
Katiba ya nchi yoyote ile ni kielelezo cha makubaliano( consensus) kati ya watawala na watawaliwa. Kwa lugha nyingine katiba ni mkataba wa kijamii( social contract) ambao umejegwa katiba msingi wa makubaliano kati ya watala na watawaliwa kuwa nyenzo ya kujiongoza kwa ustawi wa nchi husika. Hivyo kwa mkutadha huo, sio tu kwamba lazima katiba iwe ya maridhiano, bali lazima ijengwe katika msingi shirikishi. Wananchi lazima wasikilizwe na washiriki katika kuunda katiba hiyo kwa kutoa maoni pamoja na mapendekezo wanayoona ni sahihi kwa ustawi wa nchi yao. Hii ndiyo dhana kuu inayotofautisha tawala za kidemokrasia na zile ambazo sio za kidemokrasia.
Rais wa kwanza wa Tanzania Mwl Julius Kambarage Nyerere ananukuliwa kwenye kitabu kinachoitwa 'Uhuru na maendeleo' cha mwaka 1973 katika ukurasa wake wa 70 akisema ''Hakuna mtu mwenye haki ya kusema, ''mimi ni watu''. Hakuna Mtanzania mwenye haki ya kusema, '' najua kilicho bora kwa watanzania na wengine lazima wakifanye.'' Watanzania wanatakiwa kufanya maamuzi kwajili ya Tanzania.''
Historia inaonesha dhahiri kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi Duniani ambazo hazijawahi kuwa na katiba shirikishi licha ya kubadilisha katiba zake mara nne.
Itakumbukwa kwamba Tanzania kama nchi nyingine zilizotawaliwa na wakoloni, punde baada ya kujinasua katika minyororo ya ukoloni, ilipata katiba yake ya kwanza iliyoitwa katiba ya uhuru( Independence constitution) mwaka 1961. Katiba hii ya kwanza, ilikuja kama sehemu ya kufanya mabadiliko makubwa ya kisheria kwa kuondoa na kurekebisha sheria nyingi hasa zile kandamizi zilizotumiwa na wakoloni katika kuitawala Tanyanyika (Germany East Africa). Ukweli ni kwamba katiba hii kama tatu zilizofuatia haikuwa shirikishi!
Katiba ya pili ya Tanzania ni Katiba ya Jamuhuri( Republican Constitution) ya mwaka 1962. Hii ndiyo katiba ambayo sio tu ilibadilisha mfumo wa waziri mkuu kuwa kiongozi mkuu wa nchi na kuasisi cheo cha urais na rais kuwa kiongozi mkuu wa nchi, Katiba hii ndiyo ilijenga msingi wa marais wetu kuwa wafalme rejareja na wasio shikika( untouchable)!
Kama sehemu ya kulinda utawala wa rais mwenye nguvu ya ajabu dhidi ya wale wenye mawazo kinzani juu ya utawala uliokuwepo na mfumo wa kifalme rejareja, mwaka huo huo(1962) serikali iliamua kutunga sheria kali ya kuzuia uhaini( The preventive and detention Act, 1962) lengo kuu likiwa ni kudhibiti wote waliojaribu kukinzana na utawala uliokuwepo. Hii ndiyo sheria iliyolenga kuwafunga vinywa wale ambao sauti zao hazikupendwa na masikio ya serikali ya Mwalimu Nyerere.
Ni katiba hii ya Jamuhuri ambayo ilimpa nguvu kubwa rais wa nchi kwa kumlinda yeye, wateule wake na watumishi wote wa umma wanaopatikana kwa mamlaka yake iwe kwa yeye kuwateuwa au wao kuteuliwa kwa niaba yake hata pale wanapofanya madudu. Hakika rushwa, ufisadi, wizi wa rasirimali za nchi na uonevu pamoja na kupendeleana vitabaki kuwa kanuni( principle) pale nchi itakapokuwa inafanya makosa ya kuchagua wafalme rejareja( Marais) wasiokuwa waadilifu chini ya mfumo huu mbovu wa kisheria tulionao sasa.
Ni dhahiri kuwa haya ni matokeo ya watanzania kutopewa fursa ya kufanya maamuzi kwajili ya Tanzania!
Katiba ya Tatu ya Tanzania, ilikuja kama sehemu ya kutimiza matakwa ya makubaliano ya muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar yaliyotaka, pamoja na mambo mengine, kuundwa kwa katiba ndani ya mwaka mmoja. Ni wazi mwaka mmoja ni muda mfupi sana kwa nchi kupata katiba ambayo wananchi wataijadili kindaki ndaki na kutoa maoni yao. Kitendo cha kuweka sharti la kuundwa kwa katiba ndani ya mwaka mmoja ( muda mfupi) baada ya muungano wa mwaka 1964 ni wazi kuwa kiliakisi mwendelezo wa utamaduni wa watawala kuunda katiba bila kuwashirikisha wananchi.
Katiba hiyo ya tatu ya Tanzania iliyofahamika kama katiba ya mpito( interim constitution) iliuundwa mwaka 1965 punde tu baada ya mfumo wa siasa za vyama vingi kutupiliwa mbali na watawala kwa sababu mbalimbali ikiwemo ile ya kujenga umoja wa kitaifa.
Kimsingi katiba ya mwaka 1965 ambayo iliundwa kwa kukaranga( append) muundo wa katiba ya TANU, ilikuja na mabadiliko makubwa mawili. Mosi, iliondoa muswada wa haki za binadamu( bill of rights) kwenye utangulizi wake( preamble) na kuweka haki za msingi na uhuru( fundamental rights and freedom). Hili ni kosa ambalo pamoja na katiba ya mwaka 1977 kulirudia, hatimaye baada ya mjadala mpana wa kikatiba wa mwaka 1983 na mabadiliko ya siasa za dunia, watawala waliamua kutoa ulimbo masikioni mwao kwa kukubali marekebisho na hivyo kurejesha muswada wa haki za binadamu kwenye utangulizi wa katiba ya mwaka 1977.
Jambo la pili ambalo lilifanyiwa marekebisho na katiba hii ya mpito ni kuweka mazingira ya nguvu ya mfumo wa chama kimoja( TANU) baada ya kufuta mfumo wa vyama vingi. Hakika huu ulikuwa ni ubabe wa aina yake kati ya dereva( TANU) na abiria( ANC,UTP,PDP, AMNUT n.k). Kama ambavyo katiba ya Uhuru na ile ya Jamuhuri zilivyoshindwa kuona zababu ya kusikiliza maoni ya wananchi, katiba hii pia ilifanya makosa yaleyale!
Katiba ya nne ya Tanzania ni ile ya mwaka 1977 ambayo inatumika hivi sasa licha ya kuwepo kwa majaribio kadhaa ya kuiondolea uhai. Ni marehemu mzee Thabit Kombo na wenzake 19 ndio waliopewa jukumu nyeti la kuandaa mapendekezo ya katiba mpya mnamo tarehe 16 mwezi wa tatu mwaka 1977 na Mwalimu Nyerere.
Itakumbukwa kwamba, kamati hii iliyopewa jukumu hili zito la kuandaa mapendekezo ya katiba ya nchi ni ileile iliyoteuliwa na Mwalimu Nyerere tarehe 5 mwezi wa kumi mwaka 1976 kuandaa katiba ya chama cha CCM kama sehemu ya kuviunganisha vyama vya ASP na TANU.
Kamati hiyo iliyokuwa chini ya uwenyekiti wa marehemu Thabit Kombo, ilikuwa na wajumbe wengine kama Pius Msekwa,Daudi Mwakawago, Ngombale Mwiru na Hassan Nassor Moyo. Wengine ni Jackson Kaaya,Peter Kisumo,Basheikh Mikidadi, Nikodemus Banduka na wengineo! Hawa ndio makada wakongwe wa TANU na CCM waliotunga katiba ya mwaka 1977 inayotumika hivi sasa.
Katiba ya 1977 ni katiba ambayo licha ya nchi kuwa na wasomi wengi wakati huo, bado watawala hawakuona umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika uundwaji wake.
Prof Issa Shivji katika kitabu chake 'Problems of constitution-making as a consensus-building: The Tanzanian experience'' kinachoelezea pamoja na mambo mengine, matatizo katika uundwaji wa katiba, mwanazuoni huyu nguli wa sheria anasema kamati iliyoteuliwa na Mwalimu Nyerere kuandaa mapendekezo ya katiba mpya ilianza kufanya kazi hata kabla haijateuliwa rasmi. Kwamba baada ya kamati hiyo kuwasilisha mapendekezo yake mbele ya kamati kuu ya CCM, ni siku moja tu kamati kuu ya chama hicho ilitumia kuidhinisha mapendekezo hayo ya katiba kabla ya kuiwasilisha kwenye Bunge la katiba( Constituent Assembly) baada ya siku 7.
Prof Shivji anaongeza kwa kusema kuwa ni saa tatu tu Bunge hilo lilitumia kuipitisha katiba hiyo bila kuijadili. Anasema ''Everything was forced through the throat by the powerful ruling party''. Kwa tafsiri isio rasimi ni kwamba kila kitu kililazimishwa kumezwa na chama tawala. Kwa mazingira kama haya, ni ngumu sana ajenda ya madai ya katiba mpya kukoma.
Katiba ya mwaka 1977 ilianza kukosolewa miaka mitatu mbele(1980) baada ya kukamilika kwake pale ambapo Watanzania hasa kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo CCM, Chama cha Kitaaluma cha Waalimu Tanzania( CHAKIWATA), Chama cha wanasheria(TLS), Jukwaa la wanataaluma chuo kikuu cha Dar es salaam(UDSA) na wengineo.
CCM kupitia kitengo chake cha propaganda na hamasa kilikuja na mapendekezo matano wakitaka katiba ya 1977 ifanyiwe marekebisho. Mosi, walitakata marekebisho kwenye mamlaka ya rais(kuondoa ufalme rajareja), pili walitaka bunge liongezewe mamlaka na tatu walitaka mamlaka ya wananchi yaongoezwe( consolidation of peoples power. Nne, walihitaji bunge la Jamuhuri liongeze wigo wa uwakilishi na mwisho walitaka muungano uimarishwe. Upinzani huu dhidi ya katiba ya mwaka 1977 ndio ulichochea vuguvugu la mjadala mkubwa wa kikatiba uliopelekea aliyekuwa mwanasheria mkuu wa Zanzibar Wolfgang Dourado kuwekwa kizuizini baada ya kutoa mawazo yanayounga mkono muungano wa mfumo wa serikali tatu kwenye kongamano liloandaliwa na TLS mwaka huohuo 1983. Huu ulikuwa ni uonevu usiomithirika uliobarikiwa na watawala akiwemo Judge Joseph Sinde Warioba aliyekuwa mwanasheria mkuu na waziri wa katiba na sheria wa wakati huo.
Mjadala ule wa katiba haukuondoka bila kuacha matokeo chanya licha ya utuli wa serikali ya wakati huo kupinga vikali swala la kurejesha mfumo wa vyama vingi na marekebisho mengine, serikali ilikubali kurejesha muswada wa haki za binadamu kwenye utangulizi wake mwaka mmoja baadae(1984). Sanjali na hilo mjadala pia uliweza kuamsha umma juu ya maswala ya kikatiba na uhuru wa kutoa maoni. Huenda hili lilichangia kung'atuka kwa Mwalimu Nyerere miezi michache baadae!
Hata hivyo, ukweli unabaki pale pale kwamba Tanzania kama taifa, tunahitaji katiba mpya. Lazima tukubali kuwa wakweli hata kama matumbo yetu hayataki kukiri katika hilo. Ninaamini miongoni mwa mambo yanayoangamiza taifa letu kwa kiasi kikubwa ni unafiki, uoga na ujinga. Haya ndiyo yametukwamisha kupata katiba mpya mpaka wakati huu unaosama makala hii. Ninaamini nchi hii inahitaji katiba mpya ili isaidie kutupeka mbele kimaendeleo. Pia ninaamini vita ya kutumbua majipu pekee aliyoanzisha rais Magufuli haitafanikiwa ikiwa taifa litaendelea kukumbatia katiba inayobariki mfumo unaolinda wezi, katiba isiyokuwa na miiko ya uongozi ndani yake. Kwamba ni ruhusa kwa viongozi kuwa wafanyabiashara na ni ruhusa kuficha fedha ughaibuni. Kwamba katiba isiyowapa wananchi mamlaka ya kuwawajibisha viongozi wanaowachagua! Hapana, ni lazima tukubali kuanza upya.
Mwisho, Tanzania ni chi yetu zote bila kujali tofauti zetu za kijamii, kisiasa na kiuchumi. Tujenge mazoea ya kuitetea kwa gharama yoyote bila soni. Tanzania itapata katiba bora kama watanzania wote tukiamua iwe hivyo. Tuunganishe nguvu zetu kama taifa kudai katiba bora.
-Bob Chacha Wangwe
- bobwangwe@gmail.com
1 comment:
Katika kukumbusha mtoa mada hii ya katiba ni kwamba katiba sio msahafu na ukiangalia katiba za mataifa yote duniani yanayofuata katiba kulingana na maoni ya wananchi wake basi hakuna iliyokuwa imeanzia na katiba iliyokuwa imekamilika moja kwa moja bali katiba zao zimekuwa zikifanyiwa marekebisho muda baada ya muda kulingana na wakati na mahitaji husika kuendana na mazingira ya nchi na watu wake. Kwa mfano mtoa mada anasema independence constitution ya Tanzania ya mwaka 1961 haikuwashirikishi? Ndio inawezekana ikawa hivyo kwani hata Marekani katiba yao ya independence constitution ya mwaka 1787 haikuwa shirikishi bali katika kipindi cha zaidi ya miaka mia tatu 300 tangu wamarekani kujipatia uhuru wao wameshaifanyia marekebisho katiba yao mara ishirini na saba 27, na kuwepo mapendekezo zaidi ya kumi na moja elfu na mia tano na kitu ya kufanyiwa marekebisho zaidi katiba hiyo. Kwa hivyo mabadiliko ya katiba Tanzania ni lazima sio kutokana na pressure kutoka kwa baadhi ya watu kama wanavyojinasibu bali katika uhai wa taifa lolote kunakuwa na historia yake aidha itakuwa nzuri au mbaya lakini ni kitu kilichopita na kama nzuri basi ni kuenziwa na kama mbaya basi ni kuujutia huo ubaya na kutoruhusu kutokea tena lakini la misingi na la maana zaidi ni kuangalia mbele katika kudumisha kilicho bora.
Post a Comment