Wakazi wa Kijiji cha Nala na vitongoji vyake juzi walimpelekea maji
machafu Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na
Walemavu Anthony Mavunde wakimtaka ayanywe kwa kuwa ndiyo wanayotumia.
Mavunde
alikutana na mkasa huo muda mfupi alipoingia kwenye kijiji hicho umbali
wa kilomita tisa nyakati za jioni, ambako wakazi wa eneo hilo walikuwa
wakimsubiri tangu asubuhi.
Mama mmoja aliyekuwa eneo hilo, alifika na
chupa ya maji akimtaka Naibu Waziri ayaonje mbele yao, kwani nao ni
binadamu kama yeye na wanayatumia, lakini Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya
Dodoma Mjini, Paul Luhamo alimzuia kuyanywa.
Pamoja na taarifa
ya kijiji iliyotolewa na Ofisa Mtendaji wa Kata, Mathias Ndologa, wakazi
hao walilipuka na kupiga kelele wakiipinga taarifa hiyo kwamba iligusa
kwa juu matatizo yao, lakini ikaacha jambo kubwa la maji.
Kwenye
risala yake, Ndologa alikuwa ameelezea suala la maji, umeme,
miundombinu na upungufu wa madawati, lakini kelele zilizidi kutoka kwa
wananchi wakisema jambo la msingi kwao ni moja tu, yaani maji.
Muda
mfupi kelele zilianza watu wakitaka kuuliza mambo waliyoyaita ni ya
msingi, ndipo Mavunde akaamuru wapewe nafasi ya kuuliza kwanza kabla
hajasimama kuwasalimia.
Mmoja wa wauliza maswali alikuwa Daudi
Lusinde, ambaye alieleza namna wakazi wa kijiji hicho wanavyopata adha
kubwa katika kutafuta maji ambayo aliyaita ni kama dhahabu kwao.
Lusinde
alisema wamepata tabu hiyo kwa muda mrefu na bado hawajaona mwanga wa
matumaini zaidi ya kuendelea kuumia huku ndoo ya maji ikifikia bei ya
Sh500.
“Bei ya sukari inapanda kila kukicha, lakini siyo shida
hapa tatizo ni maji, mheshimiwa sisi tunanunua maji kwa gharama kubwa na
ukishindwa kiasi hicho unalazimika kuchangia maji na mifugo sijui kama
tutapona,” alisema Lusinde na kusababisha mkutano kulipuka kwa shangwe.
Uongozi
wa kijiji na chama wilaya ulizuia kelele za vijana waliomtaka mbunge
huyo aende hadi maeneo wanayochota maji akajionee, ikiwamo uchafu wa
maji pamoja na umbali wake.
Akijibu hoja hizo, Mavunde alieleza
kusononeshwa na kuahidi kuanzia leo ataanza kutekeleza ahadi yake hiyo
kabla ya kufanya jambo lolote.
“Kwa kweli maji ni moja ya ahadi
nilizoahidi kwenu, kesho ni Jumapili siyo siku ya kazi, lakini kuanzia
keshokutwa (Jumatatu) nitaleta hapa wataalamu kuanza kuchimba kisima kwa
gharama zangu,” alisema Mavunde.
Huku akiwa amesimama na maji
aliyopewa, alisema yuko tayari kuacha shughuli za Bunge akashirikiane
nao kuhangaikia maji, hadi pale watakapoyapata na kuanza kujenga
matangi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano
huo, Naibu Waziri alisema katika kipindi cha kampeni alifika eneo hilo
na kuahidi kuwapatia maji, lakini muda ulikuwa bado. Hata hivyo,
Serikali ya awamu ya tano ina miezi sita madarakani.
“Hiyo
ilikuwa ni sehemu ya ahadi yangu kwenye kampeni, kwa hiyo matatizo ya
maji hapa nayajua na kweli ni makubwa, ndiyo maana nimeamua kuvuruga
kila ratiba ili niokoe watu hawa kweli wako kwenye mateso,” alisema.
Mhandisi
wa Maji Manispaa ya Dodoma, Simon Sasala alisema kijiji hicho kina
wakazi 7,600 ambao wanahitaji lita 230,000 za maji kwa siku, lakini kuna
kisima kinachotoa lita 89,000 na wakati mwingine hakifanyi kazi.
Sasala
alisema maji hayo hayatoshelezi kwani yapo kwa asilimia 39, hali ambayo
inawapa shida hasa kina mama kutokana na wengi wao kulazimika kufuata
maji ya kutumia umbali mrefu.
No comments:
Post a Comment