Advertisements

Sunday, July 3, 2016

SERENGETI FULL SHANGWE

Kikosi cha Serengeti Boys
Mwandishi Wetu TIMU ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, jana ilisonga mbele hatua ya pili ya michuano ya kufuzu kucheza Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa umri huo, baada ya kuifunga Shelisheli mabao 6-0.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alferd Lucas aliyepo mji wa Victoria ilipochezwa mechi hiyo, Serengeti ilimudu dakika zote za mchezo na kuonekana kana kwamba ilikuwa nyumbani.

Ushindi huo umeifanya Serengeti kusonga mbele kwa jumla ya mabao 9-0 baada ya kushinda mabao 3-0 nyumbani takribani wiki moja iliyopita. Serengeti ilianza kuhesabu bao katika dakika ya tisa likifungwa na Ibrahim Abdallah aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Shelisheli alipokuwa akijaribu kudaka mpira wa Asad Ali.

Dakika ya 43, Mohamed Abdallah aliipatia Serengeti bao la pili kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Shelisheli, bao hilo liliifanya Serengeti kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0. Asad Juma aliifungia Serengeti bao la tatu kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja kwenye nyavu za Shelisheli katika dakika 50.

Bao la nne la Serengeti lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Issa Makamba katika dakika ya 61 kabla mfungaji wa bao la tatu Juma hajaongeza la tano katika dakika ya 70 na dakika ya 90 Yohana Nkomola kumalizia kwa bao la sita.

Kwa matokeo hayo, timu hiyo sasa inayoongozwa na kocha Bakari Shime itacheza na timu ya vijana ya Afrika Kusini na mshindi wa mechi hiyo atafuzu michuano hiyo itakayofanyika Madagascar mwakani.

Serengeti Boys iliwahi kufuzu fainali za michuano hiyo zilizofanyika Gambia mwaka 2005, lakini ilienguliwa baada ya kumtumia mchezaji Nurdin Bakari aliyezidi umri. Ufaransa

HABARI LEO

No comments: