Advertisements

Saturday, July 9, 2016

Muro aigomea TFF, Awazodoa Simba

Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro.

Nicodemus Jonas, Dar es Salaam

SASA ni rasmi kwamba Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro amefungiwa kwa mwaka mmoja kujihusisha na mambo ya soka na kutakiwa kulipa faini ya Sh milioni tatu.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, jana aliliambia Championi Jumamosi kuwa, Muro amefungiwa na Kamati ya Maadili kutokana na kupingana na maelekezo ya shirikisho hilo

Inaelezwa kuwa, Muro alipingana na maelekezo ya TFF wakati wa maandalizi ya mchezo kati ya Yanga na TP Mazembe wa Kombe la Shirikisho Afrika huku shitaka la kuishambulia TFF kwenye vyombo vya habari likitupwa.

“Kamati imemfungia Muro kwa mwaka kujihusisha na mambo ya soka na kutakiwa kulipa faini ya Sh milioni tatu lakini anayo nafasi ya kukata rufaa kama hajaridhishwa na hukumu.

“Kisheria ndani ya wiki moja atapokea barua yake na muda wowote kuanzia leo (jana) barua itamfikia mlengwa,” alisema Lucas.

Wakati hayo yakiendelea, Muro mwenyewe ameliambia gazeti hili kwamba, hatambui hukumu hiyo kwani TFF wala kamati zake hazina mamlaka ya kumsimamisha kazi.

Alisema bado anatambua kuwa yeye ni ofisa habari wa Yanga miaka mingi ijayo na zaidi ya uongozi wa klabu hakuna wa kuweza kumziba mdomo.

“Ngoja nifike mjini muone moto wangu, kwa sasa niko kijijini narudi huko ili nionane nao. Siwezi kukata rufaa, kwanza ya nini wakati hakuna kifungu cha katiba chenye mamlaka ya kunifungia mimi?” alihoji Muro.

No comments: