Advertisements

Monday, July 25, 2016

Akutwa na hatia ya kumuua Mwangosi bila kukusudia

By Hakimu Mwafongo na Geofrey Nyang'oro, Mwananchi

Iringa. Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imemtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia askari wa kikosi cha kuzuia ghasia, Picificus Simon anayetuhumiwa kumuua mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi huko Nyororo wilayani Mufindi.

Akisoma mwenendo wa kesi, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Dk Paul Kihwelo amesema leo kuwa mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa kufuatia ushahidi alioutoa kwa mlinzi wa amani.

Jaji Kihwelo amesema mbele ya mlinzi wa amani mtuhumiwa alikiri kosa hilo akisema alitenda bila kudhamiria.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Adolf Maganga ameitaka mahakama hiyo kumpa adhabu ya kifungo cha maisha wakati Wakili wa Utetezi, Rwezaula Kaijage aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu ikiwa ni pamoja na kumuachia huru kutokana na majukumu aliyonayo.

Hukumu ya kesi hiyo itatolewa Julai 27.

No comments: