Advertisements

Wednesday, May 25, 2016

MBUNGE WA JIMBO LA KIBAHA MJINI AWAPATIA MSAADA WAHANGA WALIOKUMBWA NA JANGA LA MOTO

Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka akikagua moja ya sehemu ya vibanda vya biashara vilivyopo katika eneo la maili moja baada ya kuteketea kwa moto na kuweza kuunguza maduka matano moto huo ulizuka hivi karibu.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka akimkabidhi mmoja wa wahanga waliounguliwa maduka yao eneo la maili moja kiasi cha shilingi laki tano ikiwa ni kuwapa msaada wa kuanzia mtaji mwingine alipofanya ziara ya siku moja ya kuwapa pole.(PICHA NA VICTOR MASANGU)


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA 
WIMBI la kutokea kwa majanga ya moto bado limeonekana bado kuwa ni tatizo sugu kutokana na kuwepo kwa uelewa mdogo kwa wananchi kuhusiana na namna ya kuweza kuzuia majanga ya moto pindi yananapojitokeza pamoja na kutokuwa na vifaa vya kuzimia.

Hayo yamebainishwa na Afisa uhusiano wa Jeshi la zima moto na uokoaji Mkoa wa Pwani Harryson Mkonyi wakati akizungumza katika mkutano maalumu wa kuwafariji na baadhi ya wahanga ambao ni wafanyabiashara waliounguliwa maduka yao na kuteketeza mali zao zote kwa moto katika eneo la maili moja Wilayani Kibaha.

Mkonyi amebainsiha kuwa wamebaini kuna baaadhi ya wananchi pindi wanapokumbwa na ajali ya moto wanajikuta wanashindwa kuuzima na kuuzuia usiendelee kusambaa katika maeneo mengine kutokana kutokuwa na vifaa, kuwa na uelewa mdogo juu ya uzimaji wa moto pamoja na kuchelewa kutoa taarifa katika vyombo vinavyohusika.

“Kwa sasa kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa na uelewa juu ya kupambana na majanga ya moto pindi yanapotokea, tumeanza kutoa elimu katika sehemu mbali mbali ili kuweza kuwafundisha jinsi ya kuzuaia moto kwani wakati mwingine wanachelewa kutoa taarifa kutokana na kuamua kuuzima wenyewe na unaposambaa ndipo wanatoa taarifa,”alisema Mkonyi.

Akisoma risala kwa niaba ya wahanga hao wa moto Tatu Jamaly pamoja na mmoja wa wafanyabishara waliokumbwa na majanga hayo ya moto Marietha Massaji wamesema kwamba kwa sasa wamejikuta katika wakati mgumu sana kutokana na biashara ambazo walikuwa wanazitegemea kwa ajii ya kujipatia kipato cha kila siku imeteketea yote kwa moto huo.

“Tulikuwa na tunafanya biashara zetu na zilikuwa zinatusaidia sana katika kujipatia kipato lakini ndio hivyo tena tumepata majanga ya moto na mali zetu zote zimeteketea, lakini tunamshukuru sana mbunge wetu wa jimbo la Kibaha mjini Silvesty Koka kwa kwa moyo wake wa dhati kwa kutuchangia fedha amabazo zitatusaidia kuanza tena biashara zetu,”alisema Wahanga hao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa maili moja Athumani Chichi alisema kwamba kutokana na wafanyabishara hao kupatwa na matatizo wamerudishwa nyuma kimaendeleo na kuongeza kwamba ataendelea kushirikiana na mbunge wa jimbo la Kibaha kwa hali na mali kutokana na kupenda maendeleo na kuwasaidai wananachi wake pindi wanapopata matatizo.

Naye Mbunge wa jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ambaye alifanya ziara ya kuwatembelea wahanga hao wa moto ambapo amewaasa amewachangia kiasi cha shilingi laki tano kwa kila mfanyabiashara ambaye duka lake limeungua na moto na kuwaasa kutokukata tamaa na badala yake mtaji mwingine huo aliowapatia wautumie vizuri katika kukuza biashara zao na sio vinginevyo.

Koka alisema kwamba anatambua uchungu walionao wahanga hao ambapo ameahidi kuendeea kuwasaidia na kushirikiana nao bega kwa bega katika kuhakikisha wanatimiza malengo yao kupitia shughuli zao za ujasiliamali wanazozifanya.

MOTO huo ambao ulizuka katika eneo la maili moja Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani umeweza kuteketeza maduka matano pamoja na mali za wafanyabiashara,wa aina mbali mbali lakini haukuweza kuleta madhara yoyote kwa binadamu .

No comments: