Advertisements

Monday, July 4, 2016

MAKONDA AWATAKA WAKUU WA WILAYA KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA

 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda (kushoto) akimuapisha Mhe.Sophia Mjema (kulia) kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala leo katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
 Mhe.Sophia Mjema (kulia) akionesha Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (kushoto) mara baada ya kuapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala leo katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.

 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (kushoto) akimuapisha Mhe.Hashim Mgandilwa (kulia) kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni leo katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (kushoto) akimuapisha Mhe.Ally Hapi (kulia) kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni leo katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (kushoto) akimuapisha Mhe.Felix Lyaniva (kulia) kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke leo katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe.Paul Makonda akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wapya wa Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam (mbele) pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam (nyuma)mara baada ya kuisha kwa zoezi la kuapishwa lililofanyika leo nje ya Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam. Picha zote na Jacquiline Mrisho - MAELEZO .

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO 
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda amewataka Wakuu wapya wa Wilaya kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi waliopo katika Wilaya zao ili kudumisha amani.

Makonda alisema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Wakuu wa Wilaya juu ya kuwalinda wananchi na mali zao na kuhakikisha usalama unakuwepo katika Wilaya wanazozisimamia.

Alieleza kuwa kwa kuwa wao ndio wanaomuwakilisha Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika Wilaya zao, wanatakiwa kuhakikisha wametekeleza ahadi zilizotolewa na Mhe. Rais wakati wa kampeni.

“Ningependa wakuu wangu wa Wilaya mchukiwe kwa kusimamia Haki na Sheria kuliko kukumbatia uovu kwa kuhitaji furaha ya muda mfupi, hakikisheni Sheria na Kanuni zilizopo kwenye Katiba ndio ziwe muongozo wenu”, alisema Makonda.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam aliwataka Wakuu wa Wilaya zake kuwasimamia Wakurugenzi wao ili kuhakikisha wanatumia bajeti waliyopewa katika kutatua changamoto zilizopo katika Wilaya zao.

Aidha, Makonda amewasisitiza kuhakikisha kuwa kuanzia Julai 11 mwaka huu maeneo yote yanayofanya biashara ya shisha kufungwa na kuweka maeneo maalumu kwa ajili ya kuvutia sigara.

Wakuu wa Wilaya wapya wamepewa wiki mbili za kutengeneza mpango kazi kwa kusoma ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Hotuba ya Mhe.Rais John Magufuli aliyoisoma wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na mazingira ya kazi katika maeneo yao.

No comments: