Advertisements

Thursday, July 21, 2016

WACHINA WATOA TRILION 15 RELI YA KATI YA KISASA

Rais John Magufuli akizungumza na Rais wa Benki ya Exim ya China, Liu Liang (kulia) katika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma jana. Kushoto ni Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing. (Picha na Ikulu).
Rais John Magufuli akizungumza na Rais wa Benki ya Exim ya China, Liu Liang (kulia) katika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma jana. Kushoto ni Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing. (Picha na Ikulu

BENKI ya Exim ya China imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani bilioni 7.6 sawa na zaidi ya Sh trilioni 16 kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi mkubwa wa Reli ya Kati nchini kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) unaotarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha.

Rais wa Benki ya Exim ya China, Liu Liang amemueleza Rais John Magufuli jana Ikulu ndogo ya Chamwino mjini Dodoma, kuwa pamoja na kutoa fedha hizo zitakazofanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za Reli ya Kati, benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli.

Pamoja na kukubali kutoa fedha hizo, Rais huyo wa Benki ya Exim ya China amempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa dhamira ya dhati ya kuiletea nchi maendeleo, ikiwemo kuharakisha ujenzi wa Reli ya Kati na ameahidi kuwa benki yake itatoa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha mradi huo na miradi mingine ya maendeleo.

“Kuhusu huu mradi wa Reli ya Kati tuna mtazamo chanya, tunauona ni mradi mzuri na tutatoa ushirikiano wowote utakaohitajika. Tunaamini kuwa kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania mchakato wa utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa mafanikio na kwa kuzingatia muda,” alisema rais huyo wa Benki ya Exim.

Kwa upande wake, Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Benki ya Exim ya China kwa kukubali kutoa fedha hizo na amemhakikishia kuwa Tanzania imedhamiria kutekeleza mradi huo ambao tayari ujenzi wake umepangwa kuanza katika mwaka huu wa fedha kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha Sh trilioni moja zilizotengwa katika bajeti.

Rais Magufuli amebainisha kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Kwa hiyo kukubali kwao ambako ilikuwa ni kitu kikubwa, inaonesha kwamba juhudi za Tanzania kwenda haraka haraka zinakubalika kimataifa, na wenzetu hawa Wachina wana pesa nyingi. Na kule kuaminika kwamba tunakopeshwa kwa masharti nafuu, riba yake ni ndogo na huku kwetu ni mafanikio makubwa, kwa hiyo mizigo mingi tutakuwa tunaisafirisha, tutaendeleza reli yetu na bandari zetu,” alisema Rais Magufuli.

Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati utahusisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam – Tabora –Isaka - Mwanza, Tabora – Mpanda -Kalemela, Tabora – Uvinza – Kigoma na Isaka – Keza – Msongati.

Mazungumzo kati ya Rais Magufuli na Rais wa Benki ya Exim ya China yamehudhuriwa na Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Suzan Kolimba.

HABARI LEO

1 comment:

Anonymous said...

Safi sana tunaimani chini ya uongozi wa Magufuli pesa zitazotengwa kwa ajili ya mradi huo mkubwa na muhimu katika nyanja ya usafiri kwa nchi yetu basi zitatumika kama zilvyokusudiwa.