ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 7, 2016

SIMULIZI YA MAKONDA ALIVYONASWA VIBAO

Paul-Makonda
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Na Elvan Stambuli, RISASI mchanganyiko
DAR ES SALAAM: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda Jumapili iliyopita alitoa simulizi ya enzi hizo akielezea jinsi baba yake mzazi alivyomnasa vibao kwa sababu ya kung’ang’ania shule.

Alisimulia mkasa huo wakati akizungumza na watu walioalikwa katika semina maalum ya kampeni iliyoitwa Mimi ni Nani, Shtuka Mapema iliyofanyika katika Ukumbi wa Josam House jijini Dar, ambako alisema baba yake hakusoma hata darasa moja wakati mama yake aliishia darasa la saba, lakini wote wawili hawakujua umuhimu wa elimu.

“Siku moja nilijifungia chumbani nikaanza kulia, mara baba akaja na kunikuta natoka machozi na makamasi, akaniuliza kwa nini nalia, nikamwambia nataka kwenda shule. Nililambwa makofi kwelikweli, sitasahau siku hiyo. Hii ni kwa sababu baba hakujua umuhimu wa elimu,” alisema Makonda.

Akaongeza: “Baba alitaka niwe mkulima wa nyanya kwa sababu siku hizo zao hilo lilikuwa na soko nchini Kenya lakini mama kwa upande wake aliunga mkono ndoto zangu za kusaka elimu.”
Akifafanua zaidi alisema, kutokana na king’ang’anizi chake alifanikiwa kusoma hadi Chuo Kikuu na kuwa rais wa vyuo vikuu vyote nchini na kuleta mabadiliko makubwa kielimu kwani alitetea mambo mengi ya wasomi na yakafanikiwa.
“Hivi sasa baba nikimkatia tiketi ya ndege kuja Dar anasema nikatie ndege ya jioni ndiyo nzuri…” alisema Makonda na kusababisha ukumbi mzima kuangua kicheko. Aliwataka wasomi na watu wengine kutimiza ndoto zao badala ya kutegemea kuambiwa na watu au kusoma vitabu walivyoandika wenzao.

“Unajua kuna mtu aliyegundua umeme utokanao na maji lakini yupo mtu mwingine akakuna kichwa na akafikiri akaona kwa nini asitengeneze umeme kwa kutumia jua, akafanikiwa, mwingine akaona kwa nini asitengeneze umeme kwa kutumia makaa ya mawe, akajaribu na kufanikiwa… huu ndiyo ubunifu unaotakiwa,” alisema.

Katika semina hiyo wanasemina walihimizwa kufanyia kazi ndoto zao ambapo Kampuni ya Global kupitia kwa mwakilishi wao, Elvan Stambuli iliwaomba washiriki kucheza Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba kwa kukata kuponi zinazopatikana katika magazeti ya Risasi, Uwazi, Amani, Wikienda, Ijumaa na Championi ili kujiongezea fursa ya kujishindia nyumba ya kisasa.

GPL

No comments: