ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 27, 2016

RC Makonda aibua ufisadi ujenzi Machinga Complex

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
By Raymond Kaminyoge, Mwananchi rkaminyoge@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amebaini kuwapo kwa tuhuma za ufisadi katika ujenzi wa vyumba 4,200 vya jengo la Machinga Complex badala ya 10,000 kwa Sh12.7 bilioni.

Ni baada ya kupitiwa mkataba uliosainiwa kati ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Halmashari ya Jiji la Dar es Salaam na kubaini kuwa vyumba 5,800 havijajengwa licha ya kiasi hicho cha fedha kulipwa kwa mkandarasi.

Makonda alisema jana kuwa jengo hilo lilitakiwa kuwa na ghorofa sita badala yake zipo nne kutokana na vyumba hivyo kutojengwa.

Alisema NSSF ambao ndiyo wakopeshaji walikuwa wakimlipa mkandarasi wa jengo hilo badala ya jiji kinyume na mkataba huo. “Mkataba ulitaka NSSF watoe mkopo wa Sh12.7 bilioni kwa jiji, lakini hawakufanya hivyo badala yake wao ndiyo wakawa wanawalipa makandarasi wa jengo hilo,” alisema.

Alisema wakati NSSF wakikabidhi jengo hilo kwa jiji mwaka 2010 lilikuwa likidaiwa Sh19.7 bilioni, lakini hadi Machi 31,mwaka huu deni limefikia Sh38 bilioni zilizotokana na riba.

Hata hivyo, Meneja wa Masoko na Uhusiano wa NSSF, Eunice Chiume alisema hawana taarifa kuhusu tuhuma hizo kwa maofisa wao na kuahidi kutoa maelezo baada ya kufuatilia.

Kuhusu mkataba huo, Makonda alisema unaonyesha mkopaji jiji angeanza kurejesha mkopo huo kuanzia Desemba 2008 wakati ujenzi huo ungekuwa umekamilika.

Makonda alisema deni la Sh38 bilioni halilipiki na kwamba mkataba huo ni wa ovyo na haukutakiwa kusainiwa.

Alipendekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwachunguza na kuwafikisha mahakamani watu waliohusika katika mkataba huo.

Mmoja wa machinga hao, Hussein Mustafa alisema licha ya jengo hilo kujengwa kwa ajili yao, wapangaji ni wafanyabiashara wakubwa.

“Sisi tunaendelea kupanga bidhaa zetu pembezoni mwa barabara wakati tulitakiwa kuwa kwenye jengo,” alisema.

1 comment:

Anonymous said...

Hii ni hadithi ndani ya hadithi. Haya maneno ya NIME... NIME.., ina maana alifanya huu uchunguzi yeye au Kamati iliyofanya na kumletea taarifa. Na kwa nini hiintaarifa hakuweza kukaa na Meya wa jiji kulifanyia kazi kwanza. Hii copy paste ni hatari sana viongozi fanyeni kazi kwa umahiri zaidi.