ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 16, 2016

DART KUKABILIANA NA VITANZI VITANO

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo akikagua mashine za kadi za kielektroniki zitakazotumiwa na abiria katika kituo cha mabasi yaendayo haraka Kimara, Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao 

Wakati wakazi wa Dar es Salaam wakianza kulipia huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka kuanzia leo, changamoto tano zimeibuliwa na kuagizwa zishughulikiwe haraka ili kupunguza kero kwa abiria na kufanikisha mradi huo.
Awali, uongozi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart) ulitoa siku mbili za majaribio ambazo abiria walikuwa wakisafiri bure kabla ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuongeza siku tano baada ya kushauriana na uongozi huo kwa lengo la kuwaelimisha zaidi watumiaji. Tayari siku saba za majaribio ya utekelezaji wa huduma hiyo zimekamilika jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jaffo alisisitiza kushughulikia changamoto tano zilizopo baada ya kufanya ziara yake jana.
Changamoto
Alilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linaimarisha ulinzi wa njia za mabasi hayo na kutoa elimu ya matumizi ya alama za kuvuka kwa abiria, kengele na milango.
Changamoto nyingine ni Dart kuimarisha usafi wa mazingira vituoni ili kudhibiti kuzagaa kwa taka na kuwa na vifaa vya kutosha vya kuhifadhi taka.
Nyingine ni kukamilisha matumizi ya mfumo wa malipo kwa njia ya kadi ili kutambua wanafunzi na watu wazima na changamoto ya mwisho ni abiria kupinga matumizi ya daraja na badala yake kutumia njia za mkato.

Ushauri wa waziri
Akizungumzia changamoto hizo, Jaffo alisema ili mradi huo ufanikiwe wasimamizi wake hawana budi kuzitatua.
“Tunataka changamoto zote hizi zikamilike mara moja ili lengo la mradi lifanikiwe, bodaboda na abiria watii utaratibu uliopo na polisi mnatakiwa kuimarisha ulinzi wa kutosha… mradi huu ni bora kwa nchi zote za Afrika Mashariki kwa hivyo tuulinde,” alisema.
Jaffo aliwaahidi wakazi wa jiji hilo kuendelea na miradi mingine ya awamu ya pili na tatu kupitia mradi huo wa mabasi yanedayo haraka katika barabara za Mbagala – Posta na Uwanja wa Ndege – Posta. “Lakini baadaye lengo la Serikali ni kuwa na barabara hizi sehemu nyingi kwa ajili ya usafiri wa haraka.”
Kwa mujibu wa Udart, wastani wa mabasi 140 yataanza kutoa huduma hiyo kwa nauli ya Sh200, Sh400 hadi Sh800.
Pamoja na gharama hizo za nauli, Rais John Magufuli alinukuliwa akisema kupungua kwa msongamano wa foleni katika jiji hilo kutaokoa mabilioni ya shilingi. Alisema ripoti ya Ofisi ya Takwimu, 2013 pekee inaonyesha tatizo la foleni katika jiji hilo lilisababisha kupotea kwa Sh411.3 bilioni.
Katibu wa Kamati ya Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Peter Sima aliahidi kushughulikia changamoto hizo ili kuimarisha usalama kwa abiria wanaotumia usafiri huo. “Lakini ningewataka bodaboda kutii utaratibu uliowekwa kwa sababu itakuwa ni kwa ajili ya kulinda hata usalama wao pia, nisingependa kuwaona wakipita kwenye alama za pundamilia (zebra) hata waendesha baiskeli washuke ili kuwa na usalama zaidi,” alisema.

Vioja na utaratibu uliopo
Miongoni mwa vituko vilivyoonekana ni pamoja na abiria aliyekuwa akitoka Kituo cha Morocco kwenda Kimara kung’oa vishikio vya abiria wanaosimama ndani ya mabasi hayo wakati akisukumana na wenzake.
Pia, kuna wengine walikuwa wakibonyeza kengele zinazotoa ishara ya kufungua mlango kuruhusu watu kutoka nje.
Kituko kingine ni mvutano kati ya walinzi wa Kampuni ya China-Tanzania Security (CTS) na abiria waliokuwa wakipinga kutumia madaraja makubwa kuingia na kutoka katika vituo vya usafiri huo na badala yake wakitaka kutumia njia za mkato, wengine waligombania usafiri na wakati mwingine kutojali maelekezo ya kipaza sauti wakiwa ndani ya usafiri huo.

Hatua sita za kupanda hadi kushuka
Utaratibu wa kupanda hadi kushuka kwenye mabasi hayo una hatua sita.
Kwanza abiria atatakiwa kuingia kituoni, kununua kadi itakayotumika kila atakapohitaji kusafiri, kupita kwenye geti litakaloitambua kadi hiyo.
Hatua ya nne ni kuelekea kwenye viti vya kupumzikia abiria wanaosubiri usafiri, kila abiria kutakiwa kufuata maelekezo ya kipaza sauti kabla ya kuingia ndani ya basi na mwisho, abiria akiwa ndani ya basi, atatakiwa kufuata maelekezo ya kipaza sauti kinachomwelekeza mambo ya kuzingatia.

No comments: