Advertisements

Wednesday, June 22, 2016

LUKUVI ATOA SIKU 10 KWA WATENDAJI WA WIZARA KUSHUGHULIKIA SUALA LA MAKAZI MAGOMENI.

Jonas Kamaleki, MAELEZO.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe William Lukuvi (Pichani)ametoa siku 10 kwa watendaji wa Wizara yake kumshauri ili aweze kutatua mgogoro wa makazi wa watu wa Kinondoni Quarters.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati Lukuvi na timu ya wataalaam wa Wizara walipokuwa wakisikiliza malalamiko ya wakazi hao katika Wiki ya Utumishi wa Umma.

“Kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kurekebisha yaliyopinda na kutoa suluhu haraka ili kuwafuta wananchi machozi,”alisema Lukuvi na kuongeza kuwa Serikali haitaki kuona haki za wananchi zinacheleweshwa.

Aliongeza kuwa ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapatiwa makazi bora kama ilivyo katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015.

Waziri Lukuvi alisema kuhusu makazi bora, Wizara inafanya mapitio ya Sera ya Makazi ya Mwaka 2010 ili iweze kwenda na wakati na pia kutengeneza Sera ya Nyumba.

Awali, akitoa malalamiko, Mwenyekiti wa Kamati wakazi waliovunjiwa nyumba zao, Bw. George Abel alisema kuwa suala hili limechukua muda mrefu tangu mwaka 2009 hivyo wanamuomba waziri amshauri Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli abatilishe umiliki wa ardhi hiyo na kuukabidhi kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili nyumba zijengwe na wao wako tayari kununua.

“Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeshindwa kujenga kwani tuliahidiwa kuwa mwaka 2011 nyumba zitakuwa zimekamilika na sisi ndio tutakuwa wapangaji na wanunuzi wa kwanza, lakini hadi leo ni miaka mitano nyumba hazijajengwa nasi tunaishi kwa shida,”alisema Abel.

Aidha, Bw. Abel alisema kuwa  wakazi 644 wa Kinondoni Quarters walivunjiwa nyumba zao na Manispaa ya Kinondoni kwa madai kuwa ni nyumba chakavu na zitajengwa nyumba za kisasa ambazo watapangishwa na hatimaye kuuziwa jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.

No comments: