ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 20, 2016

ALAMA ZA JUMUIYA AFRIKA MASHARIKI KUTUMIKA KATIKA TAASISI ZA SERIKALI

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga, akiongea na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, ambapo alizungumzia matumizi ya Alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Bendera na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Taasisi za Serikali. 
Mkurugenzi wa Masomo katika Chuo cha Diplomasia Dkt. Watengere Kitojo (kushoto) pamoja na Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Robi Bwiru. 
Bi. Mindi Kasiga akiendelea kuzungumza na Waandishi wa Habari. 

Mkurugenzi wa Masomo katika Chuo cha Diplomasia, Dkt. Watengere Kitojo naye akizungumza kuhusu Kozi zinazotolewa na chuo hicho ikiwemo Cheti, StaShahada, Shahada katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, 
Sehemu ya Waandishi wa Habari waliojitokeza kwenye mkutano huo, katikati ni Afisa kutoka Habari Maelezo Bi. Immaculate Makilika akifuatilia kwa makini mkutano. 

Matumizi ya Alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inatoa wito kwa Taasisi za Serikali kuhakikisha kuwa zinatumia alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni Bendera na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Alama hizo zinatakiwa kutumika kwenye Ofisi za Serikali (Wizara, Idara zinazojitegemea,  mashirika ya umma na Wakala) sambamba na alama za Taifa yaani Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wimbo wa Taifa. 
Bendera ya Jumuiya inatakiwa kupepea sambamba na Bendera ya Taifa kwenye Ofisi za Serikali na Wimbo wa Jumuiya  nao unatakiwa kuimbwa sambamba  na Wimbo wa Taifa wakati wa shughuli rasmi za Kiserikali. 
Hatua hiyo ni utekelezaji wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao katika kifungu cha 7(a) umesisitiza Jumuiya hii kuwa ni Jumuiya ya watu, hivyo wananchi wa Tanzania watahusishwa katika hatua zote za Mtangamano. Aidha,  Serikali ya awamu ya tano (5) chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itahakikisha kuwa Watanzania wanashirikishwa kikamilifu katika hatua mbalimbali za Jumuiya ili kuijua kwa madhumuni ya kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya Jumuiya hiyo.
Matumizi ya alama hizi ni njia mojawapo ya kujenga uzalendo na kumfanya Mwananchi ajisikie kuwa sehemu ya Ushirikiano huu. Aidha, Taasisi binafsi hasa Mashule na Vyuo wanasisitizwa kutumia alama hizi kama sehemu ya kuelimisha na kuhamasisha vijana kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaratibu zoezi la upatikanaji wa sampuli ya alama hizo kwa gharama za taasisi husika, hivyo Wizara, Taasisi na Ofisi za Serikali zinahimizwa kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa ajili ya ufafanuzi zaidi wa upatikanaji na matumizi ya alama hizo.
MAZUNGUMZO YA USULUHISHI WA MGOGORO WA BURUNDI
WAKATI HUOHUO, Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataongoza mazungumzo kuhusu mgogoro wa Burundi yanayotarajiwa kuanza tarehe 21 hadi 24 Mei, 2016 katika Ukumbi wa Mikutano wa AICC – Arusha.
Katika mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifafanua kuwa Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni ataendelea kuwa  msuluhishi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuteua timu ya Usuluhishi ambayo itaongozwa na Mhe. Benjamin William Mkapa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Waandishi wa Habari wataruhusiwa kwenye siku ya Ufunguzi wa Mkutano huo na siku ya kufunga Mkutano tu. Aidha, waandishi wanahimizwa kujisajili ili kupata vitambulisho vya kuingia kwenye mkutano. Usajili utafanyika AICC-Arusha tarehe 20 Mei, 2016 saa 8:00 mchana chumba namba 541, ghorofa ya tano, upande wa Kilimanjaro.
Au unaweza kutuma maelezo ya Press Card yako, picha ya ndogo (passport size) kwenye email ifuatayo; media@eachq.org, CC:oothieno@eachq.org.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 19 Mei 2016.

No comments: