Advertisements

Thursday, July 21, 2016

USO KWA USO NA MRAMBA, YONA WAKIFANYA USAFI

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Nawaona wakiwasili katika Hospitali ya Sinza Palestina wakiwa ni wenye bashasha usoni, wakitembea kama watu wasio na haraka.

Hawa ni mawaziri wawili wa zamani; Daniel Yona wa Nishati na Madini na Basil Mramba wa Fedha, walipokuwa wanawasili eneo la hospitali hiyo tayari kutumikia adhabu yao. Wafungwa hao hufika hospitalini hapo siku nne kwa wiki, kutumikia adhabu yao ya kifungo cha nje kwa kufanya kazi za jamii.

Mramba na Yona walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja na kutakiwa kulipa faini ya Sh5 milioni, kutokana na kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh17 bilioni.

Hata hivyo, baada ya kutumikia adhabu hiyo kwa mwaka mmoja, walipunguziwa na kufungwa kifungo cha nje kuanzia Februari hadi Novemba 9 mwaka huu, wakitakiwa kufanya kazi za jamii.

Wanavyotumikia adhabu

Muda wa kuwasili hospitalini hapo kisheria kwa ajili ya kuanza kutumikia adhabu ni saa mbili asubuhi na kumaliza ni saa sita mchana, lakini jana walifika saa 1.49 asubuhi na kusubiri hadi saa mbili ili wasaini kuanza kazi.

Kama ilivyo ada walisaini na kuanza kazi maeneo ambayo ratiba yao inaonyesha.

Waliingia chumba cha kubadilishia nguo, baada ya muda wakatoka wakiwa wamevaa sare za bluu, glovu na viatu maalumu vya kufanyia usafi. Kwa jana, ratiba yao iliwataka kufanya usafi eneo la vipimo na nyuma ya wodi ya wazazi.

Huku wakiendelea na usafi eneo la vipimo; wafungwa hao walionekana kufahamu wanachokifanya kutokana na kusafisha vioo, kudeki kwa kutumia kifaa maalumu kwa kazi hiyo na kufuta viti vinavyokaliwa na wagonjwa.

Baada ya kumaliza kusafisha eneo hilo walihamia nyuma ya wodi ya wazazi. Mwandishi wa gazeti hili akiwa hospitalini hapo aliwasalimia bila kujitambulisha.

Mwandishi: Habari za asubuhi?

Yona, Mramba: (kila mmoja anaitikia) Salama, habari za leo.

Mwandishi: Nzuri shikamooni

Yona, Mramba: Marahaba

Yona: Kumekucha

Mwandishi: Naam, naona mnaendelea na kazi

Yona: Ehee

Bila ajizi saa 5.53 asubuhi wanakusanya vifaa vyao, ikiwamo kuanua vitambaa walivyokuwa wanatumia kufuta madirisha ambavyo walivifua kabla na kuvianika na kuingia tena chumba cha kuhifadhia vifaa.

Walikaa chumbani kwa muda kabla ya kutoka saa 6.02 mchana wakiwa wamevaa kawaida na kuondoka taratibu, huku wakiwasalimia baadhi ya vijana waliokutana nao nje kama vile wanafahamiana.    

No comments: