Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Msabaha (Chadema) ametoa tuhuma nzito kuwa ndani ya Bunge kuna wabunge vijana wanaovuta bangi na kutumia dawa za kulevya.
Mbunge huyo amemuomba Rais John Magufuli kuagiza wabunge wa aina hiyo ambao hata hivyo hakuwataja wapelekwe Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kufundishwa nidhamu.
Msabaha ametoa kauli hiyo Bungeni mjini Dodoma wakati akichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya Ulinzi na JKT iliyowasilishwa na Waziri mwenye dhamana na Wizara hiyo, Dk Hussein Mwinyi.
“Wabunge nao waende JKT kwa sababu hili Bunge wameingia vijana wengine ambao ni mateja wa unga na wengine wanavuta bangi. Wengine wanawavua mama zao nguo,” amesema Msabaha.
“Wengine mama zao wameshakufa wanakuja humu wanawatukana mpaka wazazi wao. Kwa hiyo niombe Rais Magufuli vijana wote wabunge ambao hawana nidhamu waende JKT,” alisisitiza.
Mbunge huyo amesema wabunge wa aina hiyo hawana viwango vya kuzungumza ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria hivyo ni vyema waende JKT ili wakirudi wawe wamejua namna ya kuchangia.
Ingawa hakumtaja Mbunge yeyote, lakini mchango ulioibua mtafaruku bungeni ni wa Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga aliyedai wabunge wa viti maalumu Chadema huitwa Baby ili kupewa nafasi hiyo.
Tafsiri ya kauli hiyo ni kuwa wabunge wa viti maalum Chadema lazima wafanye mapenzi au kuwa na mahusiano na viongozi wa juu wenye mamlaka ndani ya chama hicho ndipo wateuliwe kuwa wabunge.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment