MFANYABIASHARA maarufu, Mustapha Jaffer Sabodo ametangaza kutoa dola za Marekani bilioni 5 (Sh trilioni 10) kwa ajili ya kuwekeza mkoani Dodoma, ikiwa ni njia ya kumuunga mkono Rais John Magufuli kuhamisha makao makuu ya serikali kwenda mkoani humo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Sabodo alisema atawekeza kiasi hicho cha fedha, iwapo serikali yote itahamia mkoani humo, itakuwa ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alitamani kuona mkoa huo unakuwa makao makuu ya nchi.
Alisema alichofanya Rais Magufuli, kimewashinda marais wengine waliomtangulia, hivyo yeye kama mfanyabiashara na mtu mwenye mapenzi makubwa kwa nchi yake, lazima aunge mkono hatua hiyo ya Serikali kuhamia Dodoma ambayo aliita ‘Azimio la Dodoma’.
“Niliposikia anatangaza kwenye televisheni ya taifa kwamba Serikali itahamia Dodoma, ilikuwa mara yangu ya kwanza baada ya miaka mingi kupita, nilitabasamu moyoni, jambo ambalo lilinitokea miaka 10 ya kwanza ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.
“Leo nimesikia kutoka kwako nimeona ile roho ya Nyerere imezaliwa tena.
“Kwa hiyo natangaza kuunga mkono Azimo la Dodoma kwa kuwekeza dola za Marekani bilioni 5, ambazo zitatumika kwa ajili ya uwekezaji mkubwa katika huduma mbalimbali za jamii mkoani humo,” alisema Sabodo.
Sabodo alisema atatoa fedha hizo ili zitumike kuwekeza kwenye viwanda kama vya mvinyo, viwanda vya kusindika mihogo na viwanda vingine ambavyo vitahitajika katika mkoa huo.
Alisema kuwepo kwa huduma hizo mkoani Dodoma, kutasaidia kuufanya mji huo kukidhi matakwa ya watumishi wa umma watakaohamia huko.
Mfanyabiashara huyo aliongeza kuwa atafanya uwekezaji mkubwa huo kwa sababu lengo lake ni kuona mji wa Dodoma, unaungana na miji ya jirani kama Mpwapwa, Kondoa na Manyoni ili kutoa fursa ya kupanua huduma mbalimbali katika makao makuu hayo ya nchi.
Sabodo alisema kwamba juhudi zake za kuwekeza katika huduma za jamii kama shule, pia ataziendeleza katika mkoa huo kwa kuhakikisha kwamba zinajengwa shule kadhaa za kisasa, ambazo zitamudu mahitaji ya watu wa eneo hilo.
Kwa upande wa huduma ya afya, Sabodo alisema atatumia umaarufu wake kuwashawishi wamiliki wa Hospitali ya kimataifa ya Apollo ya India ili waje nchini wakashirikiane naye kujenga hospitali ya kisasa, ambayo itakuwa inatoa huduma za kisasa mkoani humo.
“Mnaifahamu hospitali ya Apollo ni wawekezaji wakubwa katika huduma za afya, kwa kusukumwa na hatua hii ya Rais nitaongea nao tushirikiane katika kujenga huduma za jamii katika mji huo,” alisema Sabodo.
Pia alisema atawashawishi wawekezaji wengine kutoka nchi za India, Singapore na kwingineko kuja kuwekeza katika mji huo wa Dodoma katika sekta ya viwanda, kuhakikisha kwamba azma ya Rais Magufuli ya kujenga uchumi wa viwanda inatimia.
Sabodo ambaye alisema wazi kuwa utendaji wa Rais Magufuli, umemvutia kutokana na hatua yake ya kupiga vita rushwa, alitangaza kuwa kuanzia sasa hatatoa tena msaada kwa vyama vya upinzani kama ambavyo amefanya miaka ya nyuma kama njia ya kuimarisha demokrasia nchini.
“Huko nyuma nilikuwa nawapa Chadema fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuimarisha demokrasia, sasa natangaza tena kwamba sitawapa tena fedha, niwape za nini wakati Rais aliyeko madarakani anafanya kazi ambayo ndio nilikuwa naipigania?" alihoji Sabodo.
Sabodo ni mfanyabiashara wa kitanzania mwenye asili ya Kihindi ambaye alizaliwa mkoani Lindi. Katika maisha yake amekuwa anafanya biashara katika nchi za Kenya, Ufaransa, India, Sudan na Zimbabwe.
Pamoja na biashara zake, Sabodo amekuwa anajihusisha kuchangia katika miradi ya maendeleo ya huduma za jamii, uimarishaji wa demokrasia nchini na pia alishiriki kutunisha mfuko wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kuanzisha bahati nasibu.
1 comment:
Safi sana kizuri kitajiuza tu hata kama watu watajaribu kukitia dosari na kibaya hata kama kitapakwa rangi nzuri na kutembeza hapa na pale lakini mwisho wa siku kitaishia kudoda tu. Licha ya kelele na unafiki wa upinzani juu ya Magufuli kuna nguvu moja tu ambayo mwisho wa siku ndio itakayotoa jawabu kati ya haki na batili na nguvu hiyo sio nyengine bali ni nguvu na jicho la M/Mungu alietukuka. Maghufuli ni mtanzania mwenzangu amapo imetokana kuwa na imani tofauti za dini kama ilivyo kwa watanzania utafauti wetu wa dini au kabila si kitu kinachotuondeshea mshikamano wetu na Mungu azidi kutupa baraka juu ya hili Amini. Lakini kubwa kuliko yote ni Ukweli na uadilifu wa hali ya juu katika utendaji wake wa kazi wa Magufuli,jambo ambalo linanifanya kumsapoti muheshimiwa Maghufuli na nitaendelea kumsapoti labda nijiridhishe yakuwa anafanya mambo ya hovyo ya kutengua uadilifu wake aliokuwa nao sasa na sio yale makosa ya kibinaadamu kwani Magufuli ni binadamu pia kukosea ni lazima. Tunaimani kabisa yakwamba kama mueshimiwa Magufuli na serikali yake wataendelea na kasi hii hii ya nidhamu na uadilifu katika utendaji wao wa kazi basi kuna akina Muheshimiwa Sabodo wengi tu kutoka nje na ndani ya Tanzania watakaokuja kuekeza. Inashangaza sana unapoona wapinzani wakimpiga vita Magufuli kwa nia yake nzuri ya kupambana na kuhakikisha maisha ya mtanzania yanakuwa bora. Kwa kiasi fulani ni jambo la kusikitisha na kwa bahati mbaya inaokena hata baadhi ya vyombo vya habari Tanzania vinashiriki katika kuupotosha umma juu ya kazi nzuri na ngumu anayoendelea kuifanya Magufuli. Mueshimiwa raisi anahitaji kuungwa mkono na watanzania wote wenye kuitakia mema Tanzania kwa nguvu zetu zote. Wale waliokuwepo kule nyumbani,wa Europe,wa Amerika, wa Asia, wa America kusini,Australia nakadhalika nakadhalika bila ya kujali tofauti zetu za kisiasa kwani kiuhalisia hatumsapoti Magufuli bali tunaisapoti Tanzania yetu. Kama wewe ni mpinzani na unahasira au wivu na kasi ya Maghufuli sidhani kama busara kupika majungu na kupita kusambaza uongo, badala yake kama unaweza zidisha kasi yako ya maendeleo izidi ya Magufuli jitahada zako zitaonekana kama anavyoonekanwa Magufuli hivi sasa. La kama mpinzani huwezi kuizidi kasi yake basi muunge mkono na kama huwezi kumuunga mkono basi ni bora kukaa kimya kuliko kumpiga vita na kumvunja moyo kwani mwisho ya siku watu makini na wenye uchungu na nchi waliokuwa wanasapoti wapinzani kwa manufaa ya Tanzania kama akina Muheshimiwa Sabodo watawacha mkono mmoja baada ya mwengine ni jambo la hatari kuwa na upinzani dhaifu nchini bado tunahitaji upizani imara wa kuipa CCM changamoto lakini kwa upinzani huu tuliokuwa nao unaongozwa na akina Mbowe wakupinga kila kitu anachofanya Magufuli hata vile vitu ambavyo havihitaji hata kuambiwa kuwa ni jambo nzuri kama vile kupigania watoto wote wa kitanzania wanapata Elimu ya lazima na bure basi kwa upinzani kushindwa kutambua angalau hilo kwa hakika hakuna faida ya upizani tuliokuwanao wa kisiasa Tanzania kwani si upizani bali ni fitna. Hata kama kutakuwa na mapungufu kwa yale alioyaanzisha muheshimiwa Maghufuli kiukweli ni kwamba kitu chochote kinahitaji maboresho na hapo ndipo watanzania utilitarajia upizani kuonesha uwezo wao jinsi gani wangetoa mchango wao juu ya maboresho ya yale aliyaanzisha Magufuli lakini badala yake tunashuhudia dharau na kejeli kwa kweli inasikitisha,upizani mmetuangusha hiyo sio aina ya demokrasia tulioitarajia kutoka kwenu. Ningechukua nafasi kumpongeza muheshimiwa Sabodo kwani yeye ni mtanzania na mzalendo wa kweli.
Post a Comment