Advertisements

Monday, June 20, 2016

CCM Z'BAR YAPIGA MARUFUKU UVAMIZI WA SHAMBA LAKE KILOMBERO.

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimepiga marufuku ujenzi holela na kazi mbali mbali za kudumu zinazofanyika katika shamba la Chama hicho bila ya kujali taratibu za kisheria  lililopo Kirombero katika Wilaya ya Kaskazini “B”  Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kimesema kuna baadhi ya watu wamevamia shamba hilo na kufanya shughuli za ujenzi wa nyumba pamoja na kupanda miti ya kudumu ikiwemo minazi na miembe, na miti mingine ya kudumu  bila ya ridhaa halali ya chama hicho.

Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,  Ndg. Vuai Ali Vuai wakati akikagua eneo na mipaka ya Shamba hilo huko Kilombero alisema CCM haitowavumilia baadhi ya watu waliofanya uvamizi wa kujimilikisha eneo halali la chama hicho bila ya kufuata taratibu za kisheria.

Alisema Shamba hilo ni urithi wa Chama cha Afro- Shiraz party (ASP), ambalo lilinunuliwa na ASP mwaka 1959 kabla ya mapinduzi matukufu ya  Januari 12, mwaka 1964 kwa ajili ya kuwapati waafrika wazalendo maeneo ya kulima na kuishi baada ya kubaguliwa  na kufukuzwa  katika mashamba ya watu wengine kwa itikadi za kisiasa.

Vuai amefafanua kwamba hakuna kiongozi yeyote ndani ya CCM mwenye mamlala ya kugawa mali yoyote ya chama bali chombo chenye mamlaka hayo ni Baraza la Wadhamini la CCM ndio linaloweza kutoa ridhaa baada ya kukaa na kujadiliana na kutoa maamuzi na siyo vinginevyo.
Ameeleza kwamba chama hicho kitaendelea kuruhusu shughuli za kijamii zifanyike katika eneo hilo zikiwemo ujenzi wa nyumba za ibada, skuli na visima vya maji kwa makubaliano na utaratibu maalum unaofaa kisheria lakini siyo kwa shughuli binafsi.

“ Watu siku hizi wamebadilika na matapeli ni wengi  tunaweza kufanya wema wa kuwaruhusu wajenge wachache baadae  na wao wakawakaribisha wengine ama kuuza maeneo hayo jambo linaloweza kuanzisha migogoro ya ardhi hali ambayo CCM haipo tayari kuona kinatokea.

Lakini pia natoa wito kwa watu wote walioanza kujenga na waliokwisha maliza ujenzi lakini hawajahamia katika nyumba zao na wanaopanda miti ya kudumu wote wasitishe zoezi hilo mpaka watakapopewa utaratibu mwingine.”, alisisitiza Vuai na kuongeza kuwa kama kuna mpango wa kubadili matumizi ya eneo hilo lazima chama kikae na kujadili kwa kina kisha kitatoa maamuzi hapo baadae.

Alitoa onyo kwa baadhi ya watu wanaofanya vitendo vya kitapeli kwa kutumia hati bandia kwa nia ya kujimilikisha mali za CCM na jumuiya zake kinyume na sheria na kuwataka kuacha kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai, na pia kwa Mwana CCM ni kosa kubwa la Kimaadili.

Aidha aliwataka viongozi na watendaji  mbali mbali wa Chama hicho nchini,   kuanza utamaduni wa kutembelea na kukagua mali zote zilizokodishwa ama kumilikishwa na taasisi ama watu ili kubaini vitendo vya udanganyifu na kuweka mali hizo katika hali ya usalama.

Alisema kwa busara na hekima za CCM itaweza kuruhusu shughuli ndogo ndogo ziendelee kufanyika katika eneo hilo zikiwemo kilimo cha mpunga, mboga mboga na mazao mengine ya muda mfupi, na kuagia viongozi wa ngazi ya mkoa Kaskazini kwa kushirikiana na viongozi wa chama na serikali katika shehia ya kilombero kuratibu vizuri shughuli zote zinazofanyika katika eneo hilo.

Aliwasihi  watu waliopewa dhamana za kulinda mali za chama kuwa makini na kuepuka kujiingiza katika vitendo vya kitapeli vinavyoweza kuhujumu mali za CCM na umma kwa ujumla.

Kwa upande wao viongozi wa CCM  katika  Shehia hiyo walisema shughuli anazotambua kufanyika katika eneo hilo ni zile za kijamii zikiwemo skuli na misima vya maji safi pamoja na baadhi ya watu wachache waliopewa kuishi katika eneo hilo kwa muda na siyo ujenzi wa nyumba za kudumu.

Viongozi hao walimuahidi  Naibu wa Katibu Mkuu huyo kutekeleza maagizo yote aliyopewa ili kuepusha migogoro ya ardhi inayoweza kutokea katika eneo hilo kwani CCM ni chama cha amani kisichotaka wananchi waishi katika matatizo.

No comments: