Tuesday, June 7, 2016

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Simu ya mdomo: 255 22 2460 735/2460 706-8
FAKSI:  255 22 2460 735/700                S.L.P. 3056
Simu pepe: met@meteo.go.tz DAR ES SALAAM
Tovuti:  www.meteo.go.tz

Unapojibu tafadhali nakili:
Ref. No.: TMA/1622            07 Juni, 2016


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MWELEKEO WA HALI YA JOTO NA MVUA KATIKA KIPINDI CHA  JUNI HADI AGOSTI 2016
Taarifa hii inatoa mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa, joto na mvua katika kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti (JJA) 2016.

1. MIFUMO YA HALI YA HEWA

Mifumo ya hali ya hewa inaonesha uwezekano wa kupungua kwa joto la bahari katika eneo la ukanda wa Tropiki la bahari ya Pasifiki wakati lile la ukanda wa magharibi wa bahari ya Hindi linatarajiwa kuwa la wastani kwa kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti 2016. Aidha joto katika bahari ya Atlantiki linatarajiwa kuwa chini ya wastani. Hali hiyo inatarajiwa kusababisha upepo kuvuma kutoka magharibi ukielekea mashariki katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria. Joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika eneo la ncha ya kusini ya bara la Afrika hivyo kuathiri msukumo wa upepo wa kusi katika kipindi cha miezi ya  Juni hadi Agosti 2016. Hali hii inatarajiwa kusababisha hali ya baridi kiasi katika kipindi hicho. Aidha, vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache ya ukanda wa Ziwa Viktoria na ukanda wa pwani ya Kaskazini hususan visiwa vya Unguja na Pemba.


2: VIWANGO VYA CHINI VYA JOTO NA MVUA: JUNI HADI AGOSTI, 2016


2.1 MATARAJIO YA VIWANGO VYA CHINI VYA JOTO KWA MIEZI YA JUNI HADI    AGOSTI 2016
Katika kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti 2016, maeneo mengi ya nchi yanarajiwa kuwa makavu na yenye hali ya baridi kiasi katika majira haya ya kipupwe. Mifumo ya hali ya hewa inaonesha matarajio ya hali ya joto la wastani hadi chini ya wastani katika maeneo yaliyopo Kusini-magharibi mwa nchi. Maeneo mengine yaliyobaki yanatarajiwa kuwa na joto la wastani hadi juu ya wastani katika kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti 2016. Aidha, izingatiwe kuwa hali ya ubaridi inatarajiwa zaidi nyakati za usiku hadi mapema asubuhi. Matarajio ya viwango vya chini vya joto katika kipindi hicho ni kama ifuatavyo:
Kanda ya ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Chato, Kagera, Shinyanga na Simiyu)
Hali ya joto inatarajiwa kuwa ya wastani (Kati ya nyuzi joto 13.0 0C na 15.8 0C) katika maeneo mengi. Matukio ya Vipindi vya upepo mkali katika Ziwa yanatarajiwa kujitokeza.

Kanda ya pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, maeneo ya kaskazini ya mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba)
Hali ya joto inatarajiwa kuwa juu ya wastani(Juu ya nyuzi joto 22.9 0C) katika maeneo mengi. Hata hivyo, katika maeneo ya miinuko ya mkoa wa Tanga hali ya joto inatarajiwa kuwa ya wastani. Matukio ya Vipindi vya upepo mkali yanatarajiwa katika kipindi cha msimu huu.

Kanda ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara)
Hali ya joto inatarajiwa kuwa ya wastani(Kati ya nyuzi joto 13.0 0C na 15.8 0C)  katika maeneo mengi. Hata hivyo, katika maeneo ya miinuko viwango vya joto vinatarajiwa kuwa chini ya wastani (Chini ya nyuzi joto 13.0 0C).


Kanda ya magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi)
Hali ya joto inatarajiwa kuwa ya wastani(Kati ya nyuzi joto 14.9 0C na17.0 0C) katika maeneo mengi.
Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma)
Hali ya  joto inatarajiwa kuwa ya wastani (Kati ya nyuzi joto14.1 0C na 14.7 0C ) katika maeneo mengi Hata hivyo, vipindi vya upepo mkali vinatajiwa katika maeneo hayo.
Kanda ya pwani ya kusini  (Mikoa ya Mtwara na Lindi)
Hali ya  joto inatarajiwa kuwa ya wastani (Kati ya nyuzi joto 13.0 0C na 15.8 0C) katika maeneo mengi.
Kanda ya kusini  (Mkoa wa Ruvuma)
Hali ya  joto inatarajiwa kuwa wastani (Kati ya nyuzi joto 13.0 0C na 15.8 0C) katika maeneo mengi.
Kanda ya nyanda za juu kusini-magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini ya mkoa wa Morogoro)
Hali ya joto inatarajiwa kuwa ya baridi ambapo viwango vya joto vinatarajiwa kuwa  (chini ya nyuzi joto 12.00 C). Hata hivyo, katika maeneo ya kaskazini ya mkoa wa Iringa hali ya joto inatarajiwa kuwa ya wastani.
    1. MWELEKEO WA MVUA KWA KIPINDI CHA JUNI HADI AGOSTI 2016

Kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti kwa kawaida huwa ni kikavu kwa ujumla, hata hivyo vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache ya ukanda wa ziwa Victoria na pwani ya kaskazini.  Hivyo matarajio yake ni kama ifuatavyo:

Kanda ya ziwa Victoria (Mikoa ya Mara na Kagera)
Kwa ujumla maeneo haya yanatarajiwa kuwa makavu. Hata hivyo, vipindi vichache vya mvua vinatarajiwa hususani miezi ya Julai na Agosti 2016.

Kanda ya pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, maeneo ya kaskazini ya mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba)
Kwa ujumla maeneo haya yanatarajiwa kuwa makavu. Hata hivyo, vipindi vichache vya mvua vinatarajiwa, hususani katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Kanda ya nyanda za juu kaskazini-mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara)
Kwa ujumla maeneo haya yanatarajiwa kuwa makavu.

3: ATHARI NA USHAURI
Katika kipindi hicho hali ya hewa inatarajiwa kuwa ya joto la wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi. Hata hivyo, hali ya hewa ya joto la chini ya wastani inatarajiwa katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini-magharibi. Hivyo, kwa shughuli zinazotegemea hali ya joto wadau wanashauriwa kuchukua hatua stahiki ili kukabiliana na madhara yanayoweza kutokea kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa.

Vilevile, kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa katika kipindi hiki, hali ya upatikanaji wa malisho ya mifugo inatarajiwa kupungua na hivyo wafugaji wanashauriwa kuchukua hatua stahiki ili kukabiliana na madhara yatokanayo na uhaba wa malisho.
Pamoja na utabiri huu wa muda mrefu, ni muhimu pia watumiaji wakazingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa kwa vipindi vifupi.

Mamlaka inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa waendelee kutafuta, kupata  na kufuata ushauri wa wataalamu  katika sekta husika.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejeo kila inapobidi.

Dkt. Ladislaus B. Chang’a
KAIMU MKURUGENZI MKUU

No comments: