Advertisements

Monday, May 2, 2016

RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI DKT. ALI MOHAMED SHEIN AAPISHWA KUWA MJUMBE WA BARAZA LA MAWAZIRI

Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman akimuapisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri ili aweze kushiriki na kutekeleza majukumu yake kwenye Baraza hilo huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia tukio hilo katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein mara baada ya kuapishwa kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman mara baada ya tukio la uapisho. PICHA NA IKULU

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein leo asubuhi tarehe 02 Mei, 2016 ameapishwa kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri ili aweze kushiriki na kutekeleza majukumu yake ndani ya Baraza hilo.

Rais Shein ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma, tukio ambalo limeshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Viongozi wengine walioshuhudia tukio hilo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo mchana ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Mawaziri, uliopo Ofisi ya Rais TAMISEMI Mjini Dodoma.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
02 Mei, 2016

No comments: