
Mchezaji wa Ndanda, Paul Ngalema (kushoto) akimdhibiti mchezaji wa Yanga, Simon Msuva katika mchezo wa Kombe l
a FA kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. Yanga ilishinda 2-1. (Picha na Yusuf Badi).
YANGA na Azam jana zilitinga hatua ya Nusu Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kushinda michezo yao ya Robo Fainali.
Yanga ilikuwa mwenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, wakati Azam ilikuwa mwenyeji wa Prisons Uwanja wa Azam Chamazi na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Kutokana na ushindi huo, Yanga na Azam sasa zinaungana na Mwadui ya Shinyanga, ambayo Jumamosi iliifunga Geita Gold Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mabao 3-0 na kufuzu Nusu Fainali. Bingwa wa michuano hiyo inayojulikana pia kama Kombe la FA, atawakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) mwaka 2017.
Katika mchezo wa jana, Ndanda ilikuwa ya kwanza kufanya shambulio la kushtukiza dakika ya sita wakati Atupele Green alipoukwamisha mpira wavuni, lakini mwamuzi alisema mfungaji alikuwa ameotea kabla ya kufunga, hali ambayo ililalamikiwa na wachezaji wa Ndanda.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, huku Yanga ikipoteza nafasi nyingi zaidi kwa washambuliaji wake kushindwa kulenga lango. Yanga ilipata bao la kuongoza dakika ya 27 mfungaji akiwa Paul Nonga akiunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu wa Juma Abdul.
Ndanda FC ilisawazisha bao hilo dakika ya 56 mfungaji akiwa Kigi Makasy baada ya kuingia katika eneo la hatari na kupiga mpira uliomshinda kipa Deogratias Munishi ‘Dida’.
Yanga ilipata bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 69 mfungaji akiwa Kelvin Yondani, baada ya beki Paul Ngalema kumchezea madhambi Simon Msuva aliyekuwa akienda langoni, ambapo kutokana na faulo hiyo Ngalema alioneshwa kadi nyekundu na mwamuzi Jimmy Fanuel wa Shinyanga.
Katika mchezo wa Azam, washindi walianza kupata bao la kwanza dakika ya tisa mfungaji akiwa Shomary Kapombe aliyemalizia kazi nzuri ya Didier Kavumbagu.
Kapombe aliifungia Azam bao la pili dakika ya 50, wakati Khamis Mcha aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi John Bocco ‘Adebayor’ alifunga bao la tatu dakika ya 86.
Robo Fainali nyingine ya michuano hiyo itakuwa Aprili 9 mwaka huu, wakati Simba itakapokuwa mwenyeji wa Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment