ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 20, 2016

CUF yaibuka kupokea cheti cha shukrani kutoka Nec

Hafla hiyo iliwaleta pamoja wadau 36 kati ya 47 waliopelekewa taarifa za kushiriki, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutohudhuria na CUF kuwakilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Shaweji Mketo, aliyepokea cheti hicho kwa niaba.

Akizungumza na Nipashe juu ya ushiriki wao, Mketo alisema wamefanya hivyo kama wadau walioshiriki uchaguzi na siyo kuzungumzia matokeo ya uchaguzi.

Alisema kwa kauli ya Mwenyekiti kuwa Uchaguzi ulikuwa huru na haki, ni wazi kuwa Uchaguzi wa Zanzibari wa Oktoba 25, mwaka jana, ulikuwa huru na haki , hakukuwa na haja ya kurudia Machi 20, mwaka huu, kwa madai kuwa kulikuwa na kosoro mbalimbali zilizoifanya Zec kufuta matokeo.

“Kwa maana ya uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mimi sina tatizo nao, nina tatizo na uchaguzi wa Zanzibar ambao nao ulikuwa huru na haki,” alisema.

Akitoa shukrani kwa niaba ya waliotunukiwa vyeti hivyo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sist Nyahoza, alisema waliojitokeza kupokea vyeti hivyo ni asilimia 78.72, hali inayoonyesha kukubalika kwa kile kilichofanywa na Tume.

“Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa na ushindani mkali. Nawaona washindani wa karibu wapo na ambao hawajahudhuria naamini walikumbwa na majukumu mengi au mvua, ila wangefika. Siyo rahisi kwa uchaguzi wa ushindani kama wa mwaka huu mshindani wa karibu kuwapo,” alisisitiza.

Alisema hali hiyo inaonyesha kuwa wamekubali uchaguzi kuwa ulikuwa huru na haki na Tume ilifanya kazi nzuri kwa wadau wote.

Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema licha ya kasoro za hapa na pale, maoni ya wananchi na watazamaji wa nje ya nchi, uchaguzi wa mwaka 2015 ulikuwa huru, uwazi na haki.

Alisema ulifanyika kwa kuzingatia taratibu za kisheria na kikatiba na kwamba ulimalizika kwa amani, jambo ambalo wananchi wenye nia njema walikuwa wakiombea.

Jaji Lubuva alisema ufanisi wa uchaguzi huo ni matokeo ya michango ya wadau mbalimbali katika sekta na nyanja mbalimbali wakiwamo serikali, vyama vya siasa, wagombea, asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari, viongozi wa dini na vyombo vya ulinzi na usalama.

Baadhi ya waliotunukiwa ni CCM, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

CHADEMA

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema barua ya mwaliko ilifika na kupelekwa kwa Katibu Mkuu, lakini ofisi kwa sasa inashikiliwa na Kaimu Katibu Mkuu ambaye yupo nje ya Dar es Salaam na Mwenyekiti amefiwa.

Alipoulizwa kama wangeshiriki hafla hiyo na iwapo watakwenda kuchukua cheti husika, alisema ni vigumu kueleza kwa kuwa hawajashika barua husika na halipo katika uamuzi wake.

Alipoulizwa juu ya kauli ya Tume kuwa uchaguzi ulikuwa huru na haki, Makene alisema hakuna kinachoweza kuondoa udanganyifu na hila za uchaguzi uliopita kama sheria ilikiukwa, daftari lilikuwa chafu na utangazaji wa kura ulikuwa tofauti na haviwezi kufutwa kwa maneno hayo.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi na Rais kuapishwa Novemba 5, mwaka jana, Ukawa ilisema haitambui matokeo.

NIPASHE

No comments: