Advertisements

Thursday, July 21, 2016

RC MKOANI PWANI HANA GARI ALAZIMIKA KUTUMIA LA DC KISARAWE

Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, akizungumza na baadhi ya watumishi wa umma na wakurugenzi mkoani hapo juu ya changamoto zinazowakabili watumishi na sekretariet ya mkoa pamoja na hatua wanazozichukua kukabiliana nazo.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani pamoja na katibu tawala wa mkoa huo hawana usafiri wa uhakika katika kutekeleza majukumu yao ya kazi hali ambayo inasababisha mkuu wa mkoa huo kutumia gari la mkuu wa wilaya ya Kisarawe ambae bado hajaripoti kazini.

Aidha baadhi ya wakuu wa wilaya magari yao ni mabovu ikiwemo gari la mkuu wa wilaya ya Kibaha huku maafisa tarafa 26 kati ya 27 waliopo mkoani hapo wanakabiliwa na tatizo la kukosa pikipiki wanazotumia kwenye kazi zao.

Akizungumzia changamoto zinazoikabili sekretarieti ya mkoa huo,mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo alisema analazimika kutumia gari la mkuu wa wilaya ya Kisarawe kwasasa.

Alielezea kuwa anatumia gari hiyo kutokana na mkuu huyo wa wilaya bado hajamwapisha kutokana na kutoa udhuru maalum na endapo mkuu huyo wa wilaya ataanza kazi yeye atakuwa hana gari la kutumia.

Mbali na hayo ,mhandisi Ndikilo alisema wanakabiliwa na changamoto nyingine ya uhaba wa fedha za matumizi ya kawaida (OC)ambapo uhaba huo unatokana na kushuka kwa ukomo wa bajeti  mwaka hadi mwaka hususan katika mwaka wa fedha 2015/2016 ulishuka kwa asilimia 40 ikilinganisha na ukomo wa fedha katika kipindi cha nyuma.

Alisema fedha pia za matumizi ya kawaida zinazopokelewa kila mwezi ni pungufu tofauti na kiasi cha fedha iliyopangwa hivyo kuathiri sekretarieti ya mkoa katika kutekeleza majukumu yake.

“Changamoto hii ni kubwa ambayo inasababisha kuzalisha changamoto nyingine ikiwemo madeni ya watumishi ambayo hadi sasa yamefikia mil.152”

“Watumishi hawapati stahiki zao kwa wakati na mazingira ya kazi yakikabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo watumishi wengine wanaamua kuhama na kwenda kufanya kazi kwingine ambapo wanafikiri wataweza kutumiwa vizuri na kupata maslahi mazuri”alisema mhandisi Ndikilo.

Akizungumzia juu ya upungufu wa vitendea kazi alisema pikipiki kwa maafisa tarafa ni tatizo jingine ambalo linahitaji kushughulikiwa.

Mhandisi Ndikilo alieleza ni tarafa moja ya Kaskazini Mafia iliyo nzima kati ya maafisa tarafa 27 waliopo mkoani Pwani.

Alisema kuwa maafisa tarafa hao ni mkono wa kulia wa wakurugenzi na wakuu wa wilaya ndio wanaochapa kazi katika pande hizo lakini hawana usafiri wa uhakika.

Alisema sekretarieti ya mkoa ,wataalamu na maafisa tarafa hushindwa kutembelea mamlaka za serikali za mtaa na maeneo mbalimbali kwa lengo la kufuatilia miradi  na shughuli zinazopaswa kufuatilia na hata wakitembelea inakuwa sio kwa kiwango kinachotakiwa .

Mhandisi Ndikilo alisema zipo hatua wanazozichukua ikiwa ni sanjali na kufikisha changamoto hizo katika wizara na idara husika ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi.

Hatua nyingine ni madeni ya watumishi kufikishwa hazina ili yaweze kulipwa licha pamoja na kuwasilisha taarifa hizo lakini hazina bado haijalipa kwa wakati.

Hata hivyo Mhandisi Ndikilo alielezea kwamba baadhi ya maafisa tarafa hawana ofisi za kudumu wanalazimika kutumia ofisi ambazo hazina hadhi huku kukiwa hakuna huduma muhimu za maji na umeme.

Mkuu huyo wa mkoa alisema ofisi ya mkoa imeshajenga ofisi 6 kati ya 27 zinazohitaji kwa maafisa tarafa hao.
Mhandisi Ndikilo aliiomba ofisi ya rais ,utumishi wa umma kuangalia kwa ukaribu matatizo hayo ili kuyatafutia ufumbuzi kwani ni moja ya sababu zinazokwamisha utekelezaji wa ufuatiliaji na jitihada za kuinua maendeleo ya mkoa kwa haraka.

No comments: