Advertisements

Thursday, August 4, 2016

MKUU WA WILAYA YA IKUNGI ATOA ONYO KWA WANASIASA WANAOKOSESHA MAPATO YA HALMASHAURI

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwahutubia madiwani wa Wilaya ya ikungi ikiwa ni mara yake ya mwanzo tangu alipochaguliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo.
Kutoka Kushoto ni Eng Sadick Chakka Mhandisi wa Maji Wilaya ya Ikungi, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji jumanne Mtaturu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally J. Mwanga, na Kulia ni Abel Suri Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Wakuu wa Idara na Vitengo, na Madiwani wakisikiliza hotuba ya Mkuu wa Wilaya hiyo
Aliyesimama ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi akisisitiza jambo
Umakini umeonekana wazi wakati wa uwasilishwaji wa hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya ikungi Miraji Jumanne Mtaturu
Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii ambaye ni Diwani wa Kata ya Issuna Steven Misai akitoa neno la shukrani kwa hotuba ya mkuu wa Wilaya ya ikungi

Na Mathias Canal, Singida
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu amewaonya baadhi ya wanasiasa hususani madiwani katika Wilaya hiyo kupitia matamko yao ya kuzuia ukusanyaji wa ushuru au kupiga vita vizuizi vilivyowekwa katika kata zote.
Madiwani hao wanatumia vibaya Uelewa mdogo wa wananchi kwa kuwazuia kuchangia shughuli za maendeleo na ulipaji kodi hivyo amewaagiza madiwani wote kuacha kuwatumia wananchi kwa muktadha wa kuwanyima ufahamu bali wawe mstari wa mbele kuwaelimisha kwa kushirikiana na wataalamu wanaopita kukusanya  kodi katika maeneo yao.
Dc Mtaturu ameyasema hayo wakati wa kikao chake cha kwanza cha Baraza la madiwani la Wilaya hiyo tangu alipoteuliwa na Rais John Magufuli kushiriki kwenye baraza la madiwani ambapo pamoja na hotuba yake hiyo amewapongeza madiwani wote kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi katika kata zao.
Dc Mtaturu amesema kuwa Baraza la madiwani ndio injini kuu ya maendeleo ya Wilaya, hivyo kama kukiwa na Baraza lisilotimiza wajibu wake kamwe Wilaya haiwezi kutoka kwenye kadhia iliyopo hususani katika sekta ya Kilimo, Mifugo, uvuvi, elimu, afya na miundombinu.

“Wilaya yetu bado ina changamoto nyingi sana,  Natambua  Wananchi wengi bado ni masikini kama sio wenye kipato cha chini sana, Natambua Wananchi wengi wanajishughulisha na Kilimo na Ufugaji ingawa wapo Wachimbaji wadogo wa Madini na Wafanyabiashara pia lakini natambua huduma za jamii pamoja na miundombinu ni changamoto kubwa sana”
“Tumekuwa Wilaya ya kuomba chakula cha msaada kila mwaka, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi VVU yanazidi kupanda, Elimu inazidi kushuka, mapato ya Halmashauri yameshuka, wananchi wetu wamekuwa wakifuga na kulima kilimo kile kile cha mazoea, huduma ya maji safi na salama imeendelea kuwa changamoto kwetu, Vituo vya Afya na Zahanati havitoshelezi mahitaji” Alisema Mtaturu


Kwenye Huduma ya Afya katika Vijiji 101 vilivyopo Wilayani Ikungi kuna Zahanati 34, Vituo vya Afya 3 na Hospitali 2, kwa uwiano huu zisipofanyika jitihada zaidi hali ya wananchi itakuwa mbaya zaidi.

Hivyo Mkuu huyo wa Wilaya hiyo alisema kuwa Madiwani wote wanatakiwa kuwa na mpango mkakati wa kuhakikisha huduma za Afya zinapatikana kirahisi.

Katika hotuba yake Dc Mtaturu ameeleza kuwa Ni lazima kwenye Kamati za Maendeleo za Kata (WDC) kuanzishwe mipango ya kuhakikisha kunapunguzwa Vifo vya Wakinamama Wajawazito na Watoto kwa kuweka mikakati itakayohakikisha Wananchi wote hawaendi umbali mrefu kutafuta huduma za Afya.

Katika suala hili la Afya ningependa kuzungumzia mabadiliko katika Sekta ya Afya yanayoendelea hapa Nchini katika utoaji wa huduma. Mabadiliko haya yana lengo la kuinua kiwango cha ubora wa huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi na kuongeza kiwango cha uwajibikaji kwa wasimamizi na watoaji wa huduma hizo.  Ili kufanikisha lengo hilo, madaraka, majukumu na kazi, rasilimali zaidi za afya zinahitajika kwa kuitaka jamii kuchangia katika mifuko ya Afya ya Jamii (CHF)” Alisema Mtaturu

Katika Mfuko wa Afya  (CHF) Kaya moja itatakiwa kuchangia Tsh. 10,000/= na atatibiwa Baba, Mama na Watoto wanne kwa mwaka mzima, hivyo Mwananchi akiuza kuku mmoja tu anatosha kumtibia yeye mwenyewe na familia yake kwa mwaka mzima.

Mwananchi asipojiunga na huduma hii atatakiwa kutoa Papo kwa Papo            Tsh. 7,000/= pale anapougua hii elfu saba ni ya kumuona Daktari bila dawa,  Mwananchi huyu akiuguliwa na watu watano, itamlazimu kutoa Tsh. 35,000/= kwa hiyo Mwananchi ambaye hajajiunga na CHF atapata hasara ya Tsh. 25,000/= na wakati mwingine anaweza akauguliwa  akiwa hana hata hela ya kutibiana hatimaye anahatarisha maisha ya watu wake wa karibu.

Dc Mtaturu amewataka Viongozi hao kujitafakari kwa nini waliomba ridhaa ya kuwaongoza Wananchi wa Ikungi, kama waliomba nafasi hiyo kwa ajili ya kuwatumikia Wananchi lakini kwenye Kata zao Shule za Sekondari hazina Maabara, hakuna Zahanati na Kituo cha Afya, hakuna barabara, hakuna huduma ya maji safi na salama na hakuna Shule; Wanafunzi wanatembea umbali mrefu kufuata Shule na hawana mpango wowote ule wa kusogeza karibu huduma hizi basi wanatakiwa kujitafakari upya.

Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kushirikiana na kila Kiongozi bila kujali itikadi ya Chama chake, Dini yake au rangi yake katika kuwaletea maendeleo Wananchi wa Ikungi.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya Madiwani wote kwa hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii ambaye ni Diwani wa Kata ya Issuna  Steven Misai amesema kuwa Hotuba ya Mkuu huyo inaonyesha taswira mpya ya kuinusuru Wilaya hiyo katika sekta ya elimu, afya, na miundombinu.

Missai alisema kuwa maagizo ya hotuba yake yatafanyiwa kazi na madiwani wote ili kuifanya wilaya ya Ikungi kuwa nguzo katika sekta hizo hususani ujenzi wa maabara.

No comments: