ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 2, 2016

MAWAKILI TANZANIA WAFIKIA 5800 SASA

Na Lydia Churi, Mahakama ya Tanzania
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman amewakubali na kuwaapisha Mawakili wapya 624 na kuifanya Tanzania kuwa na jumla ya Mawakili 5800. 
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa sherehe za kuwaapisha Mawakili leo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu wa Tanzania alisema mawakili walioapishwa wanatoka katika maeneo mbalimbali ikiwemo Serikalini, sekta binafsi, mashirika ya Umma na halmashari mbalimbali nchini.
Alisema hivi idadi ya Mawakili inaendelea kuongezeka ambapo mwezi Desemba mwaka huu Mahakama inatarajia kuwaapisha mawakili wengine zaidi ya 300. Aliongeza kuwa  kwa upande wa Afrika Mashariki, Kenya inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mawakili ambapo ina zaidi ya Mawakili 14,000.  Uganda kwa upande wake inayo mawakili 2500.
Aidha, Jaji Mkuu aliwataka mawakili walioapishwa leo kutekeleza wajibu wao katika maeneo matatu ambayo ni kuwajibika kwa wateja wao kwa kuhakikisha wanatoa huduma kwa viwango vya kuridhisha.
Aliyataja maeneo mengine mawakili hao wanayopaswa kutekeleza wajibu wao kwa ni kwa mahakama ya Tanzania pamoja na kuwajibika kwa taaluma yao kwa kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo.     
Akizungumzia hatua ya mawakili wengi kufanya kazi zao maeneo ya mijini zaidi kuliko maeneo mengine, Jaji Mkuu alisema hatua hiyo inatokana na sababu za kiuchumi zaidi ingawa baadhi ya mawakili walioapishwa leo wanatarajia kwenda kufanya kazi ya kutoa msaada wa kisheria katika mikoa mbalimbali nchini na wengine ni wale walioajiriwa na halmashari mbalimbali nchini.
Sherehe za kuwakubali na kuwaapisha Mawakili  zimefanyika kwa mara ya 54 tangu kuanzishwa kwa sherehe hizo mwaka 1986 hapa nchini.

No comments: