Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema ndani ya
chama hicho tawala kuna majipu mengi yanayohitaji kutumbuliwa.
Kwa
mujibu wa katibu huyo wa uenezi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama
mkoani Lindi, hatua hiyo ndiyo njia pekee ya kuleta mapinduzi na mageuzi
ndani ya chama hicho.
Amesema chama hicho kilishaingiliwa na
makolokolo, hivyo yanahitaji kusafishwa yote kwa mustakabali wake.
Kauli
ya Nape ni sawa na ile iliyowahi kutolewa na viongozi wakuu wa nchi.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mwanzoni mwa mwaka huu akiwa mkoani
Tanga alisema ndani ya CCM kuna watu majipu ambao wameficha makucha ili
wasijulikane uovu wao.
Siku ambayo Rais John Magufuli alipewa cheti na
Tume ya Uchaguzi (NEC) baada ya kushinda uchaguzi alikwenda kwenye ofisi
ndogo za CCM Lumumba na kuhutubia huku akisisitiza kuwa ndani ya chama
hicho kuna watu wanafiki.
Nape anasema pamoja na kutumbua majipu,
chama hicho pia kinahitaji kujitathimini muundo wake kwa kuwa uliopo
sasa ni mkubwa na hauendani na hali halisi ya kipato cha chama.
“Muundo
wetu ni mzigo mzito unaongeza urasimu. Kwa mfano wajumbe wa NEC hivi
sasa wapo zaidi ya 400 ni mzigo mkubwa kwa chama matokeo yake walitumia
fursa kutafuta ubunge, inahitaji marekebisho makubwa kwa kuwa uchumi wa
chama ni mdogo kwa sasa, tunategemea ruzuku tu. "- Nape
Alisema hata katika
upande wa watumishi wa chama wapo wengi sana na wote si wanasiasa, robo
tu ndiyo wanasiasa.
Kwa mujibu wa Nape, kwa sasa kinachohitajika ni
kutengeneza chama kidogo ili gharama ya kuendesha iwe ndogo.
Alisema
sababu nyingine ya kusafisha chama kutokana na urasimu uliopo; “Lazima
tupunguze mlolongo wa vikao vya kutoa maamuzi lakini pia tuangalie upya
sera na taratibu zetu.”
Akizungumzia watu wenye
tabia ya kuhama vyama kama ilivyotokea kwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward
Lowassa na kundi lake, Nape alisema yeye si muumini wa hilo.
“Mimi
siamini katika kuhama vyama ni sawa na
kumsilimisha Papa. Kwangu kuchukua watu kutoka upinzani ni sawa na gari
zima kuwekewa vifaa chakavu. Watanzania waliopo katika vyama vya siasa
hawazidi milioni 10 kwa nini tunyang’anyane wakati kuna zaidi ya watu
milioni 45."- Nape
Akizungumzia utendaji wa Rais John
Magufuli, Katibu huyo wa uenezi wa chama hicho anayetarajia kustaafu
hivi karibuni katika mkutano mkuu alisema ameanza vizuri na kwamba
mtindo wake wa kutumbua majipu ndiyo hasa ulikuwa ufanyike baada ya
wananchi kukosa imani na Serikali kwa muda mrefu.
“Yanayotekelezwa hivi
sasa na Rais Magufuli ni ripoti yetu. Baada ya kuzunguka nchi nzima
tuligundua mambo mengi na ili kukiweka salama chama hatuna budi
kuhakikisha tunasafisha uozo wote.
“Ilifika wakati wawekezaji wamechukua ardhi hawaitumii, wananchi hawana ardhi tena matokeo yake ni
migogoro kila kukicha, walimu wanadai haki yao watu wenye mamlaka
hawatimizi wajibu wao matokeo yake kukaanza kujengeka hisia kwamba
walimu ni wapinzani.
"Hivi mtu anakuwaje mpinzani kama anadai haki yake?
Mlipe kwanza haki yake uone kama ataendelea na malalamiko,” alisisitiza
Nape ambaye aliingia rasmi katika siasa akiwa kijana mdogo wa miaka 20
tu.
Alisema Rais Magufuli amerejesha heshima
kwani nchi ilifika mahali ambapo wezi wa mali ya umma walionekana ndiyo
wajanja na wale ambao walikuwa wana maadili walionekana legelege.
Alisema jamii ilipotea na Taifa lilikuwa likijenga jamii ya ajabu ya
watu mafisadi, wezi na wasioogopa mali ya umma na hawakuwa na wa
kuwazuia kufanya wanavyotaka.
Akizungumzia
mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya chama chake uliofanyika
mkoani Dodoma mwishoni mwa mwaka jana Nape alisema vikao vilikuwa vya
moto sana.
“Wakati mwingine tulikaa katika mkutano mpaka saa tisa usiku
na hata mkitoka hamtazamani usoni kila mmoja anaingia katika gari na
kuondoka, palichemka sana.”
Hata hivyo, Nape alisema anashukuru
Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Jakaya Kikwete kwa kuwa na kifua na
hiyo ndiyo siri ya kufanikisha mchakato huo.
Alisema Kikwete ni mtoto wa
CCM hivyo ilikuwa rahisi kumkata yeyote kwani uzoefu wake ndani ya
chama ulisaidia na kwamba itachukua muda mrefu kupata kiongozi kama yeye
lakini pia hawawezi kupuuza kazi iliyofanywa na Katibu Mkuu wa chama
hicho Abdulrahman Kinana.
“Ukongwe ulituvusha lakini pia wazee
wakarekebisha mambo tukavuka salama, hali ilikuwa mbaya lakini ndiyo
demokrasia,” alisisitiza Nape ambaye ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe,
marehemu Moses Nnauye. CCM itafanya mkutano mkuu Julai 23 mwaka huu.
1 comment:
Tuanze na wewe
Post a Comment