ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 20, 2016

Liyumba kuagwa leo, kuzikwa Morogoro

Mtoto wa marehemu, Moses Amatus, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam jana, alisema mipango na taratibu za mazishi ya marehemu inaendelea kufanyika kati ya ndugu na jamaa.

Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida Nipashe ilipofika nyumbani kwa marehemu, haikushuhudia uwepo wa kiongozi yeyote wa serikali, licha ya marehemu kuwa mmoja wa watu ambao walikuwa na wadhifa mkubwa katika utumishi wa umma.

Liyumba alifariki dunia juzi katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam baada ya kulazwa mwishoni mwa wiki kutokana na kuugua ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu.

“Baba alikuwa akiugua ugonjwa huo kwa muda mrefu lakini hivi karibuni alizidiwa ghafla, hivyo kumpeleka hospitalini kwa matibabu zaidi ingawa alifariki dunai baada ya siku mbili tangu kulazwa,”.

Liyumba lizaliwa mwaka 1948, ameacha watoto saba na kwamba hajaacha mjane kutokana na mke wake kufariki miaka zaidi ya 10 iliyopita.

“Marehemu hakubahatika kuoa tena baada ya mke wake kufariki dunia mwaka 2005,” alisema Moses.

Liyumba aliwahi kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwaka 2009, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 221.

Hata hivyo, alishinda kesi hiyo baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo.

Januari 27, 2009 Liyumba na aliyekuwa Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuidhinisha ujenzi wa majengo pacha ya BoT bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi.

Kabla ya kuanza kusikiliza ushahidi wa kesi hiyo, upande wa mashtaka ulimwachia Kweka na uliwasilisha mashahidi wanane, wakiwamo wakurugenzi wa Bodi ya BoT na vielelezo mbalimbali.

Mahakama hiyo baada ya kusikiliza pande zote, Mei 24, 2010 ilimhukumu Liyumba kwenda jela miaka mwili, baada ya kukutwa na hatia ya kutumia madaraka vibaya akiwa mtumishi na mkurugenzi wa BoT.

Imeandikwa na Christina Mwakangale na Abraham Ntambara

NIPASHE

No comments: