ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 11, 2016

MIGAHAWA ZANZIBAR KUANZA KUFUNGULIWA

By Hassan Ali, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Zanzibar. Wizara ya Afya Zanzibar inatarajia kuanza kuondoa karantini na zuio la uuzaji wa vyakula hadharani na ndani ya migahawa, kufuatia ugonjwa wa kipindupindu kupungua.

Karantini hiyo ya Serikali ilitolewa kutokana na mlipuko wa kipindupindu ulioigubika Zanzibar tangu Septemba 2015, huku watu kadhaa wakipoteza maisha na kuwakumba zaidi ya 2,000.

“Yalikuwa ni mazingira magumu, tangu jana nimeshindwa kupata chakula na mpaka sasa asubuhi sijaona pa kupatia chai,” alilalamika Mitchell Stanley ambaye ni raia wa Uingereza aliyekuwa visiwani hapa kikazi mwishoni mwa wiki.

Jana, Wizara ya Afya ilisema inatarajia kuanzia wiki hii kufungua migahawa ambayo ilifungwa.

Mkurugenzi wa Kinga wa wizara hiyo, Dk Mohammed Dahoma alisema wameamua kuifungua migahawa hiyo ili kuwapa nafasi wafanyabiashara kufanya kazi za utoaji wa huduma ya chakula kwa jamii.

Alisema ufunguzi wa migahawa utaanzia katika Kanda ya Mjini kwa kuanzia na maeneo 39 na matayarisho yamekuwa yakiendelea ikiwa ni pamoja na kuagalia vigezo vya kisheria na afya ya wahusika.

Dk Dahoma alisema migahawa ambayo itakidhi vigezo itapata leseni za kufanya biashara na itakayoshindwa itaendelea kufungwa hadi itakapokamilisha utaratibu wa kisheria.

Alitaja baadhi ya vigezo hivyo kuwa ni pamoja na kuwa na vyoo viwili, mabomba mawili ya maji baridi na moto, eneo kubwa la watu kula vyakula, chumba maalumu cha dharura, madirisha makubwa na mazingira safi.

Dk Dahoma alisema pamoja na vigezo hivyo, wizara itafuatilia usafi wa mazingira ya biashara.

No comments: