ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 21, 2016

WATOTO WAWILI WAFIA KWENYE SHIMO LA MAJI

By Salim Mohammed, Mwananchi

Tanga. Watoto wawili wakazi wa Kange Kasera mkoani hapa wamefariki baada ya kutumbukia kwenye shimo la maji lililopo nje ya nyumba ya jirani yao.

Watoto hao, Antony Godfrey mwenye umri wa miaka mitatu, na Emmanuel Aidan (4) walitumbukia kwenye shimo hilo jana saa 4:00 asubuhi.

Baba mzazi wa Antony, Godfrey Komba alisema alipata taarifa za mtoto wake kufa maji akiwa njiani wakati akitokea kazini.

Alisema wakati akikaribia nyumbani kwake alimkuta mke wake, Flora Vicent akilia na majirani wakiwa wamekusanyika kwa wingi.

“Hapa jirani kuna shimo la choo liko mbele ya mlango wake na lilikuwa limejaa maji mengi na lilikuwa halijafunikwa. Watoto wangu na wajirani wamekuwa wakicheza na mara nyingi nilikuwa nikiwambia wasicheze karibu na lile shimo,” alisema Komba.

“Tukio limeshatokea sina la kusema na kwa sasa ndio tunashughulikia mazishi,” alisema.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Leonard Paul alisema tayari polisi wamepata taarifa ya tukio hilo na jeshi lake linafanya uchunguzi kuona kama kulikuwa na uvunjwaji wa sheriw wakati wa ujenzi ulioambatana na uchimbaji wa shimo hilo.

No comments: