Advertisements

Thursday, June 23, 2016

Je, kuwalipa walimu bahshishi na kupeleka Ruzuku ya Uendeshaji moja kwa moja shuleni kunachochea kujifunza kwa watoto?


Utafiti wa Twaweza na COSTECH waonyesha dalili ya matokeo mazuri

24 Juni 2016, Dar es Salaam: Baada ya miaka miwili ya majaribio, Twaweza, kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na shirika la Innovations for Poverty Action (IPA), wameonyesha kuwa kuwalipa walimu bahshishi ya fedha pamoja na kupeleka ruzuku ya uendeshaji moja kwa moja shuleni kunaweza kuboresha matokeo ya ujifunzaji.

Hii ni kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa Mpango ujulikanao kama KiuFunza, utafiti mkubwa na wa aina yake Afrika Mashariki, Matokeo haya yaliwasilishwa kwenye mkutano uliojadili utungaji wa sera za elimu unaozingatia ushahidi wa kisanyansi (evidence-based policy-making in education) uliofanyika Tume ya Sayansi na Teknolojia tarehe 23 na 24 ya mwezi Juni.

Kwa kipindi cha miaka miwili, Twaweza na IPA wamefanya majaribio ya aina 3 katika shule 350 kwenye wilaya 10 za Tanzania:-
  1. Jaribio la kupeleka ruzuku: - Kupeleka TZS 10,000 kwa kila mwanafunzi moja kwa moja shuleni kama ilivyopangwa na serikali badala ya kuzipitisha kwenye mamlaka za wilaya (jaribio hili lilifanyika kabla ya uamuzi wa serikali wa kupeleka fedha hizo yenyewe moja kwa moja kwenye shule).
  2. Malipo kwa Utendaji Bora (bahshishi kwa walimu/motisha ya fedha): – walimu walilipwa bahshishi ya TZS 5,000 na walimu wakuu walilipwa TZS 1,000 kwa kila mwanafunzi aliyefaulu majaribio ya kusoma (Kingereza na Kiswahili) na kuhesabu kwa darasa la 1, 2 na 3.
  3. Jaribio lililounganisha mbinu zote mbili kwa pamoja: utoaji wa bahshishi pamoja na kupeleka ruzuku moja kwa moja shuleni.

Matokeo makuu yaliyopatikana ni:
  • Kupeleka kiwango kamili cha pesa moja kwa moja shuleni na kwa wakati kunaongeza upatikanaji wa nyenzo za kufundishia na kujifunzia kwa muda mwafaka. Hii huchangia uwepo wa mazingira mazuri kwa wanafunzi na walimu na kuwafanya wahudhurie shule. Hata hivyo, jaribio hili halikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na uboreshaji wa matokeo ya ujifunzaji ndani ya miaka miwili ya utekelezwaji wake.
  • Kuwalipa walimu bahshishi kunaonekana kuwa na matokeo chanya katika kuboresha matokeo ya ujifunzaji, japokuwa si kwa kiwango kikubwa.
  • Mbinu mchanganyiko iliyohusisha kupeleka ruzuku moja kwa moja shuleni pamoja na kuwalipa walimu bahshishi kwa pamoja iliyoonyesha matokeo makubwa zaidi katika kusababisha watoto kupata maarifa na stadi katika hesabu na uwezo wa kusoma. Hii inamaanisha kuwa uwepo kwa wakati mmoja, wa nyenzo za kufundishia pamoja na walimu wenye motisha ndiyo vichocheo vikuu vya watoto kujifunza.

Mwaka 2014
  • Kiasi cha shilingi bilioni 1.125 za pesa za ruzuku ziliingizwa moja kwa moja kwenye akaunti za shule.
  • Kiasi cha shilingi milioni 237 zililipwa kwa walimu wakuu na walimu wa masomo kama malipo ya bahashishi. Fedha hii ililipwa kwa Walimu wakuu 157 na walimu wa masomo 969 walioshiriki kwenye jaribio hili.
  • Jumla ya Wanafunzi 42,725 kutoka madarasa ya 1, 2 na 3 walipimwa katika stadi za kusoma na kuhesabu kwenye shule zilizokuwa kwenye mpango wa ‘Malipo kwa Utendaji Bora’ ili kupata kiasi cha bahashishi ambacho walimu wao walichopaswa kulipwa.

Asilimia kubwa ya walimu wakuu (93%) kwenye shule za KiuFunza wanakubali kuwa majaribio yanayotumiwa katika utafiti wa  ‘Malipo kwa Utendaji Bora’ yanafuata mtaala wa kitaifa. Wastani wa ufaulu katika madarasa yote kwenye majaribio ya mwaka 2014 ilikuwa, asilimia 55 (Kiswahili), asilimia 6 (Kingereza) na asilimia 32 (Hisabati).

Kwa upande mwingine, utafiti wa Viashiria vya Utoaji wa Huduma Tanzania (Tanzania Service Delivery Indicators) uliotolewa hivi karibuni unaonyesha kuwa asilimia 47 ya walimu (madarasa yote) hawapo madarasani wakati wa ziara za kushtukiza mashuleni. Mara nyingi walimu hao wapo shuleni lakini wanafanya shughuli zingine. Matokeo yake ni kwamba wanafunzi wanapata asilimia 39 tu ya muda uliopangwa kwa ajili ya kufundishwa.

Kutokana na mafanikio ya awamu ya kwanza ya KiuFunza, Twaweza inaendesha awamu ya pili ya KiuFunza. Katika awamu hii, walimu wanapewa bahshishi kwa kuboresha matokeo ya wanafunzi, na si tu pale mwanafunzi anapofaulu jaribio zima. Hii inawapa fursa walimu kupata kiasi fulani cha bahshishi hata kama wanafunzi wao hawajafikia kiwango kinachotakiwa, lakini wakiwa wameonyesha maendeleo ndani ya kipindi cha mwaka wa masomo.

Twaweza imechagua kujikita kwenye utoaji wa motisha kwa walimu katika awamu ya kwanza na ya pili ya KiuFunza kwasababu ushahidi kutoka tafiti mbalimbali duniani unaonyesha kuwa jitihada za mwalimu zinaweza kuwa na mchango mkubwa kwenye matokeo ya ujifunzaji.

Matokeo haya ya utafiti chini ya KiuFunza yalitolewa katika mkutano ambao uliandaliwa na Twaweza pamoja na COSTECH, ambapo wadau muhimu kutoka sekta ya elimu, ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, walipata maelezo ya kina ya matokeo hayo pamoja na maelezo kuhusu awamu ya pili ya utafiti. Washiriki pia walipata fursa ya kutafakari kwa ujumla kuhusu motisha kwa walimu (nini kinaweza kuwahamasisha walimu kuboresha utendaji wao), uwajibikaji (tunawezaje kuhakikisha walimu wanatekeleza majukumu yao) na ufuatiliaji (tunawezaje kufahamu nini hasa walimu wanafanya/wanachofundisha).

Katika mkutano huo pia ulizinduliwa mpango mpya wa kimataifa utakaotafiti jinsi ya kuboresha mifumo ya elimu (RISE). Twaweza pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni washiriki.

Mshauri mwandamizi wa Twaweza, Kitila Mkumbo, anasema “Twaweza na IPA wameonyesha kuwa kutumia mbinu ya kupeleka pesa moja kwa moja shuleni na kuwapa walimu bahashishi kunaweza kuboresha matokeo ya ujifunzaji. Japokuwa ujifunzaji unachangiwa na mambo mbalimbali magumu, tumeonyesha kupitia utafiti wa kisayansi, mambo hayo mawili kwa pamoja yanaweza kuleta mabadiliko. Kutokana na ahadi zilizotolewa kipindi cha kampeni pamoja na serikali ya awamu ya tano yenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma na maisha ya wananchi wa kawaida, tunaamini utafiti huu utasikika kwenye ngazi za juu. Hatimaye sasa tuna ushahidi thabiti wa kile kinachoweza kufanyika kuhakikisha watoto wanajifunza. Changamoto iliyopo hivi sasa ni namna ya kufanya mpango huu kudumu kwa muda mrefu.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema “Walimu ndiyo chanzo na ukomo wa ujifunzaji. Lakini katika sekta ya umma, kuna mambo muhimu yanayopaswa kufanyika ili kuhakikisha kuwa walimu wanawajibika kwa kizazi kijacho cha watanzania. Tunahitaji ushahidi – wa namna ya kutoa mafunzo bora kwa walimu, jinsi ya kuhakikisha kuwa kila shilingi inayowekezwa kwenye elimu inatumika ipasavyo kuleta matokeo makubwa. Tunahitaji pia kutoa motisha – watumishi wa umma kwa sasa hawazawadiwi kwa utendaji mzuri wala hawaadhibiwi kwa uzembe. Ni lazima tufuatilie kile hasa kinachoendelea; Je, mwalimu alikuwa shuleni leo? Je, daktari alitumia lugha nzuri wakati wa kumhudumia mgonjwa? Haya ni mambo muhimu sana kwa sekta ya umma imara ambayo inaweza kutoa huduma nzuri kwa wananchi wake.”

---- Mwisho ----

No comments: