Advertisements

Wednesday, July 20, 2016

MAHAKAMA YATOA HATI YA KUKAMATWA MENEJA WA DIAMOND ‘BABU TALE’

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa hati ya kukamatwa kwa Hamis Tale ‘Babu Tale,’ ambaye ni meneja wa mwanamuziki wa bongo fleva,Diamond Platnumz.

Mahakama imetoa hati hiyo kutokana na Babu Tale kutotii amri ya mahakama iliyomtaka amlipe Shekhe Hamis Mbonde Sh. 250 milioni.

Babu Tale anatakiwa alipe fedha hizo kutokana na kuvunja mkataba kati yake na Shekhe Mbonde, kwa kuuza na kusambaza nakala za mawaidha (DVDs) bila ridhaa ya shekhe huyo, jambo ambalo ni kinyume na haki miliki.

Kutokana na Babu Tale na mwenzake Iddi Tale kushindwa kulipa fedha hizo kama ilivyoamriwa tarehe 18, Februari  mwaka huu, mahakama ilitoa hati ya kukamatwa kwa wadaiwa hao tarehe 8 Julai mwaka huu.

Katika hati hiyo, mahakama ilimuelekeza Kamanda wa Polisi Kanda ya Ilala kuwa, hadi jana tarehe 19 Julai mwaka huu awe amewakamata wadaiwa hao ili wafike mahakamani kueleza kwanini wasipewe adhabu kwa kukiuka amri ya mahakama.

Shauri hilo limetajwa tena jana mbele ya Juma Hassan, Kaimu Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambapo alitoa hati nyingine kumuelekeza Kamanda wa Polisi Kanda ya Kinondoni kuwakamata wadaiwa hao.

Msajili Juma alitoa hati hiyo baada ya Mwesigwa Muhingo, Wakili wa Shekhe Mbonde,  kuomba hati hiyo ipelekwe Kinondoni kwa kuwa Babu Tale anaishi huko na si Wilaya ya Ilala kama hati ya kwanza ilivyoeleza.

Tarehe 18 Februari mwaka huu, Jaji Augustine Shangwa, aliwaamuru wadaiwa kulipa Sh. 200 milioni  kama fidia ya kuvunja haki miliki ya Shekhe Mbonde na Sh. 50 milioni kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na kuvunja makubaliano.

Katika uamuzi wake Jaji Shangwa alisema, Juni 16, 2013, Mbonde aliingia makubaliano na wadaiwa hao na wenzake ya kufanya biashara ya kurekodi mawaidha na kutengeneza nakala DVDs kwa ajili ya kuziuza nchini.

Wadaiwa hao waliahidi kumjengea nyumba, kumnunulia gari na kuitangaza kazi yake pia walimpa Sh milioni mbili na kumnunulia kanzu na kofia (baraghashia) na kurekodi DVDs zenye ujumbe Uzito wa Kifo, Fitina Juu ya Wanawake, Umuhimu wa Swala, Mwanadamu Yumo Ndani ya Hasara na Maadui wa Uislam.

Alisema, makubaliano ya awali yalikuwa kurekodi halafu baadaye wakubaliane kuhusu bei na jinsi ya kuziuza, badala yake waliziuza na kuzisambaza nakala hizo na kujipatia faida bila kumshirikisha Mbonde ambaye alitumia ujuzi wake.

Mbonde kupitia wakili wake Muhingo, Gwamaka Mwaikugile na Clement Kihoko,  alifungua kesi ya madai namba 185/2013 akiiomba mahakama iamuru wadaiwa wamlipe Sh. 700 milioni kama  fidia ya kuvunja makubaliano na Sh. 50 milioni kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na kuvunjwa kwa makubaliano.

No comments: