Huduma hiyo ilianza jana kati ya saa tano asubuhi na kubeba abiria bila kulipia, kabla ya kuanza kulipa kuanzia kesho kwa nauli ya kati ya Sh 650 na 800 kwa safari moja. Usafiri huo ulianza jana na kwa mabasi machache na kwa siku mbili wananchi hawatalipa nauli na kazi inayofanyika ni kutoa elimu kwa wananchi wakiwa ndani ya mabasi ya namna ya kutumia mabasi hayo.
Pindi abiria anapoingia ndani ya basi, dereva anataja jina lake na kutangaza mwanzo na mwisho wa safari na kutoa tahadhari ya kutosimama maeneo yaliyokatazwa ya karibu na mlango, kuacha maeneo ya watu wenye ulemavu na kuzingatia usafi kwa kutupa taka katika visanduku vya taka vilivyoweka ndani ya basi.
Hata hivyo, siku ya jana, maofisa wa UDA-RT walikuwa na kazi ya kuwafundisha wananchi namna ya kutumia kadi (tiketi) ambazo baada ya kulipia unatakiwa kuipitisha kwenye mashine kabla ya kizuizi kufunguka.
Mabasi hayo yamekuwa yakitumia kati ya dakika 48 hadi 50 kutoka Kivukoni hadi Kimara Mwisho, dakika 30 kutoka Kivukoni au Kariakoo kwenda Morocco huku muda wa kusimama katika kituo ni sekunde 30.
Kutokana na wingi wa abiria kwenye vituo na uzito wa abiria kufuata maelekezo, madereva wamekuwa wakilazimika kutumia muda zaidi kituoni, kwani walinzi walilazimika kupunguza abiria kutokana na kujaa kabla ya kuruhusu kuendelea na safari.
Dereva Hipohiti Mallya anayeendesha moja ya mabasi hayo, alisema kumekuwapo na idadi kubwa ya abiria ambao anaamini watapungua pindi watakapoanza kutoza nauli. “Watu wanasimama eneo ambalo linakatazwa na kutofuata taratibu, lakini hizi ni changamoto za muda.
Safari yangu moja nimebeba zaidi ya watu 220, ikiwa ni zaidi ya kiwango kinachotakiwa,” alisema Mallya. Naye abira Yunusi Meshack ambaye ni mkazi wa Kimara Korogwe, alisema amefurahia utaratibu wa safari hizo na kuwa nauli ya Sh 650 kwake anaona ni nafuu kulingana na huduma inayotolewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa UDART, David Mgwasa alisema katika siku ya kwanza wameshindwa kufuata ratiba ambayo wamewekewa kutokana na upya wa huduma hiyo kwa wananchi. Alisema kadri siku zitakavyoendelea kusonga mbele, watahakikisha wanafuata ratiba ya kukaa sekunde 30 katika kila kituo bila kujali gari lina abiria au la.
Alisema changomoto ya pili, ni tabia ya wananchi ya kutaka kugombea wakati wa kuingia badala ya kufuata utaratibu wa kupanga foleni sambamba na matumizi ya viti vilivyotengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
“Kesho (leo) tutaanza asubuhi sana, lengo ni kuona namna ya kukabiliana na msongamano wa watu,” alisema. Asubuhi Abiria walionekana kuwahi vituoni kwa imani ya kutumia usafiri huo na kujikuta wakisubiri muda mrefu vituoni bila mafanikio.
Gazeti hili lilizunguka katika vituo kadhaa kuanzia Ubungo-Magomeni- Morocco ambako kulikuwa na umati ambao ulikuwa ukisubiri huduma hiyo. Baada ya kuona usafiri huo haupatikani, baadhi ya wananchi walilazimika kutumia usafiri wa magari madogo na bajaji ambazo zimekuwa zikitoza nauli kuanzia Sh 2,000 kutoka Ubungo hadi Posta au Kariakoo kwa mtu mmoja.
Katika kituo cha Kivukoni wafanyakazi wa UDA-RT walifika kufungua milango kwa ufunguo maalumu huku baadhi ya wananchi ambao walishuka kwenye kivuko na kuingia ndani ya kituo saa 3:50 wakipitia geti la kutokea mabasi.
Akizungumzia hilo, Meneja Uhusiano wa UDA-RT, Deus Bugaywa ambaye alisema taarifa zilizotolewa awali kuwa mabasi yangeanza saa 11 asubuhi, ilikuwa ni ratiba ya mabasi kwa kila siku.
Alisema ofisi yake iliamua kuanza saa nne wakati wa idadi ndogo ya abiria ili kutoa nafasi kwa watumishi wa mabasi hayo kupata uzoefu kabla ya kuanza kuhudumia nyakati za msongamano wa abiria jioni na leo asubuhi.
Vituko Pamoja na UDA-RT kuamua kutoa huduma hiyo nyakati za abiria wanapokuwa wachache, lakini kulikuwa na mwitikio mkubwa wa abiria kutumia huduma hiyo iliyokuwa ikitolewa bure kwa jana na leo.
Hata hivyo, usafiri huo umekumbwa na changamoto kubwa hasa kutokana na watu kutoshuka kwenye mabasi na kujikuta wakifanya utalii wa ndani kwa kuzunguka na usafiri huo bila kushuka.
Hali hiyo ya wingi wa watu iliwafanya madereva kushindwa kusimama kwenye baadhi ya vituo na kuwatangazia wananchi wanaotaka kushuka kuhakikisha wanabonyeza kengele ambazo zinatoa ishara kwa dereva, lakini baadhi ya abiria wamejikuta wakiwataka madereva kusimama kwa kupiga kelele za ‘nishushe.’
Katika Kituo cha Posta ya Zamani watu walilazimika kupitia pembeni badala ya kituo kutokana na kutofunguliwa kwa vituo vingi huku vingine vikiwa havijafanyiwa usafi. Pia wapo waliotumia fursa hiyo kupiga picha wakiwa ndani ya mabasi hayo na wale waliopiga simu kuwajulisha ndugu na jamaa kuwa yuko kwenye mabasi yaendayo haraka.
Wengi wa abiria waliopanda basi wanaendelea na utaratibu wa kugombea kwa lengo la kupata viti, lakini juhudi hizo zinakuwa hazina matunda kwa kukuta abiria waliofika na basi hilo kutoshuka.
Pamoja na juhudi za maelezo ya madereva na askari walikuwa hawana sare, lakini kufuata maelekezo imekuwa ngumu hasa katazo la kukaa mlangoni, kukaa eneo lililotengwa kwa ajili ya walemavu wa viungo na wasioona.
Katika kituo cha Kimara Mwisho, Mkurugenzi Mtendaji wa UDA-RT, David Mgwasa alifanya kazi ya ziada kwa kuingia kwenye kila gari na kuwakataza na kutoa elimu ya abira kutokaa kwenye viti vilivyotengwa kwa ajili ya walemavu wa viungo na wale wasioona hata kama abiria hao hawapo.
“Hizi ni alama za watu wenye ulemavu, wewe kama mzima usikae hapa, ni lazima mjenge tabia ya kuheshimu hili. Mkisema kwa sababu hawapo ndio mkae tabia hii itazidi kujengeka,” alisema huku baadhi ya abiria wakitaka kukaa katika viti hivyo kutokana na kutokuwapo na watu wenye ulemavu.
Watumiaji wengine wa barabara Baadhi ya watumiaji wengine wa vyombo vya moto kama magari madogo, bajaji, bodaboda na guta bado wameonekana kuendelea kutumia miundombinu hiyo pamoja na kuwepo kwa katazo.
Tatizo lingine lipo kwenye makutano pale ambapo taa zinapozuia kupita katika upande mmoja wa barabara, lakini waendesha bodaboda na bajaji bado wamekuwa wakionekana kuchomoka ghafla jambo ambalo linafanya mabasi hayo kufunga breki au kukosakosa kuwagonga.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga alikiri kuwa pamoja na jana kuwa siku ya kwanza, bado changamoto ya watumiaji wa vyombo vya moto kuendelea kutumia barabara hizo ipo. “Tumeanza vizuri, lakini bado kuna watu ambao wanatumia barabara za DART wakati hawatakiwi kuzitumia.
Leo tumeongeza askari wa barabarani zaidi ili kudhibiti hali hii, pamoja na kuwa idadi imepungua lakini wapo na sisi tumejipanga kuhakikisha hawatumii kabisa,” alisema Mpinga.
Lakini tatizo lingine limeonekana kwa wananchi wanaotembea kwa miguu kushindwa kufuata utaratibu na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuvuka na badala yake wamekuwa wakikimbiakimbia wakati wa kuvuka .
Kadi maalumu Bugaywa alisema kutakuwa na kadi maalumu ambazo zitauzwa kwa Sh 500 kama promosheni ambayo abiria atatakiwa kuwa nayo na kuongeza fedha kupitia miamala ya simu.
Alisema kadi hizo takribani 100,000 zitauzwa watakapoanza kutoza nauli na mwenye kadi atatakiwa kuitunza na endapo ataipoteza atatoa taarifa UDART itakayomtengenezea nyingine na kurejesha fedha zitakazokuwamo.
Waziri Mkuu anena
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema anaamini taasisi inayoshughulika na kusimamia suala la mabasi yaendayo haraka itahakikisha yanatoa huduma kama ilivyopangwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu usafiri wa mabasi hayo chini ya usimamizi wa UDA-RT, alisema usafiri huo umeanza kwa kutoa elimu kwa wananchi na watumiaji wa usafiri huo na kwamba utatekelezwa vizuri kama ulivyopangwa.
Waziri Mkuu alihimiza wananchi na watumiaji wengine wa barabara kuhakikisha wanaipata elimu hiyo ili wafuate sheria na taratibu zilizowekwa za matumizi ya usafiri huo utakaosaidia kusafirisha abiria kwa muda mfupi.
“Utaratibu wa barabara umewekwa wa magari ya kawaida, na vyombo vingine vya usafiri na barabara za mabasi yaendayo haraka… kuanzia sasa lazima watu wafahamu barabara za mabasi yaendayo kasi ni kwa ajili ya magari hayo tu,” alisema Majaliwa.
Kuhusu nauli, Waziri Mkuu Majaliwa alisema tayari zimeshatangazwa na kwamba zimezingatia hali halisi ambazo ni Sh 400, 650 na 800 kulingana na maeneo husika. Habari hii imeandikwa na Anastazia Anyimike na Angela Semaya.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment