The Hague. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) imeamua Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto hana kesi ya kujibu kuhusiana na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu yaliyokuwa yanamkabili.
Aidha, imeamua pia kwamba mwandishi wa habari, Joshua arap Sang, aliyeshtakiwa pamoja na Ruto, hana kesi ya kujibu.
Ruto alikabiliwa na mashtaka ya mauaji, kuhamisha watu kwa lazima na mateso yaliyotekelezwa wakati wa vita vya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Alikana mashtaka hayo na mawakili wake walitaka kesi hiyo itupiliwe mbali kutokana na ukosefu wa ushahidi.Watu takriban 1,200 waliuawa wakati wa mapigano hayo.
Majaji wamesema kuwa upande wa mashtaka haukutoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai dhidi ya Ruto na Sang.
Hivi karibuni mahakama hiyo ilimfutia mashtaka Rais Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya aina hiyo.
Baadhi ya wachunguzi wa mambo nchini Kenya wanasema kuwa kufutiwa mashtaka kwa mwanasiasa huyo kutamwezesha kutekeleza vyema majukumu yake hatua ambayo itamsaidia pia kupanda kisiasa.
Katika hatua nyingine, Kenya na Ufaransa zimetia saini mikataba mitano itakayogharimu Euro 250 milion kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ikiwamo umeme wa vijijini.
Mikataba iliyotiwa saini inajumuisha ufadhili wa mpango wa usambazaji umeme vijijini maarufu kama “Last Mile Connectivity (Euro 120 milioni), ufadhili kwa miradi wa ujenzi wa barabara kwa jina “Roads 2000” awamu ya pili (Euro 15 milioni, ufadhili wa mradi wa Uzalishaji Kawi kutokana na Upepo na Ufadhili wa Bwawa la Ruiru na Mradi wa msambazaji maji (Euro 19 milioni).
Akiongea na waandishi baada ya kusaini mkataba huo, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliusifu uhusiano kati ya Kenya na Ufaransa. Alitaja Ufaransa kama rafiki na mshirika katika mchakato wa maendeleo.
Mbali na hayo, Rais Kenyatta alisema mazungumzo kati yake na mwenyeji wake, Rais Francois Hollande, yaligusia masuala makuu kama vile usalama.
Ufaransa na Kenya zimeathirika na mashambulizi ya kigaidi jambo ambalo kila mara Kenya imependekeza litatuliwe kupitia ushirikiano wa mataifa yote ya ulimwengu.
Mwanzoni mwa 2016 magaidi walitekeleza shambulio jijini Paris na watu 130 waliuawa.
Mwaka 2015 Al-Shabaab walishambulia Chuo Kikuu cha Garissa na kuuwa watu 147.
Mapema mwaka 2016 kambi ya wanajeshi wa Kenya (KDF) katika eneo la El Adde, Somalia ilishambuliwa na wanamgambo hao ambapo wanajeshi, ambao idadi yao haikujulikana, waliuawa.
Rais Hollande alimwambia mwenyeji wake, Rais Kenyatta, kwamba taifa hilo litashirikiana na Kenya katika vita dhidi ya ugaidi.
“Tumekubaliana kufanya kazi pamoja kwa lengo la kushinda ugaidi. Tutafanya hivyo kwa kuhakikisha kuwa vitengo vyetu kwa ujasusi vinapashana habari” alisema Rais Hollande.
Viongozi hao pia walisema Kenya na Ufaransa zitashirikiana katika nyanja za utekelezaji miradi ya miundombinu, maji na usafi, mazingira, uwekezaji, utamaduni, elimu na michezo.
Kuhusu biashara viongozi hao walikubaliana kuendeleza ushirikiano utakaosababisha Ufaransa kununua mazao kama vile kahawa, chai, matunda, maua na mboga kutoka Kenya.
Kenya hivi karibuni imeingia katika mvutano na Uganda, ikiitaka jirani yake huyo kurudisha mpango wa kulipitisha bomba la mafuta nchini humo (Kenya) badala ya Tanzania.
Baada ya kumaliza ziara yake Paris, Ufaransa aliyoianza Aprili 4 hadi 6 atakwenda Berlin, Ujerumani na kufanya ziara kwa siku mbili nchini humo. Itakuwa ni mara ya kwanza katika miaka 17 kwa Rais wa Kenya kuitembelea Ujerumani.
Mara ya mwisho, ziara ya aina hiyo ilifanywa na Rais Daniel arap Moi mwaka 1999, huku Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel aliitembelea Kenya mwaka 2011.
Ziara ya Ufaransa kwa mujibu wa Ikulu ya Kenya, imeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa mwaliko wa Rais Francois Hollande.
No comments:
Post a Comment