ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 28, 2016

ASKARI ALIYEMUUA MWANAHABARI DAUDI MWANGOSI AFUNGWA JELA MIAKA 15

Ndugu  wa Marehemu  Daudi  Mwangosi  mama Mfugale  kushoto  akitoka mahakama  kuu kanda  ya  Iringa akiwa na furaha baada ya  hukumu ya  kesi  hiyo  kutolewa leo kwa askari  aliyeuwa  kufungwa  jela miaka 15 Picha zote na MatukiodaimaBlog
Mjane  wa marehemu Daudi  Mwangosi Itika Mwangosi mwenye  kilemba cheusi  akiwa katika  foleni ya ukaguzi  wa polisi ili   kuingia mahakama kuu kanda  ya  Iringa 
Mjane  wa marehemu Daudi  Mwangosi Itika Mwangosi mwenye  kilemba cheusi  akiwa katika  foleni ya ukaguzi  wa polisi
Mjane  wa marehemu Daudi  Mwangosi Itika Mwangosi mwenye  kilemba cheusi  akifurahi jambo na ndugu  yake  mzee Marko Mfugale mahakamani  hapo  
Mdogo na marehemu Mwangosi Bw Mecky Mwangosi kulia akisalimiana na Rais wa UTPC Deo Nsokolo kabla ya mahakama kuanza 
Rais  wa umoja  wa klabu  za waandishi wa habari Tanzania Bw  Deo Nsokolo  akizungumza na wanahabari  baada ya hukumu ya kesi ya mauwaji  ya  Mwangosi
Wanahabari  mkoa wa Iringa  wakimsikiliza Bw Nsokolo 
Wanahabari  wakiwa nje ya viwanja  vya mahakama baada ya  kesi  kumalizika
Mjane  wa Mwangosi Itika  Mwangosi  mwenye  kilemba  akitoka mahakamani hapo huku akiwa na uso wa furaha  baada ya  hukumu  kutolewa kwa  muuaji kufungwa miaka 15  jela
Mjane  wa Mwangosi  akiwa katika  viwanja  vya mahakama  kuu kanda  ya Iringa
Mjane  wa marehemu Daudi Mwangosi  akizungumza na  wanahabari ikiwa ni  pamoja na  kuwashukuru kwa  umoja  wao
Rais  wa UTPC Deo  Nsokolo akiwa na mtaalam wa IT Lukelo Mwaipopo nje ya mahakama kuu kanda  ya Iringa 


Na MatukiodaimaBlog , Iringa
  MAHAKAMA   kuu  kanda  ya  Tanzania kanda  ya Iringa   imemhukumu   kwenda  jela  miaka 15 askari   Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia ( FFU )Iringa   namba G 58 Pacificius Cleophace Simon (27)  kwa   kosa la  kumuua bila   kukusudia   mwaahabari  Daudi  Mwangosi   mwaka 2012 katika  kijiji  cha  Nyololo  wilaya ya  Mufindi. wakati akiwa  katika  majukumu  yake ya  kuchukua  habari huku mke  wa marehemu Mwangosi Itika Mwangosi  akipongeza  vyombo  vya habari nchini  kwa  ushirikiano mkubwa katika kufuatilia kesi  hiyo.  .

"Mahakama   inatambua  uchungu  wa familia iliyoupata  kwa kifo  cha marehemu  Daudi Mwangosi ambaye aliuwawa  pia  marehemu  aliuwawa  kikatili ....siku  zote  adhabu  inapaswa   kulingana na kosa   husika mahakama  haiafiki maombi  ya  wakili  wa upande  wa  utetezi  kuomba  mshtakiwa apewe  adhabu ya kuachiwa   huru  kwa kuwa ni  yatima  ....mgongano  wa hisia umeonekana katika  kesi   hii ila mahakama  inampa adhabu ya  kwenda  jela  miaka 15" alisema jaji  Dkt  Paul Kiwelo

Akisoma   shauri   ya  kesi   hiyo  kabla ya  kutoa  adhabu    mahakamani  hapo jaji Dkt Kiwelo  aliwashukuru wazee  wa baraza  la mahakama   kwa  michango yao  mkubwa  mchango  ulioisaidia  mahakama hadi   kufikia  siku   hiyo  ya  hukumu pia  mawakili   wote walioshiriki katika  kesi  hiyo.

" Suala  la aina  gani  ya adhabu inafaa halikuwa  rahisi  sana  kwani  shauri  hili  upande  wa  jamhuri  uliomba  adhabu  ya  kufungwa  maisha  jela  huku upande wa  utetezi  ukiomba mshitakiwa aachiwe   huru kwa masharti  ambayo  mahakama  ingeona  yanafaa  kutokana na  kuwa na majukumu ya  kulea  wadogo  zake  na yeye kuwa yatima .....mahakama  imetazama  ukubwa  wa   kosa husika  pia  jamii ina mtazamo  gani katika  kesi hiyo lakini  mahakama  haitoi  hukumu kwa  mitazamo mbali mbali  inatumia  vifungu  vya  sheria suala la  kutoa  adhabu  ni la  kisheria  si  vinginevyo"

Jaji  Dkt  Kiwelo  alisema  kuwa  adhabu haitolewi  kwa  ajili ya  kulipiza   kisasi  ila  inatolewa  kama   sehemu  ya  onyo  na  kuifanya  jamii  kutambua  kuishi  kwa  kuheshimu misingi  ya  sheria  kwani   kuna mambo  manne  katika  kesi  yanatazamwa likiwemo  la medhania  ya  kosa alilotenda  na  aina  ya  kosa pia  maslahi  ya  jamii  katika  kosa  husika.

"Naomba  kusema mgongano  wa  hisia  umeonekana katika kesi  hii pamoja na kuwepo kwa  changamoto  hizo  bado mahakama haijayumbishwa na migogano   hiyo .....mahakama haiitoi hukumu kwa  kutazama  ni  kosa la kwanza wala mhusika hana rekodi  mbaya  ya makosa  mahakama  inaendeshwa  kwa sheria ndugu  wangefurahi  kuona mtuhumiwa anafungwa  hivyo  siafiki  maombi  ya  upande wa  utetezi  juu ya  mkosaji  naamini kabisa  kwa kosa   hili kumwachia kwa Masharti  haki haitakuwa  imetendeka"

Kwa  mujibu  wa  sheria kuua bila  kukusudia  ni  kosa  kubwa sana  ambapo  adhabu  yake   huwa ni kufungwa  jela  maisha japo  kila  kosa  huamuliwa  kutokana na mazingira yake  hivyo lazima upewe  adhabu ambayo  itakuwa funzo  kwa   wengine.

" Kuua si  jambo  dogo na  mahakama  hii kwa  kuzingata vifungu vya  sheria  na  pia mtuhumiwa  umekaa mahabusu  miaka minne  inakuhukumu  kwenda  jela  miaka 15 rufaa ipo  wazi kwa  asiyeridhika"



Akizungumza na  wanahabari  mara  baada ya  hukumu   hiyo  aliyekuwa  wakili  wa  utetezi Lwezaula Kaijage alisema  kuwa alisema  kuwa  yeye  alikuwa  ni  wakili  wake na  kuwa kwa  sasa hawezi  kusema  ni uamuzi  gani  ambao mteja  wake anaweza  kuchukua hadi hapo atakapowasiliana  nae

" Nafikiri   wote  mlikuwepo mahakamani  mmesikia  kuwa amefungwa  miaka 15  itabidi  sasa  mimi niende magereza  kuzungumza nae ili  nichukue sheria nione  zinasemaje  pia  kuomba mwenendo  mzima  wa  sheria  kuona jinsi  ulivyokwenda  ili  nione  ni  kitu  gani  ambacho  labda  mahakama  ilielekezwa  vibaya kabla ya  kutoa hukumu  hiyo kama  nitaona  kuna  jipya  basi  tutakwenda kwenye  rufaa"


Wakili wa  mtandao  wa  watetezi wa haki  za  binadamu ((THRDC)Benedict  Ishabakaki  alisema  kuwa katika  hukumu   hiyo mahakama  kuu kanda ya  Tanzania kanda ya Iringa imetenda  haki pasipo kuegemea  upande  wowote  na  kuwa pamoja na nguvu  kubwa ya polisi na jinsi ambavyo  ushahidi  uliokuwa  umepelekwa  kulenga  kumnasua mwenzao  ila mahakama hiyo imetumia ushahidi  wa ungamo la mlinzi  wa amani kutoa   hukumu ambayo kimsingi haijaacha maswali kwa wananchi .

Wakili Shabakaki  alisema  kuwa kesi   hiyo  polisi  waliifanya kama kesi  ya nyani  kumhukumu ngedele  kwa  kula mahindi   kwani  alisema aliyetenda  kosa alikuwa ni askari ,mchunguzaji  wa  kesi  hiyo  ni  askari hivyo katika mazingira  hayo haikuwa rahisi  kesi  hiyo kufikia hukumu   hiyo  ila mahakama imetenda haki na  kuwa  wao kama  watetezi  wa haki  za  binadamu  wataona  ni hatua  zipi  za  kuchukua baada ya mahakama  kutenda haki .

Alisema  pamoja na jukumu la  polisi la ulinzi  wa jamii ila polisi baadhi  yao  wameendelea  kukiuka  wajibu  wao na kuogopwa zaidi na raia   jambo  ambalo si  jema  na  kuwa nguvu  kubwa iliyotumika siku  zote  wakati wa  kesi  hiyo ni  kielelezo  tosha  kuwa polisi walikuwa wakitegemea  mwisho wa  siku  mwenzao  huyo  kuachiwa  huru .



Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo alisema kuwa  wao kama UTPC  wanapongeza mahakama  kuu ya Tanzania kanda ya Iringa  kwa  kutenda  haki katika kesi  hiyo kwani  alisema  kuwa jeshi  la  polisi  walipanda  kuharibu  kesi  hiyo ila jaji kwa umakini  wake  ametoa  adhabu

" Sisi  kama  wanahabari tunajipongeza pia kwa hukumu  hii kwanza  kutiwa hatiani kwa  mtuhumiwa na pili  kufungwa  jela  miaka 15....... na  ifahamike  kuwa  kesi   hiyo  ilikuwa ikiihusu  serikali hivyo  hukumu ya  kesi  hiyo  imeingia katika rekodi ya dunia  kuwa  mwandishi  aliuwawa na muuaji  amefungwa  miaka 15  jeshi  la polisi  Iringa  kwa muda  wote  limekuwa likiwanyanyasa  waandishi  hivyo  sisi kama  viongozi  wa wanahabari  tutakwenda  kuonana na viongozi  wao wa juu"

Alisema  kuwa yapo mambo ya msingi ambayo  jeshi la  polisi  linapaswa  kufanya  ila si kwa kutumia nguvu  kubwa  kunyima uhuru  wa  vyombo  vya habari hasa katika  kesi  hiyo  ya Mwangosi .

" Polisi katika  kesi  nyingine   wamekuwa  wakiwasaidia  wanahabari  kupata picha  kirahisi  kwa  watuhumiwa  pindi  wanapofikishwa mahakamani  ila katika  kesi  hiyo  wamekuwa  wakimfunika mwenzao na kuzuia  waandishi  kupiga picha ila pamoja na yote  hayo adhabu imetolewa pale  pale"

Makamu Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile   alisema  kuwa  polisi  Iringa  walitamani kuona  kesi   hiyo  inaharibika na kama  lisingelikuwa  ungamo la mlinzi  wa amani mtuhumiwa  huyo  alikuwa anaachiwa  huru na  ungamo  chini ya mlinzi  wa amani  ni mahakama  yenyewe  hivyo ni wazi mahakama  imeweza  kutenda haki zaidi .


" Adhabu  ni  kumfanya  mtu ajirekebisha  na  wapo waliotegemea  kuwa muuaji wa Mwangosi nae ana hukumiwa  kufa   ila  si haki binadamu  ....lakini mtuhumiwa huyo   wakati  wote wa  kesi  hiyo hakupaswa  kufikishwa mahakamani  na polisi wenzake  badala ya askari wa magareza ambao  ndio  wanawajibu  wa  kumpeleka  mahakamani na mahabusu  ila .....hata leo  baada ya  hukumu hatujui amepelekwa  wapi maana wameondoka nae wao  wenyewe  ambao  walitaka kesi  ivurugike  sasa  sijui  wanampeleka  rumande ama  gerezani au  wamempeleka nyumbani kwanza kula  chakula lakini naomba hili  kuliacha  hapo"

Bw Balile alisema kuwa kwa sasa  wanaanzisha  mchakato  wa  kufungua  kesi  ya madai  kwa  ajili ya familia ya Mwangosi  na  kuwa kujua ni mahakama  ya ndani ama  ya Afrika ambayo  kesi  hiyo itafunguliwa itajulikana baada ya  kwenda  kukaa na  viongozi  wenzake japo  alisema haki yote itafikishwa kwa familia ya Mwangosi

Juzi Julai 25 mahakama  kuu ya Tanzania kanda ya Iringa ilimkuta  na hatia askari Simon  katika  kesi  hiyo namba 45 ya mwaka 2013 ya mauaji ya bila  kukusudia  ya   mwahabari   Mwangosi    aliyeuwawa kinyama  Septemba 2 mwaka 2012 katika  kijiji  cha  Nyololo  wilaya ya  Mufindi  wakati  chama cha Demokrasia  na maendeleo (chadema)  wakifanya uzinduzi wa matawi  huku kukiwa na katazo la matukio  ya  mikutano  ama mikusanyiko ya  kisiasa  kutokana na serikali  kuongeza  muda  wa kuendelea na zoezi la  senza ya  watu na makazi.

Mjane  wa  marehemu  Mwangosi  Bi Itika Daudi  Mwangosi  alitoa  pongezi  nyingi kwa  wanahabari kwa  ushirikiano  wao  wakati  wote  wa kesi  hiyo hadi ilipofikia  mwisho .

" Napenda  kumshukuru  mwenyezi  Mungu  mwingi wa rehema  kwa kutufikisha  salama siku  hii ya  leo .....na  niishukuru mahakama  kuu ya Tanzania kanda ya  Iringa  kwa  kuweza  kutenda haki pili  ninawashukuru  sana ninyi  waandishi  wa habari  kwa  umoja  wenu ...nawashukuru  sana  tena  sana  zaidi  ya  sana hata  kama  mtu  amekutendea  wema  gani  Mungu alitupa  neno  moja  tu la ahsante  pia  napenda  kuwatia  moyo  msiogope  songeni mbele Mungu  yu  paoja  nanyi kama alivyowapigania hadi  kufika  leo atazidi  kuwapigania  zaidi teteeni kazi  zenu  elimisheni  jamii vile  mnavyoendelea  kusaidia  jamii ndivyo  Mungu anavyowabariki daima sina neno la  zaidi zaidi ya ahsante "

Marehemu Daudi Mwangosi  aliuwawa  kinyama Septemba 2 mwaka 2012 katika  kijiji  cha Nyololo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa   wakati wa chama  cha Demokrasia  na maendeleo (Chadema) kilipokuwa  kikifanya  mikutano ya  ufunguzi  wa matawi wakati  kukiwa na zuio  la mikutano  hiyo  kutokana na kuongezwa kwa muda  wa  senza  ya  watu na makazi .





No comments: