ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 10, 2016

MABASI YAENDAYO HARAKA HATIMAE KUANZA KAZI LEO

Mabasi yaendayo kasi yakiwa katika kituo kikuu cha mabasi hayo, Kariakoo.
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imetangaza nauli zitakazotumika kwa mabasi yaendayo haraka kuwa ni Sh 800 kutoka Mbezi hadi Kivukoni huku mwanafunzi akilipa Sh 200 kwa njia zote.

Aidha, usafiri huo unatarajia kuanza leo kwa mabasi machache na kwa siku mbili wananchi hawatalipa nauli kazi itakayofanywa na Kampuni ya UDA-RT. Akizungumza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema nauli hizo zimepitishwa na Bodi ya Sumatra baada ya kutafakari viwango vilivyotokana na ukokotoaji uliozingatia masuala muhimu ya uendeshaji na kuwa nauli hizo zitaanza kutumika keshokutwa Alhamisi.

Ngewe alisema njia ya pembezoni (kutoka Mbezi Mwisho hadi Kimara Mwisho) itakuwa Sh 400, njia kuu ya Kimara-Kivukoni, Kimara-Kariakoo, Kimara-Morocco, Morocco- Kivukoni, Morocco- Kariakoo na Kariakoo- Kivukoni itakuwa Sh 650.

Alisema pia nauli ya pembezoni wameweka Sh 400 kutokana na kuwa UDA-RT itakuwa ikitoa huduma sambamba na mabasi ya kawaida ya daladala hivyo kuweka usawa wa nauli na kusisitiza kuwa mpango wa biashara uliowasilishwa na UDA-RT ulikuwa na mapungufu.

Awali, UDA-RT ilipeleka mapendekezo ya nauli Sumatra ikionesha njia za pembezoni kuwa Sh 700, njia kuu Sh 1,200 na njia kuu na pembezoni kuwa Sh 1,400 na mwanafunzi akitakiwa kulipa nusu ya nauli ya mtu mzima.

Hata hivyo, Sumatra ilifanya mkutano wa kupokea maombi kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo watumiaji wa huduma hii kwa mujibu wa sheria, uliofanyika Januari 5, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Aidha, Sumatra imekabidhi UDART leseni ya kutoa huduma hiyo ya mwaka mmoja itakayoishia Mei 8, mwakani. “Tunajua kuwa Kampuni ya UDA-RT inatakiwa kuendesha kwa miaka mwili kabla ya kuipata kampuni halisi itakayofanya kazi hiyo, tumempa leseni ya mwaka mmoja na wiki nne kabla ya kuisha kwa leseni hiyo wanatakiwa kuja kuomba tena kama wanaona wanataka kuendelea,” alisema Ngewe.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), Ronald Lwakatare alisema usafiri wa mabasi ya haraka utaanza leo kwa kuanza na mabasi machache ambapo wananchi watapanda mabasi hayo bure kwa siku mbili lengo ni kutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi.

“Tutatumia siku mbili kutoa elimu kwa wananchi wakiwa ndani ya mabasi, hivyo watasafiri bure na wakiwa humo watapewa elimu ya matumizi ya mabasi hayo,” alisema Lwakatare.

HABARI LEO

No comments: