Expert on Indicators of Sustainable Development Goals).
Pamoja na kujadiliana kuhusu viashiria na umuhimu wake katika kupima utekelezaji wa Agenda-2030, washiriki wa mkutano huu pia walijadili ajenda nyingine zilizohusu takwimu za wakimbizi,, program ya ulinganifu wa kimataifa wa data, na misaada ya kitakwimu katika utekelezaji wa Agenda 2030.
Agenda 2030 ina malengo malengo 17 yakiwa pia na viambatisho 169 na ilipitishwa rasmi na Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali mwezi Septemba mwaka jana na utekelezaji wake umeanza mwezi Januari mwaka huu.
Ajenda imebeba maudhui ya “kubadili dunia yetu: ajenda ya mwaka 2030 kwa maendeleo endelevu”. Ni ya kihistoria ikijumuisha masuala yote muhimu yanayowahusu na kugusa maisha ya kila mtu na ikiwakilisha matarajio makubwa ya maendeleo ya dunia nzima.
Inaelezwa pia kwamba ni ajenda ya watu, ambayo imesheheni mipango ya kutokomeza umaskini wa aina zote, bila kumwacha mtu yeyote nyuma. Ikilenga pia kuhakikisha Amani na usalama, kuongeza ufanisi katika shughuli za maendeleo na kubuni ubia unaojali binadamu na sayari Dunia.
No comments:
Post a Comment