Advertisements

Saturday, July 9, 2016

Kikwete apigiwa debe kuiongoza AU

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Na Leonard Msigwa/Mtandao/GPL.

Kuanzia kesho jumapili jiji la Kigali, Rwanda litakuwa na ugeni mzito wa viongozi wa juu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya nchi huru za Afrika (AU). Ni mkutano wa kawaida wa 27thutakaoanza kesho na kumalizika julai 18,2016 ndani ya jengo la kisasa la Kigali Constructed Convection Centre (KCC), likiwa moja ya majengo bora ya hadhi ya juu kusini mwa jangwa la Sahara.

Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akifanya yake katika jamii.

Ni katika jengo hili jipya la kisasa Rais wa sasa wa Jumuiya ya Afrika mwanamama Dlamini-Zuma atakabidhi uongozi kwa mtu mwingine atakayechaguliwa na baadaye kuidhinishwa na viongozi wa juu wa jumuiya yenye makazi yake ya kudumu jijini Addis Ababa, Ethiopia.Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete anapigiwa chapuo kubwa sana la kuwa mrithi wa mwanamama Dlamini-Zuma ambaye ni mke wa zamani wa Rais wa sasa wa Afrika Kusini bwana Jacob Zuma. Bwana Kikwete anapewa nafasi kubwa ya kuongoza chombo hicho muhimu kutokana na ukweli kwamba mama Dlamini-Zuma ameweka bayana hatogombea tena nafasi hiyo.


Jina la Dr. Kikwete linaonekana kuwa gumzo zaidi miongoni mwa majina yanayopewa chapuo la kumrithi mama Dlamini-Zuma, ambaye hajarudisha fomu za kuwania awamu ya pili ya miaka minne, na mpaka sasa bado haijawekwa wazi sababu hasa zilizopelekea mwanamama huyo kutogombea tena. Ambaye mkataba wake umemalizika toka mwezi machi mwaka huu baada ya kuchaguliwa mwaka 2012.

Nchini Afrika Kusini tetesi zimezagaa kwamba mwanamama huyo anajiandaa na mbio za Urais ndani ya chama tawala cha African National Congress (ANC) aweze kuwa mrithi wa Rais Zuma ambaye atastaafu mwaka 2019. Mwanamama Dlamini-Zuma anataka apate muda wa kutosha kuweka mizizi ndani ya chama tawala kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2019.

Ni lazima viongozi wa juu wa mataifa yanayounda umoja wao wapitishe mrithi wa mama Dlamini-Zuma na endapo suala hilo lisipofanikiwa zoezi hilo litaahirishwa hadi mwakani mwezi wa kwanza katika mkutano mkuu wa viongozi wa juu wa mataifa ya Afrika.

Jina la Dr Kikwete limekuwa likitajwa sana kutokana na ukweli kwamba nafasi hiyo kwasasa inahitaji mtu mwenye uzoefu kimataifa na mwenye uwezo wa kujipambanua kwenye medani za kimataifa. Moja ya lawama anazopewa mwanamama Dlamini-Zuma ni ukimya wake uliopitiliza wa kushindwa kukemea mambo mbalimbali yanayohusu umoja huo. Pia analaumiwa kwa kutokuwa kiongozi mwajibikaji.

Pamoja na mwanamama Dlamini-Zuma kumaliza muda wake mrithi wake atapokea uongozi na changamoto nyingi zikiwemo sura ya AU kimataifa, uhakika wa mapato ya jumuiya, na kuhakikisha malengo ya jumuiya yanafikiwa mwaka 2063, ikiwa ni maadhimio ya mwaka 2013. Hivyo anahitajika kiongozi msikivu na mwerevu ambaye mbali na kuongea pia awe mtekelezaji.

Ni dhahiri Dr Kikwete anaonekana kuwa aina ya kiongozi anayehitajika, amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa kipindi cha miaka kumi na baadaye kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka kumi. Hivyo anauzoefu na masuala ya kimataifa kwa miaka zaidi ya miaka 20.

Usikivu wake wa kusikiliza pande zote , uvumilivu wa kusemwa vibaya, uhuru wa vyombo vya habari wakati wa utawala wake na ujenzi wa barabara za kiwango cha lami pamoja na kuboresha elimu na afya umempa sifa kubwa kimataifa. Anatajwa kama mwanadiplomasia bora wa sasa wa Afrika. Pia ni mbunifu bora wa kutafuta njia bora ya kumaliza matatizo yanayo wazunguka wale anaowaongoza. Itakuwa vyema endapo atakabidhiwa jukumu hilo kwasababu viongozi wengi waliopo madarakani wengi wao wamefanya kazi pamoja na Dr. Kikwete kipindi akiwa waziri na baadaye Rais. Hivyo kurahisisha namna bora ya kuzungumza nao.

2 comments:

Anonymous said...

I don't think people of South Africa are ready to have another Zuma in the country.

Anonymous said...

No comments