ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 17, 2016

UNAWAFANYIA NINI WAZAZI WAKO KIPINDI HIKI WAKIWA HAI?

Amrani Kaima GPL

Assalam aleikum mpenzi msomaji wangu. Uhali gani wewe uliyepata bahati ya kunisoma tena wiki kupitia ukurasa huu? Ni matumaini yangu kwamba kwa rehema zake Mwenyezi Mungu umzima na unaendelea vyema na mishemishe zako za kimaisha.

Mimi nitakuwa mchoyo wa shukurani kama sitatumia fursa hii kumshukuru Mungu kwa kila ambalo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu. Niseme tu kwamba Mungu ni mwema sana kwangu.

Mpenzi msomaji wangu, najua Waislam wako katika mfungo wa Mwenzi Mtukufu wa Ramadhani na wale wanaofuatilia safu hii watakumbuka niliwahi kuzungumzia suala la kila mmoja kuiheshimu imani ya mwenzake.

Asitokee hata mmoja wa kujiona yeye ni bora zaidi ya mwingine au kwamba yeye ndiye ambaye yuko kwenye mstari ulionyooka. Wote

tuko sawa na sote ni ndugu, tofauti zetu za kiimani, kikabila na kirangi zisitufanye tukafarakana.

Baada ya kusema hayo nirudi sasa kwenye mada yangu ambayo nimedhamiria kukuletea kwa wiki hii. Nawazungumzia wazazi na yale ambayo kila mmoja anapaswa kumfanyia mzazi wake aliyefanya jitihada za kumleta hapa duniani kisha kumlea hadi kufikia hapo alipo sasa.

Kwa nini leo nimeamua kuandika mada hii? Ni kutokana na tukio lililompata rafiki yangu aitwaye Rashidi Salim wa Dar ambaye huko nyuma alikuwa na maisha magumu sana huku mama yake akiishi kwa tabu huko kijijini kwao Mlalo Lushoto.

Mwanzo mwa mwaka huu Mungu akamuwekea mkono wa Baraka, mambo yakaanza kumnyookea lakini wakati anajipanga kwenda kumjengea nyumba mama yake sambamba na kumfanyia mambo mengine ili aishi kwa furaha, yule mama akaugua ghafla na kufariki. (Inna Lillah Wainna Ilaih Rajiuun).

Lilikuwa ni pigo kubwa sana kwa rafiki yangu huyo, alijua thamani ya mzazi wake huyo lakini wakati akijiandaa kumfanya ajisikie kuwa amezaa, Mungu akakatisha ndoto zake.

Wakati rafiki yangu huyo akiumia kwa kushindwa kumpa furaha mama yake akiwa hai, wapo watu ambao hawajui kabisa thamani ya wazazi. Wamezaliwa, wakalelewa hadi wakakua na kuwa na maisha yao lakini leo hii wanajiona wao ndiyo wao, wazazi wao wamewasahau kabisa kana kwamba wamejileta wenyewe kisha wakajikuza wenyewe.

Mimi nadhani ni wakati wako wewe msomaji wangu kujitathmini upya na kuona umewafanyia nini wazazi wako katika kipindi cha uhai wao ili waweze kujivunia uwepo wako.

Maisha yako ya raha mustarehe hayawezi kuwa na maana kama wazazi wako watakuwa wanaishi kimaskini. Kama ulikuwa hujui,

wengi ambao waliwatelekeza wazazi wao baada ya kupata vijisenti leo hii wanaishi maisha ya ajabu sana, si ajabu yamesababishwa na laana za wazazi wao. Unataka hilo likupate ndiyo uanze kujuta?

Usisubiri hilo, kama umejaaliwa kuwa na wazazi wako mpaka leo na Mungu amekujaalia kufanya kazi na kuwa na kipato, hata kama siyo kikubwa sana, wakumbuke wazazi wako.

Kumbuka wakati wewe ‘unawapotezea’ wazazi wako walio hai, wapo ambao wanatamani wazazi wao leo hii wangekuwa hai ili wawafanyie mambo makubwa. Kwa nini? Kwa sababu wanajua umuhimu wao, wanajua bila wao wasingekuwa hivyo walivyo leo! Wewe hulijui hilo?

Mpenzi msomaji wangu, hili si jambo la kutumia nguvu kubwa sana kukufanya uelewe. Kikubwa hapa ni kwamba, tuwakumbuke wazazi wetu, tuhakikishe wanaishi maisha wanayostahili kuishi.

Wafanyie kila unaloweza zuri ili kesho ukiwa umeondoka duniani, wazidi kukuombea. Pia wakitangulia wao, ubaki na amani kwamba hukuwatenga bali ulijitahidi kuwafanya wajivunie uwepo wako.

Ni hayo tu, tukutane tena wiki ijayo.

1 comment:

Anonymous said...

Well written and great advise. Asante and May you be showered with more Blessings.