Advertisements

Thursday, August 25, 2016

MAUAJI YA POLISI DAR PASUA KICHWA

Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya

WAKAZI wa Mtaa wa Mbande Magengeni katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam walioshuhudia tukio la mauaji ya askari polisi wanne na kujeruhi raia wawili juzi usiku, wamelielezea kuwa ilikuwa kama ni sinema ya kizungu, kwa kuwa wamezoea kuona mambo hayo kwenye filamu na si kwa kushuhudia.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi nchini linawasaka watu wenye silaha waliofanya shambulio dhidi ya askari wa jeshi hilo na kusababisha vifo vya askari wake wanne wakiwa kazini na kujeruhi raia wawili.

Kundi la watu wanaodhaniwa kuwa majambazi ambao idadi yao haijajulikana walivamia eneo la Benki ya CRDB tawi la Mbande, na kuwaua kwa risasi askari wanne waliokuwa wakibadilishana lindo na kujeruhi wananchi wengine wawili.

Akisimulia tukio la kujeruhiwa na risasi mkononi, mmoja wa majeruhi hao, Aziz Ally ambaye ni muuza chipsi katika mgahawa wa jirani, alisema risasi hiyo ilimpata wakati akikimbia kutafuta eneo la kujificha ili kuokoa uhai wake.

Alisema wakati tukio hilo linatokea alikuwa akiwahudumia wateja wake wawili, lakini ghafla alianza kusikia milio ya risasi ambapo walikimbia ili kujificha na ndipo ilipompata risasi hiyo. “Namshukuru Mungu nilitibiwa usiku ule ule hospitali ya hapo jirani na nilishonwa nyuzi sita… sasa hivi nina maumivu tu, lakini namshukuru sana Mungu,” alisema Aziz.

Naye Meneja wa mgahawa wa Swabran n Jamil uliopo karibu na benki hiyo, Abdallah Salum alisema majira ya saa 1:15 usiku wakati wakiendelea na shughuli zao katika mgahawa huo, ghafla walianza kusikia milio ya risasi.

Alisema awali walidhani ni kawaida ya askari hao ya kupiga hewani risasi moja au mbili wanapokwenda kubadilishana lindo, lakini waligundua milio hiyo si ya kawaida kwani risasi ziliendelea kurindima mfululizo bila kukoma ambapo waliamua kulala chini ili kuokoa maisha yao.

Aliongeza kuwa, miongoni mwa watu wawili waliojeruhiwa mmoja ni kijana wake wa kuuza chipsi nje ya mgahawa huo ambaye risasi ilimpata kwenye mkono wake wa kushoto.

Alisema milio hiyo ya risasi awali ilisikika kwa dakika tano mfululizo na baadaye ilipoa na kuendelea tena kwa dakika kati ya tatu hadi nne, na hivyo kufanya tukio hilo kuchukua muda wa dakika 15.

Shuhuda mwingine wa tukio hilo, Winnie Ngibwa alisema tangu majira ya saa 10:30 hadi saa 11:00 jioni alimuona kijana ambaye alikuja kusimama mbele ya duka lake na kumtilia shaka kuwa si mtu mzuri.

Alisema baadaye aliamua kufunga duka lake kwa kuwa alikuwa hajisikii vizuri tangu amuone kijana huyo na kwamba baada ya kufunga na kuanza kuondoka ndipo alianza kusikia milio ya risasi ikitokea eneo hilo la benki.

“Nafikiri sasa kuna ulazima wa kujenga kituo kikubwa cha polisi, tumekuwa tukisema kila siku, lakini hakuna kinachotekelezwa. Mbande imekuwa kubwa, siyo tena ile ya zamani,” alisema Winnie.

Kauli ya Polisi

Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya alisema katika tukio hilo ambalo ni shambulizi dhidi ya Polisi, watuhumiwa hao walipora bunduki mbili aina ya SMG na risasi 60 na kutokomea nazo.

“Majambazi ambao idadi yao haikufahamika, wakiwa na silaha za moto walivamia Benki ya CRDB tawi la Mbande ambapo waliwashambulia na kuwaua askari wanne wa Jeshi la Polisi waliokuwa kazini na kujeruhi raia wawili waliokuwa jirani na eneo hilo,” alisema Kamishna Mssanzya.

Alisema msako mkali unaendelea na kwamba watuhumiwa hao watapatikana na kuchukuliwa sheria, hivyo kuwataka wananchi na jamii kwa ujumla kushirikiana na polisi kutoa taarifa dhidi ya watu au vikundi vyovyote vya kihalifu ili wawatie nguvuni.

Aliwataja askari waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni askari wawili wenye cheo cha Koplo waliotambulika kwa majina moja moja ya Yahaya na Hatibu, na wengine wawili waliotambuliwa kwa majina ya Tito na Gaston huku raia waliojeruhiwa kuwa ni Aziz na Ally Chiponda, wote wakazi wa Mbande.

“Ni dhahiri kuwa, wahalifu hao walikuwa na kusudio moja tu la kushambulia askari Polisi, kwani baada ya kufanikiwa kupora silaha hizo hawakusogelea kabisa jengo la Benki na hakuna fedha au mali iliyoibwa au kuharibiwa,” alisema Kamishna huyo.

Alisema kutokana na eneo hilo kuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu ilikuwa ngumu kubaini kwa haraka nyendo zozote za kihalifu, kwani hata watuhumiwa hao walifika hapo wakiwa katika pikipiki na wengine wakitembea kwa mguu.

Aidha, alilaani waliobeza na kukejeli kupitia mitandao ya kijamii mazoezi ya kawaida yanayofanywa na Jeshi la Polisi, huku wengine wakiandika ujumbe wa kushabikia kuuawa kwa askari hao.

“Wale wote walioandika au kusema maneno kwa lengo au nia ya kushabikia uhalifu huo tutawasaka, na wapo waliodiriki hata kuandika ujumbe unasema kwamba, endapo watapigwa na Polisi Septemba mosi, basi viongozi wa Jeshi la Polisi wawaondoe askari wanaoishi uraiani na kuwarudisha kambini, la sivyo watawashambulia,” alisema Marijani.

Pia alisema wapo baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wamesikika katika majukwaa ya kisiasa wakihamasisha wafuasi wao washambulie polisi.

Aidha alisema katu tukio hilo la mauaji halitalitereresha jeshi hilo na badala yake litaendelea na azma ya kulinda raia na mali zao na kuongeza kuwa nchi ipo salama.

Mwigulu anena

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro ni miongoni mwa viongozi wa jeshi hilo waliofika eneo la tukio muda mfupi baada ya mauaji kutokea.

Kwa upande wake, Mwigulu alisema serikali haitaishia kulaani tu mauaji na matukio hayo ya kihalifu yanayosababisha mauaji, bali alitoa rai kwa wahusika wa tukio hilo kujisalimisha wenyewe na kuwataka raia kushirikiana na Polisi nchini kufichua wahalifu.

“Hatutaishia kulaani tu tukio hili na matukio mengine kama haya, natoa rai kwa wahusika kujisalimisha. Vilevile wananchi na raia wema tunaomba ushirikiano wenu katika vita hii ya kupambana na wahalifu hawa na wanaotuzunguka kwenye maeneo yetu,” alisema Mwigulu.

Kauli ya DC

Akizungumza baada ya kufika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva alisema kwa sasa vyombo vya dola tayari vimeshaanza kufanya msako wa kuwatafuta wahalifu hao ili kuhakikisha wanapatikana wakiwa hai au wamekufa.

“Lakini pia nimefurahishwa na kitendo cha wananchi wa hapa kuchanga matofali 4,500 na mifuko 33 ya sementi kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi,” alisema Lyaniva.

Aliongeza kuwa tayari Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ametoa mabati ya kuezekea kituo hicho na wananchi wa mtaa huo wameanza kuchangishana fedha kwa ajili ya mafundi, pia amemuagiza mtendaji wa mtaa huo kwenda polisi kwa ajili ya kupewa ramani ya ujenzi wa kituo hicho.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Sadiki Makwana alisema wakati gari la askari hao aina ya Ashok Leyland Stile lenye namba PT 3889 lilipofika eneo hilo, kabla ya askari kuteremka garini milio ya risasi ilianza kusikika ikilielekea gari hilo.

“Mlinzi mmoja aliyetoka kwa ajili ya kuwalaki wenzake ndiye aliyeanza kupigwa risasi kisha akapigwa dereva, kuna mlinzi mmoja alitoka kibandani baada ya kumuona mwenzake ameanguka akafanikiwa kukimbia huko nyuma kujificha kwa bibi,” alisema Makwana.

Akiwazungumzia wahalifu hao, alisema hadi sasa hawajawahisi ni watu wanaotokea maeneo gani, lakini baadhi ya wananchi wanadai waliwaona watu hao kwa kuwa walikuwa kwenye mavazi ya kawaida.

Alisema baada ya kufanya uhalifu huo watuhumiwa hao walikimbilia karibu na kituo kidogo cha polisi jirani na benki hiyo na kupanda pikipiki zao kisha kutokomea katika barabara ya Serengeti kuelekea Mvuti na kwamba walikuwa na silaha zao kabla ya kupora za askari hao.

Marufuku mikutano ya ndani

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku mikutano yote ya ndani ya vyama vya siasa kwa kile ilichodai mikutano hiyo inatumika kupanga mbinu za uchochezi.

Kamishina wa Polisi wa Oparesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya alisema si mikutano ya siasa tu, bali hata mikutano ya makundi mbalimbali ya jamii na vikao vya harusi ambavyo vitabainika kutumika kama majukwaa ya kisiasa.

“Jeshi la Polisi lilikuwa halijazuia mikutano ya ndani, kwa sababu ilikuwa inazungumzia au ilikuwa izungumzie suala la maendeleo ya wananchi, lakini katika kufuatilia mikutano hiyo tumegundua inatumika sasa kuchochea wananchi na kuwahamasisha kuvunja sheria za nchi na kufanya mapambano na polisi,” alisema.

Alisema mkutano unaweza kuwa wa halali, lakini inapofika jambo linalozungumziwa kinyume cha sheria mkutano huo unakuwa si halali tena.

Alisema awali iliaminika kuwa mikutano ya ndani ilikuwa ikijadili maendeleo ya wananchi, lakini imekuwa ikitumika tofauti hivyo kuanzia sasa amepiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya ndani.

Aidha, alisema kuna taarifa kuwa wapanda pikipiki maarufu kama bodaboda wanahamasishwa kufanya vurugu na kushambulia askari, alitoa onyo kwa bodaboda hao na wanaofanya biashara hiyo kutojihusisha na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria.

Alionya wamiliki wa pikipiki kuhakikisha zinatumika katika malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo tofauti na kinyume na hapo watachukuliwa hatua na pikipiki hizo kutaifishwa.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli aliwataka polisi kuhakikisha kuwa wanakabiliana vilivyo na watu wanaovamia vituo vya Polisi, kuua askari na kupora silaha.

HABARI LEO

No comments: