Advertisements

Thursday, August 25, 2016

WAKULIMA MBARONI KWA KUUA NG'OMBE 12

 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa

POLISI mkoani Dodoma inawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kusababisha vifo vya ng’ombe 11 wenye thamani ya Sh milioni 10.2 mali ya Simon Isaya (32).

Watu hao ni wakazi wa kijiji cha Chitego, kata ya Chitego Tarafa ya Zoisa Wilaya ya Kongwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa akizungumzia tukio alisema Jumanne saa 12 jioni katika kitongoji cha Suji, ng’ombe jike 10 na dume mmoja walikutwa wamekufa kwenye shamba la mkulima Simon Chihande (56) baada ya kula nyasi zilizokuwa zimewekwa sumu.

Kamanda huyo alisema upelelezi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni chuki binafsi ya mkulima huyo dhidi ya mfugaji. Hata hivyo, kijiji hicho mara nyingi hukumbwa na migogoro ya wakulima na wafugaji. Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Kenneth Mkapilani (32), Haji Juma (45), Ezekiel Mpakanyi (36) na Hamis Kondo (51).

Wote hao ni wakazi wa Chitego. Aidha, mabaki ya sumu inayosadikiwa kuwa ya panya yamepatikana shambani hapo na yamechukuliwa pamoja na sampuli za ng’ombe hao tayari kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linamshikilia Shabani Daud (36) ambaye ni mfanyabiashara wa Kibaigwa kwa kosa la kujeruhi baada ya kumuunguza mapajani mtoto wake kwa moto. Taarifa ya kuunguzwa kwa mtoto huyo iliripotiwa na mwalimu aliyetambulika kwa jina la Shida Lazaro wa Shule ya Msingi Karume, Kata ya Kibaigwa wilayani Kongwa.

Ilielezwa kuwa Jumatatu saa tisa alasiri mwalimu huyo alimgundua mwanafunzi huyo akiwa na majeraha ya moto maeneo ya mapaja ya miguu yote mwilini na kuamua kumuuliza mtoto huyo ambaye alisema kwamba ameunguzwa na baba yake mzazi.

Mtoto huyo, Baraka Daud (8) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule hiyo, alieleza kwamba Agosti 18, 2016 alichomwa na baba yake mzazi kwa kutumia kisu kilichokuwa na moto baada ya kurudi nyumbani kabla ya muda wa kutoka shule, ndipo mzazi alichukia na kumuadhibu kwa njia hiyo.

HABARI LEO

No comments: