Advertisements

Friday, July 8, 2016

KAPALATA MBUNIFU WA GARI ASIYEJUA KUSOMA

Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi akimsikiliza
By Kalunde Jamal, Mwananchi

Ukifika katika banda la Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (Sido) lililopo Viwanja vya Mwalimu Nyerere ambako Maonyesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) yanayomalizika leo, ungevutiwa na vitu vingi, lakini zaidi kwenye gari iliyobuniwa na Kapalata, Mkazi wa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.

Kapalata siyo jina halisi la mbunifu wa gari hilo bali limevuma kutokana na tabia yake kushabihiana mtu mmoja, ambaye ni mkazi wa Mkoa wa Shinyanga aliyejulikana kwa jina hilo.

Jina halisi la Kapalata ni Jackob Luis, lakini kutokana na utundu wake wa kutengeneza na kubuni vitu kama Kapalata, watu waliamua kumpachika jina hilo.

Kapalata alizaliwa mwaka 1978 katika Wilaya ya Mpanda ambayo kwa wakati huo ilikuwa mkoani Rukwa. Rukwa uligawanywa na kuanzishwa mkoa mpya wa Katavi Machi mwaka 2012.

Anasema licha ya kubuni vitu vingi ikiwamo gari hilo, hakuwahi kubahatika kusoma hata darasa moja katika maisha yake kutokana na sababu ambazo hakuzitaja.

Jinsi alivyobuni gari

Kapalata anasema akiwa kijana mdogo kijijini kwao alikuwa akifanya kazi ya kuuza maji katika baadhi ya maeneo ya mji wa Katavi kwa kutumia mkokoteni.

Anasema wakati mwingine ilimlazimu kutengeneza mkokoteni huo mwenyewe kutokana na kuharibika mara kwa mara.

“Mkokoteni ule haukuwa wa kwangu, siku moja niliwaza kwanini nisitengeneze wa kwangu kama naweza kutengeza huu ambao ulikuwa ukinusumbua kwa kuharibika mara kwa mara,” anasema.

Kapalata anasema baada ya kufikia uamuzi huo, alianza kutafuta vifaa kidogo kidogo na kutengeneza mkokoteni wake na kumaliza kazi hiyo kwa muda mfupi. Kwa mujibu wa Kapalata, shauku ya kubuni vitu vingine zaidi iliongeeka ndipo aliamua kutengeneza baiskeli na kutimiza ndoto hiyo baada ya wiki moja. “Hapo ndiyo jina la Kapalata lilipoanza na siku moja watu wa Sido walikuja kijijini kutafuta watu wenye vipaji, wanakijiji walipendekeza jina langu,”anasema.

Anasema aliwaonyesha vitu alivyotengeneza nao wakaonyesha kuridhika navyo na kumuomba ajiunge nao katika Maonyesho ya Viwanda Vidogo yaliyofanyika mkoani Iringa 2004.

Anasema alikwenda mkoani humo kuonyesha baiskeli hiyo ambayo ilikuwa na magurudumu mawili mbele na moja nyuma. “Ilikuwa maarufu katika maonyesho kwa sababu hakuna aliyewahi kubuni aina hiyo ya baiskeli, ilinipatia sifa sana kila mtu alitamani kuiona,” anasema na kuongeza: “Katika maonyesho hayo alikutana na wabunifu waliobobea na kupata fursa ya kujifunza zaidi ubunifu.”

2005 alishiriki maonyesho mengine ya Sido ya Nyanda za Juu Kusini ambako alichaguliwa kama fundi kutoka Rukwa.

Anasema alikwenda kushiriki maonyesho hayo akiwa na baiskeli yake, lakini kutokana na wabunifu kuongezeka ilikuwa haina maana wala jipya.

Anasema ndipo wazo la kuja Dar es Salaam lilimjia kuendeleza ubunifu wake. “Kuna mtu alijitolea kunipa malazi nikifika Dar es Salaam, nikarudi nyumbani na 2006 nikatimiza azma yangu na bahati nzuri nilimkuta mwenyeji wangu amepata tenda ya kutengeneza viti vya walemavu hivyo tulishirikiana kutokana na kupata mafunzo kutoka Sido.

Anasema akiwa Dar es Salaam alipata wazo la kutengeneza mashine ya kutotolea vifaranga na kumlipa kiasi cha Sh450,000 kama faida kwa kila mashine moja.

No comments: