Advertisements

Wednesday, July 13, 2016

Akili za Muro ni za kijinga, zenye akili kuliko TFF ya Malinzi


MAKALA: SALEH ALLY

Dar es Salaam: GUMZO kubwa kwa takribani wiki moja iliyopita ni kuhusiana na mzozo kati ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania maarufu kama TFF. Mwishoni mwa wiki hiyo ya mzozo, ulihamia kwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro na mwisho akafungiwa kufanya shughuli za soka kwa mwaka mzima.
Ukifuatilia kwenye maoni ya watu wengi kuna msigano wa mawazo, wengine wakiamini Muro acha afungiwe, wengine wakipinga kabisa, kwamba TFF sasa imepitiliza ubabe.

Kamati ya Maadili ya TFF ambayo mwenyekiti, makamu wake na wajumbe waliteuliwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi Ndiyo walioamua adhabu hiyo ya Muro bila ya yeye kujitetea. Walimwita awali, akafi ka pale na kueleza mapungufu ndani ya barua ya wito ambayo iliandikwa ilimradi na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine.

Ikaonekana kweli ni barua ya hovyo, ikaandikwa nyingine kipindi cha sikukuu, Muro hakuwepo na mwisho alitoa maelezo kwamba alikuwa kwao mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya sikukuu.

TFF inamfungia Muro mwaka mmoja ikiwa ni baada ya mwaka mmoja kumfungia Dk Damas Ndumbaro kwa ujanjaujanja wa namna hiyo, maana aliitwa wakati akiwa safarini Ujerumani, akafungiwa bila ya kujitetea!

Dk Ndumbaro alifungiwa wakati akizitetea klabu zipate haki yao. Hakuna klabu iliyompigania baadaye, lakini ukweli alionekana ni ‘tatizo’ kwa uongozi wa TFF kwa kuwa alianza kusikilizwa sana, alionekana mtenda haki na inawezekana hoja zake zilianza kuuelemea upande wa pili ambao unajua mambo yake mengi si sahihi.

TFF inajijua kwamba kiutendaji sasa ni dhaifu, inajua imeandamwa na kashfa kibao ikiwemo ile ya suala la upangaji matokeo, tuhuma ambayo inaonekana kuzungushwa bila ya majibu bila sababu za msingi.

Hakuna anayeifungia TFF kwa madudu kibao na inaendelea kufanya mengine. Tokea amefungiwa Muro, siku nne zilizopita hadi jana mchana hata ile hukumu haikuwa imetoka kwa maandishi na hii ilitokana na Muro kuonekana mjanja, mwelewa na anajua wapi wameboronga.

Kumekuwa na taarifa kwamba inarekebishwa ili kuendana na hoja za Muro ambazo aliziibua mara tu baada ya kufungiwa. Lakini usisahau, TFF imemfungia Muro bila ya kumhoji lakini kitu kibaya zaidi, hoja zilizoonekana kwao ni ‘matusi’ hawakuwahi kuzijibu.

Pamoja na mengi, lakini yale ya Muro kusema hawawezi kuilipa TFF kwa kuwa hawakuingiza kipato, wala hawana sababu ya kulipa kodi kwa kuwa hakuna kilichoingia imeonekana ni kashfa lakini TFF ilishindwa kujua hilo, ikapeleka barua ndefu yenye uchanganuzi ikitaka nayo ilipwe. Hii ishu ilikuwa ni ule uamuzi wa Yanga kuamua mashabiki wake waingie bure katika mechi dhidi ya TP Mazembe. Kitu kibaya zaidi, TFF ilionekana kutojua mengi yakiwemo ya kutaka Mamlaka ya Mapato (TRA) nayo ilipwe, lakini yenyewe ikatoa tamko kwamba hakuna wanachotakiwa kulipwa kutoka Yanga.

Kingine cha kushangaza kinachoonekana TFF ni yenye visasi ni hiki; imemfungia Muro haraka sana wakati inaonyesha wazi ina hasira na imechukizwa na kutopata kitu cha mgawo kwa kuwa mashabiki waliingia bure.

Dk Ndumbaro alifungiwa katika hali hiyohiyo na kinachoshangaza zaidi ni kuona mashabiki wanalichukulia suala hilo kishabiki! Kwa kifupi, kama unamuona Muro hana akili lakini TFF haitaki kuona wanaoizidi akili au hoja. Na huwezi kupinga kwamba wahusika hasa kamati, nao hawatendi haki huenda pia kuna haja ya kuangalia au kubadili katiba, wanakamti wasiteuliwe na Rais wa TFF ili kuepuka ‘kutekeleza jambo la bwana’.

Nilihoji hivi; kesi ya Donald Ngoma kumpiga kiwiko Hassan Kessy akiwa Simba, hadi leo haikuwahi hata kufanyiwa kazi. Lakini kwa kuwa Muro aliikosoa TFF na kuitoa jasho huku akionekana anawazidi maarifa kwa hoja, wamemfungia kwa kutafuta ‘vikosa’ ilimradi ili kutimiza lengo.

Mnaoshangilia leo, mnaipa TFF nguvu ya kumfungia kila inayeona amekuwa kigezo au kigingi kwao kwa kuwa mambo yao mengi yanaonekana hayana ‘akili’ sahihi iliyolenga kuleta maendeleo.

Nani anaweza kusimama hadharani akainua mkono na kusema TFF chini ya Jamal Malinzi, imeleta mabadiliko ukilinganisha na ile la Leodegar Tenga?

Lakini ukiuliza wangapi wanaona TFF ya Malinzi imeturudisha nyuma na afadhali ile ya Tenga, rundo la mashabiki wapenda soka watajitokeza kuinua vidole na kusema ni kweli.

Itakuwa jambo jema kuangalia hoja za msingi katika ufungiwaji wa Muro. Sina haja ya kumtetea, tena naona kama hukumu hiyo inatumia vigezo vya zamani. Wote tunajua Muro naye amekuwa akiboronga mara kibao kwa kuzungumza kwa jazba au maneno ya mbwembwe bila hata sababu ya kufanya hivyo.

Achana na hayo ya awali, maana hawakuwahi kumshitaki. Katika hili la bure, kipi hasa kilikuwa kibaya? Kusema watu watakaa juu ya paa, ndiyo kosa la kumfungia mtu mwaka mzima? Kumbukeni, mzigo wa Muro wa Yanga, kesho utahamia kwa nanihii wa Simba, Mtibwa Sugar au Stand United.
 Maigizo matupu!
CREDIT:SALEH ALLY

1 comment:

Anonymous said...

Kwa kweli wakati huu Tanzania ipo katika kipindi muhimu sana katika historia ya nchi yetu yaani ni yale mageuzi makubwa iliyokuja nayo serikali ya Magufuli ya kuwataka watanzania hasa watumishi wa umma kuacha kufanya kazi kwa mazoea, yaani yale mazoea ya kizembe, kwa kwetu kufikiri ndio ujanja kama vile rushwa,ufisadi, uvivu, ubinafsi,ukabila,undugu bila ya kujali sifa stahiki ya mhusika katika nafasi fulani ya kazi nakadhalika nakadhalika . Ama ukija katika taasisi moja nyeti sana tena sana lakini kutokana na kwamba bado watanzania wengi tunaendelea kuishi katika zama za uzembe tunakichukulia chama mpira wa miguu kama taasisi isio na maana hili ni kosa kubwa sana linaloendelea nchini na tunaiomba serikali ya Magufuli kama ipo serious kuliletea taifa maendeleo na heshima kwa wote basi sekta ya michezo mimi naiita sekta ya vijana lazima itizamwe kwa jicho la tatu hasa mchezo wa mpira wa miguu. Hakuna haja ya mimi kupoteza muda kueleza umuhimu wa mchezo huu na muunganiko wake katika kuzitangaza sekta nyengine za biashara kama utalii na kadhalika. Leo hii duniani kokote ukitaja Ivory coast licha ya nchi hii kutawaliwa na vurugu za wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu, vurugu hizo zimeshindwa kuitanangaza nchi hiyo kama nchi ya majanga badala yake soccer ni kitambulisho na kivutio kikubwa kinachiitangaza nchi hiyo. Sisi licha yakuwa na amani mwanana mtu ukimtajia Tanzania anakushangaa sana ni nchi gani hiyo hata baadhi ya waafrica wanashindwa kuifahamu lakini njia moja rahisi na smart ya kuitangaza nchi yetu na kuwapatia vijana wengi ajira za maana tumeipa mgongo na badala yake tunawaachia watu wa hovyo kuingoza taasisi muhimu kama TFF. Inawezekana rahisi huo kachaguliwa kwa kura lakini nnaimani kabisa ufisadi lazima ulitumika katika uchaguzi huo kwani hata Sep Platter aliekuwa raisi wa fifa alichaguliwa kwa kura na sasa hivi yuko wapi? Malinzi na TFF yake bado wanaishi zama za akina Sep platter kwa hivyo haja ya kutumbuliwa ipo sana tena haraka. Malinzi anamawazo yanayomlevya yakwamba TFF hawezi kuguswa na serikali na ataendelea kufanya manyago yake apendavyo kwa kutegemea mgongo wa FIFA lakini akumbuke hata raisi aliekuwa wa shirikisho la mpira duniani Sep Platter alikuwa na mawazo hayo ya kijinga na mwisho wa siku kaishia ujingani. Kwa manufaa ya Taifa lazima yafanyike madaliko makubwa katika shirikisho la mpira wa miguu Tanzania la sivyo kila siku zikienda mbele tena kwa kasi basi na sisi tunazidi kurudi nyuma tena kwa kasi vile vile. Hata CCM ilijivua gamba na kama vile haitoshi waliamua kumuengua rubani aliekuwa akiongoza safari ya matumaini angani licha ya misuko suko iliotokea lakini hakuna anaeibisha yakwamba ndege yao ilitua salama na rubani mpya aliepa CCM mafanikio ya haraka, makubwa na ya ajabu kabisa hadi kufikia Africa na dunia kote wanaizungumza Tanzania.Sasa ikiwa imewezekana kwa CCM na Tanzania kwanini ishindikane kwa taasisi nyengine? Kwa nini wadau soccer tushindwe kuibadilisha TFF kwa manufaa ya taifa letu? Watanzania wote tumeshajiridhisha yakwamba Jamali Malinzi hafai kuiongoza taasisi hiyo muhimu nchini sasa tunachosubiri kitu gani kwanini kusiwe na maamuzi magumu na ya maana kuokoa mpira wetu? Huu ni wakati wa mabadiliko ya maendeleo Tanzania na TFF ni moja kati ya jibu tena la utosini kama sio sehemu ya siri kuliachia kuendelea kukuwa ni kukisogelea kifo.